Akizungumza katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma leo, Rais John Magufuli amesema kuwa wagombea wote wa Ubunge waliojitokeza katika Chama cha Mapinduzi (CCM) ni 10,367 na waliotimiza vigezo ni 10,321 na kutaka kutumika kwa mfumo uliotumia kuhesabu kura za wagombea urais katika kuhesabu kura za maoni za wagombea wa nafasi hiyo.
“Haijawahi kutokea kwamba wagombea katika chama kimoja kwenye kiti tu cha Ubunge wawe 10,367 na mimi nawapongeza sana wote waliojitokeza kwenda kuomba nafasi mbalimbali kupitia chama chetu ni matumaini yangu kuwa watakaosimamia kura za maoni watasimamia kwa uwazi bila mizengwe yoyote” amesema Rais Magufuli.
Chama cha Mapinduzi kinatarajia kufanya mchujo kwa wagombea wote wa ubunge leo na kesho kwa kupitisha majina yatakayokwenda kamati ya mkoa na baadaye taifa ili kupata jina moja la atakayegombea kwa tiketi ya chama hicho.