Magufuli agonga kengele shule aliyosoma watoke

10Jan 2017
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Magufuli agonga kengele shule aliyosoma watoke

RAIS John Magufuli jana aligonga kengele ili kuwatoa darasani awasalimie wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Chato alipofanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.

Kabla ya kufika katika shule hiyo ambayo alisoma kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, Rais Magufuli alitembea na wasaidizi wake kwenda benki ya CRDB iliyopo umbali wa mita takribani 100 kutoka nyumbani kwao kisha kuwatembelea wasafisha viatu.

Rais Magufuli alipata elimu ya msingi katika shule hiyo kuanzia mwaka 1967 hadi 1974 kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika Seminari ya Katoke ambayo iko Biharamulo mkoani Kagera na baadaye Sekondari ya Lake jijini Mwanza kati ya mwaka 1975 na 1978.

Akiwa na wasafisha viatu hao, Rais alisafisha viatu vyake na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwapo eneo hilo kilipokuwa kituo cha zamani cha magari kisha kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu hao ili kuongeza mtaji wa biashara yao.

Baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Chato, Rais aligonga kengele kuwatoa darasani walimu na wanafunzi na kuzungumza nao.

Rais Magufuli aliahidi kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu kufuatia ombi la walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa kulinganishwa na idadi ya wanafunzi waliopo.

Pia aliwataka wanafunzi kutilia mkazo masomo ili wafaulu na kuwataka walimu kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na serikali kila mwezi katika kutoa elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa kama ilivyo kwa baadhi ya shule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chato, Mwita Chacha, alimshukuru Rais Magufuli kwa msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa na pia kuitembelea shule yao kuwatia moyo walimu na wanafunzi.

KUSHEREKEA MAPINDUZI SHINYANGA

Katika hatua nyingine, Rasis Magufuli anatarajiwa kufanya ziara mkoani Shinyanga keshokutwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, alisema kuwa katika ziara hiyo, Rais pamoja na mambo mengine, atazungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

"Natoa taarifa hii kwa waandishi wa habari ili muuhabarishe umma kuwa kutakuwa na ugeni mkubwa mkoani Shinyanga kwa kutembelewa na Rais wetu John Magufuli,” alisema Telack.

Mkuu wa Mkoa huyo alitumia fursa hiyo kueleza kuwa mkoa wa Shinyanga hauna njaa, isipokuwa Wilaya ya Kishapu ambayo imekumbwa na changamoto hiyo kutokana na ukame.

Aliwataka wakazi wa mkoa huu kuendelea kuhifadhi chakula cha akiba walichonacho kwa kuwa tayari kuna dalili ya uhaba wa mvua mwaka huu unaoweza kusababisha baa la njaa.

*Imeandikwa na Daniel Limbe (CHATO) na Marco Maduhu (SHINYANGA)

Habari Kubwa