Mahakama Kuu yabariki mapitio tozo za miamala

14Oct 2021
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama Kuu yabariki mapitio tozo za miamala

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ifungue maombi ya kuiomba ifanye mapitio ya sheria ya mfumo wa taifa wa malipo pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu.

Kadhalika, mahakama hiyo imesema imeruhusu LHRC kufungua maombi kwa kuwa wamekidhi vigezo vya kufungua maombi hayo kama walivyoomba.

Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji John Mgeta.

Alisema mahakama yake baada ya kusikiliza hoja za LHRC na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, imeona kituo hicho kimetimiza vigezo vinavyotakiwa kufungua maombi hayo.

"Mahakama hii imeruhusu LHRC kufungua maombi yao kwamba wamekidhi vigezo vya kufungua maombi hayo," alisema Jaji Mgeta.

Akifafanua uamuzi wake, jaji alisema LHRC imezingatia kufungua maombi hayo ndani ya muda kama matakwa ya kisheria yanavyotaka, kabla ya miezi sita kupita tangu sheria husika ilipotangazwa.

Alisema sheria ilipotangazwa na waziri Juni 30, mwaka 2021 na LHRC ilifungua shauri hilo Julai 27, 201 na hakuna ubishi hata kwa pande zote mbili kuwa maombi hayo yaliwasilishwa ndani ya muda.

Jaji alisema kigezo cha pili ni kama mleta maombi ana hoja za msingi ambazo anataka zizungumzwe katika maombi yake.

Alisema waliangalia maombi ya LHRC, kiapo na maelezo yanayounga mkono maombi hayo na alikubali kwamba LHRC wana hoja za msingi.

Kigezo cha tatu ni kama mleta maombi ana maslahi katika shauri husika na Jaji alisema kwa mujibu wa kiapo cha mleta maombi imeelezwa kwamba wamiliki simu za mtandao wa Tigo, Airtel na Vodacom ambazo anazitumia kutuma na kupokea fedha na kwamba ameathirika na sheria hiyo.

Jaji alisema kwa maana hiyo anaona mleta maombi ana hoja, anapaswa asikilizwe na LHRC imekidhi vigezo vitatu na ameruhusiwa kuleta maombi yake mahakamani.

LHRC ilifungua shauri hilo dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo LHRC inaomba mahakama ifanye  mapitio kuhusu sheria ya mfumo wa taifa wa malipo pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu.

Shauri hilo lilitokana na kupitishwa kwa mapendekezo ya bajeti ya serikali ya mwaka 2020/2021 na Sheria ya Fedha iliyosababisha kuweka tozo ambayo anaitaja kuwa mzigo kwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara ndogondogo.

Habari Kubwa