Magufuli ateua DC mpya Ilala

10Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli ateua DC mpya Ilala

RAIS John Magufuli amemteua, Ng’wilabuzu Ludigija, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi huo, Ludigija alikuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, na anachukua nafasi ya Mussa Chogelo, ambaye amepangiwa kazi maalum katika Ofisi ya Rais.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu ya Chamwino, Gerson Msigwa, ilisema kufuatia uteuzi huo, Rais Magufuli amemhamisha kituo cha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi, Erasto Kiwale ambaye anakwenda kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam.

Kiwale anachukua nafasi ya Ludigija ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Catherine Mashalla kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Kabla ya uteuzi huo, Mashalla alikuwa Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam, na anachukua nafasi ya Kiwale ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.

Taarifa hiyo ilisema uteuzi na uhamisho wa viongozi hao umeanza jana.

Habari Kubwa