Magufuli apeleka neema Dangote

06Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
MTWARA
Nipashe
Magufuli apeleka neema Dangote

RAIS John Magufuli ametoa siku saba kuanzia jana kwa Wizara ya Nishati na Madini kuwa imemega mgodi wa makaa ya mawe katika eneo la Ngaka, wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na kuipa kampuni ya Dangote.

Rais John Magufuli akiwa na mkoani Mtwara.

Eneo hilo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jana ilisema, litakabidhiwa kwa kampuni hiyo ili ichimbe yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo mkoani Mtwara.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa kurugenzi hiyo, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa malori 580 ya Dangote kwa ajili ya kusafirisha saruji yake nchi nzima.

Wakati Rais Magufuli akitoa agizo hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na mmiliki wa kiwanda, Alhaji Aliko Dangote walikuwapo, taarifa ilisema.

Mbali na kuagiza kampuni ya Dangote ipatiwe eneo la kuchimba makaa ya mawe, Rais Magufuli pia aliitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo.

Lengo la kutaka gesi ifikishwe kiwandani hapo mapema iwezekanavyo, ilisema taarifa, ni ili kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.

Aidha, Rais Magufuli alirudia wito wake kwa Dangote wa kuwasiliana moja kwa moja na serikali inapohitaji huduma yoyote badala ya kuwatumia watu wa kati.

Watu wa kati, alisema Rais Magufuli kwa mujibu wa taarifa hiyo, wamekuwa wakisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na bidhaa na hivyo kuathiri uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho.

MALORI MAPYA
Kabla ya kuzindua rasmi malori hayo, Rais Magufuli alipokea kero za madereva ambao walifanya usaili miwili iliyopita baada ya kuomba kazi, taarifa ilisema, ambao walilalamika kutoitwa kazini.

Madereva hao pia walimueleza Rais kushangazwa na menejimenti ya kiwanda hicho kuendelea kutumia malori ya watu binafsi kupitia kampuni za kati ambazo ndizo zimekuwa zikitumika kutoa huduma nyingi kwa kiwanda, taarifa ilisema.

Kufuatia malalamiko hayo, taarifa ya Msigwa ilisema zaidi, Rais Magufuli alimshauri Alhaji Dangote kuiangalia vizuri menejimenti yake.

Alhaji Dangote, taarifa ya Ikulu ilisema, aliahidi uzalishaji kiwandani hapo kufikia tani milioni tatu mwakani, kuzalisha ajira 20,000 na kusaidia kupunguza bei ya saruji nchini kutoka Sh. 15,000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufikia Sh. 10,000.

Habari Kubwa