Magufuli afichua siri  kubeba Jumuiya Wazazi

13Dec 2017
Augusta Njoji
Nipashe
Magufuli afichua siri  kubeba Jumuiya Wazazi

RAIS John Magufuli amefichua siri ya mgawanyiko ndani ya jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho huku akibainisha kuwa Wazazi pekee ndiyo iliyosimama imara na kuahidi kutoitupa. 

Wakati akiahidi hayo, Magufuli alishamteua Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo anayemaliza muda wake, Abdallah Bulembo, kuwa Mbunge. 

Akifungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi jana mjini hapa, Rais Magufuli alisema jumuiya hiyo ndiyo pekee iliyobaki na msimamo wakati zingine (Vijana na Wanawake) zikiyumba baada ya kuteuliwa wagombea wa CCM katika kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2015. 

Licha ya kutokuyumba, alisema jumuiya hiyo ilisimama kidete kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi mkuu wa 2015 na kuahidi kutoitupa kutokana na msimamo huo. 

“Kikubwa kwa Jumuiya ya Wazazi na ninataka niliseme wazi baada ya kuteuliwa majina ilibaki na msimamo, jumuiya zingine mnafahamu kilichoendelea, zilibebwa kutokana na kutosimama imara,” alisema Rais Magufuli na kueleza zaidi:

“Namfahamu Bulembo kwa asilimia nyingi, namfahamu ni mkweli na ninajua katika kuzunguka kwake na mimi alitengeneza maadui. 

"Baada ya hapo amechekwa kweli, lakini nakushukuru (Bulembo) kwa kuwa mvumilivu. Unachekwa kwa ajili ya CCM, lakini nashukuru kwa sababu nilimwelewa na ninamwelewa na najua na yeye ananielewa.”

Kuhusu ubunge wa viti maalum, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alikubali ombi la jumuiya hiyo la kuwa na uwakilishi sawa wa wabunge kutoka jumuiya zote za chama hicho ndani ya Bunge. 

“Kama Jumuiya ya Vijana wako watano kwa nini Wazazi aingie mmoja? Hii nitaifuta tutaenda pasu kwa pasu. Nitaangalia taratibu zote zinavyoenda kwa jumuiya zote hizi (Wazazi, Vijana na Wanawake). Mimi Mwenyekiti wenu nitahakikisha zote ziko sawa sawa,” alisema.

Magufuli aliwahakikishia wajumbe wa mkutano mkuu huo kuwa jumuiya hiyo haitafutwa wakati yeye akiwa kiongozi kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya chama na ustawi wa taifa.

“Jumuiya hii ilianza 1955, aliyeianzisha ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere… nitakosa busara na nitalaaniwa ikiwa siku moja jumuiya hii itapotea kwenye mikono yangu,” alisema.

Rais Magufuli alisema jumuiya hiyo ina wanachama takribani milioni mbili ambao ni mtaji mkubwa kwa CCM na ina zaidi ya matawi 23,000 ambayo yamesambaa nchi nzima.

KUPATA WANAFUNZIRais Magufuli alisema kuna changamoto katika utoaji wa elimu kwenye shule zilizo chini ya Jumuiya ya Wazazi kutokana na sera ya elimu bure na uwapo wa shule za serikali zinazotoa elimu bure, hivyo kuwa vigumu kwa shule zingine za kulipia kupata wanafunzi, zikiwamo za wazazi.

“Imekuwa changamoto kubwa na ninaambiwa shule za wazazi zipo takribani 54. Mwaka jana tulipoenda Kagera baada ya tetemeko la ardhi nilitembelea Shule ya Omumwani na nikaona inavyotoa huduma nzuri kwa wanafunzi waliokuwa shule zao zimeanguka. Napenda nishukuru jumuiya mlikubali kupokea wanafunzi,” alisema.

Alibainisha kuwa aliomba kuichukua shule hiyo iwe ya serikali na jumuiya hiyo ilikubali na kwamba wiki iliyopita, serikali imelipa Sh. bilioni 1.7 na kuagiza fedha hizo zitumike kuwekeza katika miradi ya jumuiya hiyo.

“Uongozi utakaokuja kama mtaona inafaa kwa baadhi ya shule ambazo mmeshindwa kuziendesha na hasa shule hizi 54 mkaamua shule 20 zichukuliwe na serikali, tutazichukua na tutawalipa fedha ili mkafanye miradi mingine kwa manufaa ya Jumuiya ya Wazazi,” alisema Magufuli.

Awali, Bulembo alisema wakati akiingia madarakani aliikuta jumuiya hiyo haina hata senti moja lakini kwa sasa ameiacha ikiwa na Sh. bilioni 2.5.

Pia alisema nafasi za wanawake ndani ya chama si za Umoja wa wanawake (UWT) peke yao bali ni za CCM na kumwomba mwenyekiti huyo wa taifa wa CCM awaongezee nafasi za uwakilishi bungeni.

“Hatutaki tulingane nao, tunataka tuongezewe na sisi wazazi kuwa na nafasi nane angalau kama ilivyo kwa Umoja wa Vijana (UVCCM),” alisema Bulembo.

Habari Kubwa