Mahabusi amlipua ofisa Magereza mbele ya JPM

17Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mahabusi amlipua ofisa Magereza mbele ya JPM

THOMAS Nyagombe, mahabusi katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza, amekiweka hatarini kibarua cha Ofisa Usalama wa gereza hilo, baada ya kumweleza Rais John Magufuli mambo mabaya linayoyafanya.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wafungwa, Mahabusu, pamoja na Askari wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Butimba mkoani Mwanza.

Katika ziara yake ya kushtukiza gerezani huko jana, Rais Magufuli alielezwa na mahabusi huyo na wafungwa wengine kuwa wamekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili ukiwamo uonevu wanaofanyiwa na viongozi wa gereza.

Nyagombe alimweleza Rais Magufuli kuwa ofisa huyo amekuwa akishindwa kusimamia usalama wa wafungwa na mahabusi na kusababisha mauaji kutokea katika gereza hilo.

"Gereza hili siyo la amani, kuna mauaji yalitokea wakati ofisa huyu wa usalama akiwa amekaa tu bila shughuli yoyote, mwambie mihuri akupe na simu zote akupe kwa sababu amekuwa akitoa taarifa za uongo," mahabusi huyo alisema.

Nyagombe alimwomba Rais Magufuli kuchukulia hatua za kisheria dhidi ya ofisa huyo kwa kuwa yeye na maofisa wengine wa magereza wana mbinu nyingi za kudhuru wafungwa na mahabusi.

Alizitaja baadhi ya mbinu wanazotumia kuwadhuru wafungwa na mahabusi kuwa ni kushirikiana na madaktari kuwachoma sindano za sumu na kusababisha vifo.

"Mheshimiwa Rais Magufuli, tunakuomba ondoka na huyu mkuu, tunakuomba ondoka naye (ofisa usalama) ili amani iendelee kuwapo, ukimwacha atanidhuru," Nyagombe alisema.

"Wana mbinu nyingi hawa, ngoja nikwambie wakikuona mjuaji wanapanga na daktari, wanakuchoma sindano wanakuua, na si mara ya kwanza kuua watu.

"Nilipanga nije nikuambie mambo yote lakini Mungu katukutanisha nikuambie, nikitoka nitakuletea mambo yote ya jela. Lakini huyu usimwache, ukimwacha, utaandika maelezo ya mauaji, uwiiii!" Mahabusi huyo alisema huku akikatisha maelezo yake na kuketi akiwa ameweka mikono kichwani.

Kutokana na maelezo ya mahabusi huyo, Rais Magufuli alilazimika kumhoji Ofisa Usalama wa gereza hilo ambaye alisema anatimiza wajibu wake vizuri na alishafanya ukaguzi na kuchukua vitu vyote visivyotakiwa kuingia gerezani, zikiwamo simu za mkononi.

Alisema alikusanya simu nne ambazo amezihifadhi Ofisi ya Mkuu wa Gereza na kwamba kazi hiyo amekuwa akiifanya kila siku asubuhi.

Ofisa huyo alijitetea kuwa mahabusi huyo aliamua kueleza mambo ya gereza hilo kwa kutaka kusikilizwa na Rais Magufuli.Sehemu ya mahojiano ya Rais Magufuli na ofisa huyo ilikuwa hivi:

Ofisa: Huyu amesema kwa sababu ni miongoni mwa watu, wanaotaka asikilizwe yeye tu, anakuja na vitu viovu.

Rais Magufuli: Wewe hukutaka nimsikilize? Mbona wewe nimekusikiliza?

Ofisa: Namshukuru Mungu kwa kufanya hivyo, ameeleza ukweli, ameniinua kwa kiasi fulani.

Rais Magufuli: Umejuaje kama amekuinua, nikikung'oa nyota zako hapo atakuwa amekuinua?

Ofisa: Kwamba mimi nafanya... (alikatishwa na Rais)Rais Magufuli: Halafu wewe naona una kiburi.

Ofisa: Hapana mkuu.Rais Magufuli: Unazungumza mbele yangu kuwa huyu amekuinua?

Ofisa: Kwamba nimesikika.Rais Magufuli: Una uhakika gani mimi nitatoka na jibu gani kwako? Yaani unazungumza hivyo mbele yangu?

Ofisa: Nimekosa mkuu.

Rais Magufuli: Kwa hiyo, kuja kwangu hapa ilikuwa ni ili wewe uinuliwe?

Ofisa: Hapana mkuu.

Rais Magufuli: Amekuinua!

Ofisa: Niwie radhi mkuu.

Rais Magufuli: Mkuu wa Gereza...(aliita Rais Magufuli). Mimi nilikuja hapa kusudi huyu ainuliwe?

Ofisa: Nisamehe mheshimiwa.

Ofisa: Nisamehe afande.

Rais Magufuli: Eeeh! Nafikiri unajua nafanya mzaha. 

Awali, Rais Magufuli alisema anafahamu katika gereza hilo kuna simu nyingi, dawa za kulevya aina ya bangi na mali nyingine ambazo zinaingia katika gereza hilo, huku akiahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili askari magereza na wafungwa nchini.

'HATA MIMI MFUNGWA MTARAJIWA'

Hashim Kijuu,  diwani mstaafu wa Kata ya Mbugani, alimweleza Rais Magufuli kuwa wafungwa na mahabusi wengi wamebambikwa kesi.

"Ninaomba mvumilie, hata mimi, hata sisi tuliopo hapa ni wafungwa au mahabusi wa baadaye, kufungwa au kuwa mahabusi, haina maana wewe kutopata haki yako ya utu wa binadamu, ndiyo sababu nimepita hapa leo," alisema Rais.

Kurwa Hemeli, mahabusi katika gereza hilo, alimweleza Rais Magufuli kuwa alikamatwa na mafuta ya dizeli madumu 16, akapelekwa Kituo cha Polisi Nyegezi ambako aliambiwa alipe Sh. milioni moja, lakini akawa na uwezo wa kulipa Sh. 200,000.

Alidai Sh. 200,000 zake zilikataliwa na kwamba askari walimpeleka kituo kikuu cha polisi ambako aliunganishwa na watuhumiwa wengine kwa kosa la mauaji.