Magufuli aagiza maeneo matatu kupatiwa maji Desemba

13Oct 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli aagiza maeneo matatu kupatiwa maji Desemba

RAIS John Magufuli amemwagiza Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, kuhakikisha maeneo ya Kinyerezi, Bonyokwa na Kifuru, jijini Dar es Salaam yanapata huduma ya majisafi na salama ifikapo Desemba, mwaka huu.

Alitoa agizo hilo jana wakati akiwa katika mkutano wa kampeni kwenye kata ya Kinyerezi wilayani Ilala, alipokuwa akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kama kuna Waziri wa Maji ananisikia basi anisikie vizuri, hii ni amri ya John Pombe Joseph Magufuli, hayo maeneo ya Kinyerezi, Bonyokwa na Kifuru, waanze kunywa majisafi na salama ifikapo Desemba, mwaka huu,” alisema.

AELEZA CHANGAMOTO

Aidha, alieleza changamoto alizokutana nazo wakati akiingia madarakani mwaka 2015, mojawapo ikiwa ni kuhakikisha vitendo vya ujambazi vinatokomea katika Jiji la Dar es Salaam.

“Niliupata urais bila ya kutumwa na mtu, wala kuhonga. Nilipoingia madarakani nilikutana na changamoto ikiwamo baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kutokuwa na amani, polisi waliuawa Kibiti, mkoani Kigoma watu walikuwa wanatekwa, wanauawa, Ubungo mchana majambazi walivamia benki na kupora fedha. Nikasema nitakomesha,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Jiji la Dar es Salaam lilikuwa limekithiri matukio ya ujambazi, wafanyabiashara wa maduka walikuwa wanavamiwa na kuporwa mali zao mchana.

“Yaani jambazi alikuwa anakupigia simu anakuambia leo nakuja kuchukua pesa na kweli anakuja na kupora. Nikasema jambo la kwanza ni kujenga amani ya Watanzania, na hili tumelifanya vizuri japokuwa bado kuna changamoto,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema kila kitu katika Jiji la Dar es Salam kilikuwa ni shida, ikiwamo wajasiriamali kuteseka na kwamba alianza kujenga ‘fly over’ pamoja na barabara.

“Wajasiriamali waliteseka, kila sehemu walikuwa wanafukuzwa, ndiyo maana nikaamua kuwatengenezea vitambulisho kwa gharama ya Sh. 20,000 kwa mwaka, awali walikuwa wanalipa Sh. 1,000 kwa siku. Leo wanafanya biashara kwa uhuru, hawabugudhiwi,” alisema.

Alifafanua kuwa dhamira ya serikali ni kuona Watanzania wanakuwa na maisha mazuri kwa kupata huduma bora za kijamii, ikiwamo kushusha bei ya umeme miaka ijayo.

“Ninataka bei ya umeme ishuke iwe kama kwao (Ulaya). Ila nawashangaa baadhi ya Watanzania wanazunguka Ulaya wanasema Tanzania inyimwe mikopo, wanatutukana. Nawaomba Watanzania muwapuuze.”

Aliwataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kumpigia kura nyingi ili awe Rais kwa awamu ya pili na kwenda kutekeleza mambo ambayo bado hajayatimiza.

Habari Kubwa