Magufuli aahidi kutatua kero sugu 12

17Sep 2020
Gwamaka Alipipi
Bukoba
Nipashe
Magufuli aahidi kutatua kero sugu 12

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Kagera kutatua kero sugu 12, zilizokuwa zinawasumbua kwa muda mrefu, mojawapo ni kukatika kwa umeme kila wakati.

Akiwa katika viwanja vya Gymkhana mkoani Kagera jana, Dk. Magufuli aliwahidi kuwatatulia kero hizo ambazo zimewatesa kwa muda mrefu, ndani ya miaka mitano ijayo, zingine hivi karibuni.

UJENZI WA STENDI

Akiwa katika viwanja hivyo, Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi na wa Manispaa ya Bukoba kuwajengea stendi ya kisasa, ambayo ujenzi wake umekwama tangu mwaka 2014 kutokana na mvutano wa wanasiasa.

“Ndugu zangu nileteeni mbunge Steven Byabato, kwenye kura za maoni alishika nafasi ya nne, lakini tulimchukua kwa sababu tulitaka kuvunja makundi Bukoba. Bukoba tumejichelewesha wenyewe, sasa nileteeni huyo ili stendi hiyo tuikamilishe,” alisema Dk. Magufuli.

SOKO KUBWA

Dk. Magufuli alisema kumekuwa na tatizo la baadhi ya madiwani kulaumiwa kuuza vizimba vya kufanyia biashara, pamoja na wafanyabiashara wadogo kuuziwa kwa gharama kubwa.

Alitoa agizo kwa mamlaka husika kushughulikiwa kwa kero hiyo ndani ya muda mfupi kuanzia sasa.

MGOGORO WA ARDHI

Alisema kumekuwa na mgogoro wa ardhi eneo la Kiebitembe kwa muda mrefu kutokana na viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuuza kiwanja kimoja kwa watu wengi.

“Namuagiza mkuu wa wilaya, maofisa ardhi waanze kushughulikia kero hii sasa hivi, hili zege haliwezi kulala”.

MTO KANONI

Alisema kuwa Mto Kanoni umekuwa ukileta mafuriko ya mara kwa mara kwa wananchi mvua zinaponyesha. Aliagiza mamlaka husika kumaliza tatizo hilo ndani ya muda mfupi.

MGOGORO WAFUGAJI, WAKULIMA

Aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kumaliza tatizo la mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ambao umedumu kwa muda mrefu.

UJENZI BARABARA

Vilevile, aliwaahidi wakazi wa Kagera kuwajengea barabara kutoka Umuru-Shaka-Karagwe hadi mpakani mwa Tanzania na Uganda (kilometa 90).

“Hili naomba mniachie mimi na mbunge wa Kyerwa tutalimaliza. Ni barabara inayounganisha Tanzania na Uganda.”

UJENZI WA MAHAKAMA, HOSPITALI

Kadhalika, aliwaahidi wakazi wa Misenyi kuwajengea mahakama kutokana na wakazi wa eneo hilo kwenda umbali mrefu kupata huduma hiyo. Pia aliwaahidi kuwajengea hospitali ya wilaya.

KUBORESHA MAWASILIANO

Dk. Magufuli alisema katika eneo la Kanyigo, Mabare na sehemu zingine za makao makuu ya wilaya, wananchi wanakabiliwa na tatizo la mtandao wa mawasiliano ya simu.

Aliwahakikishia kumaliza kero hiyo ndani ya muda mfupi.

MALIPO YA KAHAWA

Alisema serikali itakwenda kulivalia njuga na kumaliza tatizo la ucheleweshaji wa malipo ya kahawa kwa wakulima.

“Haiwezekani wakulima wetu walipwe bei ya chini wakati nchi za jirani bei iko juu, ikiwezekana masoko ya nchi za jirani tutayaamishia hapa. Ninawahakikishia tutalipa madeni yote. Serikali ya CCM haiwezi kuwa ya kudhulumu, kama tulivyofanya kwenye pamba na korosho, ndivyo tutafanya kwenye kahawa.”

KERO YA MAJI

Alisema katika kipindi cha miaka ijayo, serikali itamaliza tatizo la upatikanaji wa maji.
Katika kuhakikisha hilo, alisema serikali kwa sasa imeanza kutekeleza baadhi ya miradi ya maji na ifikapo Novemba, mwaka huu baadhi ya maeneo yatakuwa yameanza kupata maji.

“Tunataka maeneo ya mjini upatikanaji wa maji ufikie asilimia 87.6. kwa miaka mitano tumeshatekeleza miradi mingi yenye thamani ya Sh. bilioni 50.17.”

KUKATIKA KWA UMEME

Alisema mkoa wa Kagera unakabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme kila wakati, pamoja na kutegemea kutoka nchi za jirani, hivyo serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi, mojawapo ni kupata umeme kutoka katika maporomoko ya Mto Lusumo, Kakono yatakayokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 87.

Pia mradi wa bwawa la Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme zaidi ya megawati 2,115 litasaidia kupatikana kwa umeme wa uhakika nchini.

Mbali na kutoa ahadi ya kutatua kero hizo, Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo itahakikisha inavifufua viwanda vilivyokufa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Alisema viwanda vya kilimo, nyama na maziwa, uvuvi, mazao mbalimbali vitapewa kipaumbelea katika kuviendeleza.

Habari Kubwa