Magufuli aanika mitihani Mashariki

25Apr 2018
Romana Mallya
Nipashe
Magufuli aanika mitihani Mashariki

RAIS John Magufuli, ametaja changamoto tano ambazo ni kikwazo cha maendeleo ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwamo vikwazo vya biashara na uwekezaji na kutaka Bunge hilo lizifanyie kazi.

Rais Magufuli alitaja changamoto hizo jana mjini Dodoma wakati akilihutubia Bunge la nne la Afrika Mashariki na kutaja changamoto ya kwanza ni vikwazo vya biashara na uwekezaji.

Pia alisema changamoto nyingine ambayo nchi hizo zinapaswa kupambana nayo ni migogoro ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu wengi. “Changamoto nyingine ni kutokuaminiana ndani ya wanachama wa Afrika Mashariki, mara nyingi huwa hatupendi kuyasema sema haya, nayasema myabebe, mjue hizo changamoto zipo,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli alisema umoja ndani ya nchi hizo unatakiwa uwe kama walivyo maraisi, mawaziri, wabunge, watendaji na wananchi.

“Nyinyi kama wabunge wawakilishi wa nchi mnazotoka mna jukumu kubwa, ifike mahali sisi tupendane, tujione ndugu, nilikuwa naangalia namna mlivyokaa, nilitegemea kuwe na makundi ya watu wa aina fulani au wa kutoka nchi fulani, lakini mmechanganyika,” alisema na kuongeza:

“Muendelee hivyo hivyo, tukianza sisi kuwa na changamoto tutashindwa kuwasaidia tunaowangoza, jumuiya ni ya wananchi siyo viongozi.”

Rais Magufuli alitaja changamoto nyingine ni ukosefu wa viwanda licha ya nchi hizo kuwa na utajiri wa rasilimali.

Alisema moja ya mambo yanayosababisha hayo yote ni kukosekana kwa viwanda vingi kwenye nchi hizo na matokeo yake zimekuwa zikiuza rasilimali nyingi nje ya nchi zikiwa malighafi, hali ambayo inazikosesha mapato mengi. 

Habari Kubwa