Magufuli, Kenyatta waagiza mawaziri

21May 2020
Na Mwandishi Wetu
Singida
Nipashe
Magufuli, Kenyatta waagiza mawaziri

MARAIS John Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya, wamewaagiza mawaziri wanaohusika na uchukuzi na wakuu wa mikoa iliyoko katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya, kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo.

Rais Magufuli alisema hayo jana, alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Singida akiwa safarini kutoka Chato mkoani Geita kwenda makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Siku chache zilizopita umeibuka mgogoro katika vituo vya mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro baada ya malori ya mizigo ya kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa madai ya madereva wanaopimwa kukutwa na maambukizo ya virusi vya corona.

Rais Magufuli alibainisha kwamba, Rais Kenyatta alimpigia simu juzi na jana, na katika mazungumzo yao, amempa pole kutokana na msiba wa dada yake na pia wamekubaliana kuwa viongozi wa pande zote mbili wanapaswa kukutana na kuutatua mgogoro huo haraka iwezekanavyo ili Watanzania na Wakenya waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.

Alisema kwamba kuzuiwa kwa malori ya Tanzania yanayokwenda Kenya ama kuzuiwa kwa malori ya Kenya kuja Tanzania hakukubaliki.

“Haiwezekani madereva wetu wote wawe na corona, haiwezekani magari ya Tanzania yakwamishwe kwenda Kenya na magari ya Kenya yakwamishwe kuja Tanzania, tunataka tuutumie mpaka huu kufanya biashara sisi na ndugu zetu Wakenya, tusichonganishwe na corona," Rais Magufuli alisisitiza.

Aliwataka viongozi wa pande zote mbili waweke maslahi ya Tanzania na Kenya mbele, waache kuamua mambo kwa jazba na akaagiza wakuu wa mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge, kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika ndani ya wiki moja.

Rais Magufuli pia aliwapongeza wananchi wa Singida kwa kuchapa kazi na kujenga mkoa wao ambao umepiga hatua kubwa za kimaendeleo na akawataka waendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa hasa kuzalisha mazao ya chakula.

Baada ya kusikiliza kero za wananchi, Rais Magufuli alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, kushughulikia haraka mgogoro wa ardhi kati ya familia ya Mzee Masoud na wamiliki wa Sekondari ya Al-Azhary na pia akaagiza vyama vya ushirika vinavyonunua mazao ya wakulima, kuhakikisha vinawalipa fedha zao badala ya kuwakopa.

Kabla ya kufika Singida, Rais Magufuli alikutana na wananchi wa Nzega mkoani Tabora na kuwapongeza kwa kupata maji kupitia mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria ambao kwa sasa upo katika hatua ya majaribio, na akaahidi kuwa serikali itaendelea kushughulikia tatizo la maji katika mkoa huo.

Rais Magufuli alisisitiza Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona (Covid-19), lakini wasikubali kujazwa hofu kiasi cha kuathiri maisha yao na kwamba hiyo ndiyo sababu serikali iliamua kutowafungia wananchi majumbani (lockdown) wala kufunga mipaka.

Habari Kubwa