Mahakama yakubali mshtakiwa kutoka gerezeni kuhojiwa polisi

24Sep 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama yakubali mshtakiwa kutoka gerezeni kuhojiwa polisi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali ombi la Jamhuri kwamba Mkurugenzi wa Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber Ltd, Khairoon Jandu, kutoka gerezani na kwenda kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa siku tano.

Amri hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Kasian Matembele, baada ya upande wa Jamhuri kuomba kwenda kumuhoji mshtakiwa huyo.

Kabla ya amri hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliiomba mahakama kutoa kibali cha mshtakiwa Khairoon, kurejeshwa polisi kwa mahojiano kwenye kesi nyingine dhidi yake zilizopo kwenye hatua ya upelelezi.

"Mheshimwa tunaomba mshtakiwa arejeshwe polisi akahojiwe kwenye kesi zingine mbalimbali na hii, na atahojiwa kwa siku tano na kukabidhiwa tena mahakamani hapa Jumatatu Septemba 28, 2020," alisema Wankyo.

Mbali na Khairoon ambaye ni mke wa marehemu Jandu, washtakiwa wengine ni, Zainabu Tharia, binti yake, Wakili Mohamed Majaliwa na Meneja wa benki ya Stanbic, Ibrahim Sangawe.

Katika kesi ya msingi inadaiwa, katika muda tofauti kati ya Januari na Juni, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja na kwa kudhamiria waliunda genge la uhalifu, kwa lengo la kughushi na kuiba fedha.

Katika shtaka la pili imedaiwa, Januari 16, 2017 jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa Khairoon Jandu, Majaliwa na Sangawe, walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka zilizoonesha kuwa ni halali za kikao cha Kampuni ya Jandu huku wakijua si kweli.

Alidai katika kosa la tatu washtakiwa hao kasoro Zainabu, walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka za kampuni zinazoonesha amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo akionyesha ni nyaraka halali huku akijua si kweli.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa Mei 25, 2019 katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa na nia ya udanganyifu walighushi saini ya Inderjit Jandu, wakionyesha kuwa amehamishia hisa za kampuni kwa Khairoon huku wakijua si kweli.

Shtaka jingine la kughushi linalomkabili Khairoon ni la nyaraka za wosia ulioandikwa na Inderjit akionyesha ni wosia halali huku akijua si kweli.

Ngukah aliendelea kudai kuwa katika shtaka la sita, saba na nane, Khairoon alitoa nyaraka za uongo kwa BRELA zilizoonyesha kuwa ni nyaraka halali za vikao vya kampuni ya Jandu kuwa amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo na pia amehamishiwa hisa za kampuni huku akijua kuwa si za kweli.

Katika shtaka la tisa washtakiwa wote wanadaiwa tarehe tofauti mwaka 2020 waliiba Sh. 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber.

Mshtakiwa Sangawe pia anadaiwa kati ya mwaka 2019 na 2020 akiwa ameajiriwa kama meneja wa benki ya Stanbic, alishindwa kutumia mbinu zote kuzuia wizi wa kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimehifadhiwa katika benki hiyo.

Katika kosa la mwisho la utakatishaji inadaiwa kati ya Januari 2019 na Juni 2020, jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia Sh. 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Construction huku wakijua kuwa fedha ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamili hivyo aliomba tarehe nyingine ha kutajwa.

Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 28, 2020.

Habari Kubwa