Magereza yatekeleza agizo la JPM

05Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Magereza yatekeleza agizo la JPM

JESHI la Magereza limeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kuhamisha wafungwa 1,535 kwenda kwenye magereza 10 ya kimkakati kwa ajili ya kuzalisha chakula kutosheleza mahitaji yake na ziada kuuzwa.

Msemaji wa Jeshi hilo, Mrakibu (SP) Amina Kavirondo, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa wafungwa hao wamepelekwa katika magereza hayo ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kutaka rasilimali waliyo nayo  itumike ipasavyo ili kuleta tija na kupunguza utegemezi kwa serikali.

Kavirondo aliyataja magereza walikohamishiwa wafungwa hao kuwa ni Songwe, Kitai, Ludewa, Kitengule, Mollo, Pawaga, Idete, Kiberege, Kitete  na Nkasi. Pia alisema  gereza la Arusha  halikupokea  nguvu kazi  mpya kwa kuwa wafungwa  walioko  wanajitosheleza  katika uzalishaji.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza  katika  Gereza  Kuu  la Ukonga, Dar es Salaam na kuagiza jeshi hilo kujitathmini kwa kuwa  wana rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri, halitakuwa na haja ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Rais Magufuli alisema Magereza  ni kati ya taasisi za serikali zenye maeneo makubwa kuliko taasisi nyingine yoyote ya uzalishaji lakini cha ajabu inasubiri fedha za serikali ili kulisha wafungwa badala ya wafungwa kuzalisha chakula chao na ziada kuuzwa kwa ajili ya kupata fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji mbalimbali na hata kujenga majengo yake yenyewe.

Alisema ni aibu kwa serikali kupanga bajeti ya kulisha wafungwa wakati wafungwa wanaweza kufanya kazi na wakazalisha, hivyo akaagiza wafungwa wafanye kazi kwa kuwa hawafanyi kazi vya kutosha.

Kavirondo alisema yako magereza 11 ya kimkakati ambayo wamepelekewa  wafungwa ambako kuna miradi 23  ya uzalishaji  iliyo chini ya Shirika  la  Uzalishaji la Jeshi la Magereza la Corporation Sole,  ambalo hujishughulisha na  kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda.

Alisema  baadhi ya viwanda vinavyoendeshwa na Magereza ni vile vya usindikaji wa ngozi za  mifugo, utengenezaji wa viatu  kwa ajili ya askari na biashara, uzalishaji kokoto  na ufyatuaji matofali yanayotumia  saruji na udongo.

Pia alisema Jeshi la Magereza lina ardhi yenye ukubwa wa hekta 130,482 na 60,540 kati ya hizo,  zimetengwa kwa shughuli  za kilimo, hekta 3,000 kwa ajii ya makazi, hekta 47,459 malisho ya mifugo  na 50,459 kwa matumizi  mengineyo.

Mpaka sasa Tanzania ina magereza makuu 12, magereza ya wilaya 75 na magereza ya wazi 42 yanye uwezo wa kuhifadhi wastani wa wahalifu 380,000 kwa siku. Kwa sasa jumla ya wahalifu wote wanaoshikiliwa nchi nzima ni 36,544 wakiwamo wafungwa 18,205 na mahabusu 18,339.

Habari Kubwa