Magufuli amfuta machozi kwa mil.5/- aliyefiwa na mama mzazi

12Aug 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli amfuta machozi kwa mil.5/- aliyefiwa na mama mzazi

RAIS John Magufuli, jana alimfuta machozi mama aliyefiwa na mama yake mzazi na kushindwa kumudu gharama za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Ikiwa kama ni muujiza, mama huyo aliyekuwa kwenye korido za kutokea Wodi ya Mwaisela alikuwa amekaa chini na alipomwona Rais anapita alinyoosha mkono akilia kuomba msaada.

Rais Magufuli alisimama kumsikiliza mama huyo ambaye alipaza sauti kueleza msaada anaohitaji na ndipo Rais alimfuta machozi mama huyo.

“Baba nimefiwa na mama yangu, hapa nilipo sina baba sina mama, alisema na Rais Magufuli  alimuuliza mama amefariki lini?

“Mama amefariki saa sita usiku wa leo sina hela za kuchukua mwili,” alisema huku Rais akimuuliza unadaiwa shilingi ngapi? Na kabla hajajibu karatasi ya bili aliyokuwa nayo ilichukuliwa na Meneja Mawasiliano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Eligeisha, ambaye alitaja kiwango cha fedha.

Baada ya kutajwa kiwango hicho mama huyo alisikika akisema: “Ninadaiwa shilingi milioni tano ambazo sijawahi kuzishika toka nizaliwe, nisaidie baba.”

Aidha, Rais alimgeukia Mkurugenzi Mtendaji wa (MNH), Prof. Lawrence Museru, na kumwambia:  “Profesa mshughulikie hii halafu mtanidai mimi.”

Baada ya maelekezo hayo Rais alimgeukia aliyefiwa na kusema: “Mama hii hapa Sh. 500,000 ikusaidie mama.”

Habari Kubwa