Magufuli ateua RC 2, DC 9 Gondwe aletwa Temeke

03Jul 2020
Dotto Lameck
Dodoma
Nipashe
Magufuli ateua RC 2, DC 9 Gondwe aletwa Temeke

RAIS Dk John Magufuli, amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa wawili na Wakuu Wilaya tisa ni kutokana na baadhi ya viongozi kustaafu huku wengine wakibadilishiwa maeneo ya kazi.

RAIS Dk John Magufuli.

Magufuli amefanya uteuzi huo leo Julai 3, Mwaka huu Jijini Dodoma.

Magufuli amemteua Thobias Andengenye, aliyewahi kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushika nafasi ya Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga ambaye amemaliza muda wake.

Pia Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Dk Philemon Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora ambapo nafasi hiyo ilishikiliwa na Aggrey Mwanri ambaye amemaliza muda wake.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SAPC), Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Dodoma ambapo kabla ya uteuzi huo nafasi hiyo ilishikiliwa na James Mugendi Ihunyo.

Naye Jamila Yusuph, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi ambapo amechukua nafasi ya Lilian Charles Matinga ambaye amemaliza muda wake.Kabla ya uteuzi huo Jamila Yusuph alikuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo.

Mhandisi Martine Ntemo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ambapo ameshikia nafasi ya Asumpter Nshunju Mshama ambaye amestaafu, nna kabla ya uteuzi huo Ntemo alikuwa Mhandisi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Naye Salum Kali ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo. Kali amechukua nafasi ya Dkt. Philemon Sengati ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Magufuli pia amemteua Wilson Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya Nyang’wale mkoani Geita ambapo kabla ya uteuzi huo Shimo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida.

Kanali Mathias Kahabi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera ambapo kabla ya uteuzi nafasi hiyo ilishikiliwa na Saada Malunde ambaye amestaafu

Abbas Kayanda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu. Kayanda amechukua nafasi ya Theresia Mahongo ambaye amestaafu.

Rais amemteua Lazaro Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara ambapo amechukua nafasi ya Elizabeth Kitundu ambaye amemaliza muda wake.

Na mwisho kabisa Rais Magufuli amemteua Toba Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambapo awali nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Godwin Gondwe ambaye amehamishwa kituo na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam. Naye Godwin Gondwe amechukua nafasi ya Felix Lyaniva ambaye amemaliza muda wake.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wateule wote kufika Ikulu jijini Dodoma tarehe 6, Julai Mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi.

Habari Kubwa