Maghembe awachimba mkwara maofisa misitu

20Jun 2016
Beatrice Shayo
Katavi
Nipashe
Maghembe awachimba mkwara maofisa misitu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amewaagiza maofisa misitu kudhibiti ukataji miti na magogo na kamawatashindwa kufanya hivyo, atawafukuza kazi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa kwanza kushoto), akikagua gwaride

Profesa Maghembe alitoa agizo hilo mkoani humu mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo ya kubadili mfumo wa utendaji kazi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kutoka mfumo wa kiraia kwenda mfumo wa jeshi usu.

Katika mafunzo hayo, wahitimu 27 wakiwamo wanawake wanne ambao ni watendaji wa ngazi za juu wa Tanapa, walikuwa wanapatiwa mafunzo ya kijeshi ikiwa ni sehemu ya kupambana na ujangili.

Waziri Maghembe alisema baadhi ya maofisa hao wa misitu wamekuwa wakijiingiza katika mtandao wa uvunaji wa magogo pamoja na ukataji wa miti kwa kwa ajili ya kutengenezea mkaa.

Alisema kwenye mapori yaliyopo katika hifadhi ya taifa kumekuwa na uchomaji wa mkaa ndani ya hifadhi za taifa huku maofisa misitu wakiwapo na hawachukui hatua.

“Lazima mkataze ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa ukubalike ule ambao ni wa matumizi ya nchi, lakini biashara ya mkaa kwenda nje ya nchi hii imekuwa ni kubwa. Ukivuka Ziwa Tanganyika, hakuna miti ya miombo ambayo imesimama, yote imekatwa,” alisema Prof. Maghembe.

Aliongeza: “Wahifadhi watakaoacha hifadhi zao zikatwe miti kwa ajili ya mkaa, naye ajiandae kuchomwa.”
Alisema watu wasichome mkaa bila kuwa na kibali na ni marufuku kutolewa kwa leseni kwa kila mtu kwani suala hilo linasababishia mkaa kusafirishwa nje ya nchi.

Aidha, Prof. Maghembe alisema uvunaji wa magogo umeshamiri akitolea mfano msitu wa Sikonge uliopo mkoani Katavi umeisha huku maofisa misitu na wahifadhi wakiwapo na mwisho wa mwezi wanapokea mshahara.

“Nyie ndiyo wahusika wakuu wa kufanya biashara ya kusafirisha magogo hata wafanyakazi wa misitu wanaokaa barabarani wakiwasimamisha wanaopitisha magogo, ninyi hupiga simu na kuwaambia `muache huyo apite," alisema Profose Maghembe.

Aidha, alisema aliwataka wananchi kufuata sheria za uhifadhi inayokataza kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi.

Aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanapambana na majangili ipasavyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema lengo la mafunzo hayo ni kujenga nidhamu ya utendaji kazi hasa katika uwindaji haramu na ujangili.

Alisema wamejipanga uhakikisha hifadhi za taifa zinalindwa bila kutetereka pamoja na kutatua tatizo la ujangili ili watalii wafurahie vivutio vya hifadhi za hapa nchini.

Meneja wa Pori la Akiba la Rukwa/Lwafi, Said Bilibili, alisema wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa wa fedha ukilinganisha na mahitaji, uchakavu na upungufu wa vitendea kazi, kukosekana kwa mawasiliano, ubovu wa miundombinu ya barabara zilizopo ndani ya pori, ukosefu wa nyumba kwa watumishi na uwindaji haramu wa wanyamapori.