Mahakama, polisi, madaktari lawamani

27Feb 2016
Dar
Nipashe
Mahakama, polisi, madaktari lawamani

Idara ya Mahakama, jeshi la Polisi na madaktari wa binadamu wamelalamikiwa kwa kushindwa kuweka mkazo katika kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Edda Sanga.

Udhaifu huo, imeelezwa, husababisha waathirika wa ubakaji na ulawiti kukosa haki mahakami kwa kesi nyingi kutupwa bila kusikilizwa au kuchukua muda mrefu.

Lawama hizo zilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Edda Sanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema Tamwa inasikitishwa na kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto kutokutolewa hukumu hali inayochangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Alisema Tamwa imebaini kuwa kesi 62 za ubakaji zimeshindwa kutolewa hukumu na Mahakama mbalimbali jijini katika kipindi cha mwaka 2014/15 na kwamba kati ya kesi 63 moja tu ndiyo mtuhumiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Alisema kesi 43 bado ziko mahakamani wakati 17 hazijafikishwa na mbili zimefutwa kwa kukosa ushahidi.
“Mahakama zinazolalamikiwa ni Kisutu, Kinondoni, Ilala na Temeke, hospitali ambazo baadhi ya madaktari wanawaomba rushwa waathirika ili wawajazie fomu namba 3 ni Mwananyamala, Ilala na Temeke na wakati mwingine wanapewa fedha wapotoshe ukweli,” alisema.

Alitoa mfano wa kesi ya mtoto wa miaka tisa aliyebakwa ambaye kesi yake imepotoshwa na kuandikwa miaka 19, ambayo iliambatanishwa kwenye jalada lililokwenda kwa mwanasheria wa serikali.

Alisema kesi hiyo haikupelekwa mahakamani kwasababu ilikosa ushahidi.

Akibubujikwa machozi mbele ya waandishi wa habari, mama wa mtoto wa miaka tisa aliyebakwa na baba mwenye nyumba eneo la Kimara alieleza alivyoombwa rushwa ya Sh 30,000 ili asainiwe fomu namba 3.

Alisema alivyoshindwa kufanya hivyo, polisi walibadili fomu hiyo na kusema mtoto huyo hakubakwa licha ya kubainika mtoto ameingiliwa zaidi ya mara moja.

Mtoto huyo alieleza kuwa baba huyo alimbaka na kumpa Sh. 500 na wakati mwingine pipi huku akimtisha asitoe taarifa kwa yeyote na akifanya hivyo atauwawa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Delila Moshi, alipoulizwa na Nipashe juu ya madai hayo aliiomba kupewa muda zaidi kufuatilia ukweli wake ikiwa ni pamoja na kupata jina la mtoto, mzazi na tarehe waliyokwenda hospitali humo.

“Tamwa imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya polisi kuwaambia wazazi wa watoto waliofanyiwa ukatili wa ubakaji wakayamalize na mtuhumiwa nyumbani,” alisema Sanga.

"Baadhi ya polisi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwa mlalamikaji, wanatoa maneno ya vitisho."

Aidha, Sanga alisema wanaunga mkono tamko la Rais John Magufuli alilotoa siku ya sheria duninia na kutaka kila Hakimu kuhukumu kesi si chini ya 260 kwa mwaka na kwa haki.

Mwakilishi wa chama cha wanasheria wanawake (Tawla), Mary Richard, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho ya fomu namba 3 ili iwe na sehemu ya daktari aliyempima mwathirika kuandika jina.

Alisema kwenye fomu za sasa baadhi ya madaktari wamekuwa wakisaini lakini wakiitwa mahakamani kutoa ushahidi wanakataa.

Mwakilishi wa Shirika la Wajibika, Janeth Mawimba, alisema polisi wamekuwa kikwazo kikubwa katika kesi hizo.
Alisema, kwa mfano, kuna mtuhumiwa hajakamatwa licha ya mtoto wa miaka miwili kubakwa na baba yake mzazi hivi karibuni na jalada kufunguliwa kituo cha polisi Magomeni.

Habari Kubwa