Magufuli, Kenyatta watema nyongo

06Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli, Kenyatta watema nyongo

RAIS John Magufuli na mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wamesema watu wa nchi hizo ni ndugu na kamwe hawezi kutokea mtu wa kuwagawa.

Marais hao waliyasema hayo jana wilayani Chato mkoani Geita baada ya Rais Kenyatta kuwasili Tanzania kwa ziara binafsi ya siku mbili.

Akizungumza na Watanzania, Rais Kenyatta alisema: “Unajua wanasiasa shida yao wengine wanaongea bila kufikiria. Mtu anajiona mahali ameishi hajatoka kijijini kwake anafikiri ndiyo mwisho wa dunia.

“Wengine wanaropoka mambo hayapo. Unawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kufanya biashara Kenya? Wawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kutembea Kenya? Wawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kwenda kutafuta bibi (mke) Kenya, inawekezana kweli?” alihoji.

Pia Kenyatta alisema mtu hawezi kumzuia Mkenya kwenda Tanzania kufanya biashara yake,  kwenda kumtembelea jirani au rafiki yake au akiwa amemwona mtoto Chatu.

“Hii ndiyo Afrika Mashariki ambayo tunaitaka,  siyo ya watu wenye fikra ndogo za zamani za kikabila na za ujinga,” alisema.

Rais Kenyatta alisema yupo Tanzania kwa sababu ya uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizo mbili.

“Tupo hapa kwa sababu ya uhusiano mwema. Kama nchi jirani, Mungu alituambia ya kwamba waweza kuchagua rafiki, lakini si jirani, jirani ni yule Mungu amekupatia, hakuna kitu kizuri kama furaha, una jirani uliyechaguliwa na Mungu lakini huyo jirani ni rafiki,” alisema.

Kenyatta alisema wapo hapo ili kuimarisha urafiki huo, kusisitiza kuwa mataifa hayo mawili yamebarikiwa na Mungu kwa rutuba na mali nyingi.

“Tuna wananchi wema, wanajuana, tunazungumza lugha moja, uende Namanga hawa ni majirani kwa lugha ya jirani na kitaifa, ufike upande wa Pwani ni ndugu na jamii moja,” alisema.

“Je, wanaweza kututenganisha sisi kweli? Hawawezi.  Ndipo sisi kama watoto wa Afrika Mashariki tunasema tunastahili tuwe kama sisi, viongozi tunafanya yote tunayoweza kuhakikisha tunaondoa vikwazo vyote ambavyo vinazuia watu wetu kutembeleana, kufanya biashara pamoja na kuoana,” aliongeza.

Pia alisema njia ya kumaliza ukabila na mipaka ni watu waoane ili mtoto akizaliwa asijue kama kwao ni Tanzania au Kenya bali mwana Afrika Mashariki.

 “Nikiwa kiongozi wa Kenya ninasema kama kuna kitu ningependa kuona kabla wakati wangu kuisha ni sisi wana Afrika Mashariki tunakuwa kitu kimoja,” Kenyatta alisisitiza.

Rais Kenyatta alisema wakati anashuka kwenye ndege, alimwambia ndugu yake (Rais Magufuli) kuwa yeye ndiye Rais wa kwanza wa nje kukanyaga Chato.

Naye Rais Magufuli alimpongeza Rais Kenyatta kwa hatua alizochukua kwa mtu mmoja ambaye alikuwa na lengo la kuwagawanya raia nchi hizo mbili huku akisisitiza kuwa nchi hizo zina uhusiano mzuri wa kihistoria ambao umekuwapo hata kabla ya ukoloni.

Alisema nchi hizo zinaunganishwa na Ziwa Victoria na Tanzania ina eneo kubwa zaidi wakati Kenya wao wana asilimia tano.

“Samaki wanaweza kutaga mayai Tanzania na kifaranga wakala Kisumu, Kenya. Mtu  anaweza kusafiri kwa ziwa hili kutoka Chato hadi Kisumu, Kenya.

Pia alisema wananchi wa nchi hizo ni marafiki na ndugu ambao wanazungumza lugha moja na wana utamaduni unaofanana na Watanzania wengi Kenya ni nyumbani, vivyo hivyo kwa Wakenya kwa Tanzania.

“Sidhani kama kuna mkoa hakuna Wakenya, kuna wengine wana nyumba kubwa Kenya halafu nyumba ndogo ipo Tanzania,” alisema Rais Magufuli.

Mbali na uhusiano wa wananchi, alisema pia serikali hizo zinashirikiana kupitia ushirikiano wa kibalozi.

“Mwaka 2009 tulianzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya Tanzania na Kenya, tunashirikiana katika nyanja za kimataifa.  Mara nyingi tumekuwa na kauli na misimamo ya aina moja,” alisema.

Rais Magufuli alisema nchi hizo zimeweza kunufaika kiuchumi mathalani biashara ambapo mwaka jana zilikuwa na thamani Sh. trilioni 1.045 ambapo Tanzania iliuza Kenya bidhaa za Sh. bilioni 482.43 na kuagiza zenye thamani ya Sh. bilioni 565 kutoka nchini humo.

Pia alisema takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kenya ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa kuwekeza Tanzania  ambayo ina miradi 504 yenye thamani Dola za kimarekani bilioni 1.7 ambayo imetoa ajira 50,929.

Alisema ikilinganishwa na wawekezaji wa Tanzania walioko nchini humo, wamefungua kampuni 24 zenye thamani ya Dola za kimarekani bilioni 185.

“Wapo Watanzania na Wakenya wanaoshirikiana kwenye miradi mbalimbali ya pamoja, kwa mujibu wa Bodi ya Utalii ya Kenya mwaka jana, Watanzania 220,216 walitembelea nchi hiyo,” alisema.

Rais Magufuli alisema nchi hizo, zimekuwa zikitekeleza kwa pamoja miradi ya maendeleo ikiwamo miundombinu ambapo tayari wamekamilisha barabara kutoka Arusha- Namanga hadi Kenya na kukamilisha vituo vya huduma mpakani.

Alisema kwa sasa wanatekeleza mradi wa barabara kutoka Arusha, Horiri hadi Taveta  pamoja na mradi wa kusafirisha umeme kwa nchi hizo.

Hata hivyo, Rais Magufuli alimweleza Rais Kenyatta kuwa ameweka historia kwa nchi kuwa ya kwanza kufika Chato na alimuhakikishia kuwa ujio wake ameufurahia.

Habari Kubwa