Magufuli apiga chini fidia kwa watu 34

06Mar 2017
Said Hamdani
LINDI
Nipashe
Magufuli apiga chini fidia kwa watu 34

RAIS John Magufuli, amezuia kulipwa fidia ya nyumba za watu 34 waliojenga eneo lilitengwa kwa ujenzi wa kituo cha magari katika Kijiji cha Nangurukulu Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Badala yake, Rais Magufuli ameagiza zilipwe fidia kaya nne tu ambazo zilikuwapo kabla ya kuwapo kwa mpango wa ujenzi wa kituo hicho.

Alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo mwishoni mwa wiki.

Rais Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya wananchi kulalamikia ucheleweshaji wa ujenzi wa kituo hicho kijijini hapo licha ya mpango huo kuwapo kwa muda mrefu, lakini hakuna utekelezaji.

Wakiwasilisha kilio chao hicho kupitia kwa Mbunge wao, Selemani Bungara (Bwege), wananchi hao walimuomba Rais Magufuli kulipatia ufumbuzi suala hilo kwani tangu mchakato wake ulipotangazwa na uongozi wa wilaya hiyo, hakuna kinachoendelea kufanyika.

Papo hapo Rais Magufuli alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Zabron Bugingo, kumpatia maelezo juu ya madai hayo na sababu zinazochangia ucheleweshaji.

Bungingo alimweleza Rais Magufuli kuwapo ongezeka la idadi ya waathirika baada ya kusikia eneo hilo linahitajika kwa kazi hiyo.

“Mheshimiwa Rais, tatizo lililojitokeza ni ongezeko la idadi ya watu. Kwani tulipoanza kulikuwa na kaya nne tu, lakini baada ya kusikia mpango wetu huu, idadi imeongezeka na kufikia watu 38 wanataka nao walipwe fidia,” alisema Bugingo.

Baada ya maelezo hayo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kilwa, Rais Magufuli alimuagiza kulipa fidia kwa kaya hizo nne tu.

Aidha, Rais Magufuli aliwataka wakazi 34 walioongezeka kubomoa wenyewe majengo yao ili kupisha ujenzi wa kituo hicho vinginevyo zitavunjwa chini ya usimamizi wa vyombo vya dola.

Rais Magufuli alisema serikali anayoingoza haitakuwa tayari kuona mtu au kundi la watu linazuia kufanyika kwa kazi ya maendeleo.

“Ninachohitaji mimi ni kuona heshima ya wana-Kilwa inarejea upya. Hivyo mkuu wa mkoa na wilaya, simamieni hilo,” alisisitiza Rais Magufuli akimaanisha Kilwa ya miaka 600 iliyopita.

Awali, akiwasilisha kilio cha wapigakura wake, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Bungara, alimuomba Rais Magufuli kuwategulia kitendawili kinachozuia kufanyika kwa ujenzi wa kituo cha magari katika kijiji hicho.

Habari Kubwa