Magereza kuburuzwa kortini?

21Feb 2017
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Magereza kuburuzwa kortini?

MAKANDARASI wadogo waliopewa zabuni na Jeshi la Magereza kukarabati Jengo la Utawala la Bunge, wamekusudia kulishtaki mahakamani jeshi hilo kama litashindwa kulipa Sh. milioni 569.4 wanazozidai.

Makandarasi hao tayari wameliandikia jeshi hilo notisi ya siku 14 yenye kusudio la kuwapeleka mahakamani kupitia wakili wao, Godfrey Wasonga kutoka kampuni ya Nation Attorney ambayo mwisho wa notisi hiyo ni keshokutwa.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa makandarasi hao, Hassan Mvungi alisema makandarasi 17 walifanya kazi hiyo na wanalidai Jeshi la Magereza Sh. 569,399,108 kutokana na kazi ya ukarabati wa Jengo la Utawala la Bunge.

“Tumefikia uamuzi huu kutokana na madai yetu kuwa ni ya muda mrefu na wenzetu wengine wameanza kufilisiwa mali zao kwani walikuwa wamekopa vifaa kwa ajili ya ujenzi,” alisema Mvungi.

Afafanua kuwa ujenzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa Bunge la Katiba mwaka 2014, lakini hadi sasa wamelipwa kiasi kidogo pasipo kufahamu hatima ya fedha hizo wanazodai.

Mvungi alisema waliitwa haraka na kupewa kazi hiyo na kila mmoja alipewa kipande chake cha kukarabati na kuambiwa malipo yao yangekuwa tayari wakati wowote baada ya kukamilisha kazi hiyo.

"Lakini hadi leo tunavyoongea na wewe, tunayumbishwa na hakuna majibu ya uhakika tunayopata,” alisema Mvungi.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Julius Sangudi, alithibitisha kupokea notisi
hiyo.

Hata hivyo, Sangudi alisema wanaotakiwa kufanya malipo hayo ni Magereza Makao Makuu na si mkoa.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, Dk. Juma Malewa, alithibitisha kulitambua deni hilo na kueleza kuwa mipango inafanyika ili makandarasi hao walipwe.

“Nakiri tunatambua tunadaiwa na makandarasi waliofanya ukarabati katika Jengo la Bunge, lakini kwa kweli hiyo notisi ya kusudio la kutushtaki mahakamani, bado sijaipokea,” alisema Kamishna Dk. Malewa.

Habari Kubwa