Mahakama yapokea risiti alizokopesha Malinzi TFF

06Dec 2018
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama yapokea risiti alizokopesha Malinzi TFF

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepokea vitabu sita vya risiti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  zilizosomeka rais wa zamani, Jamali Malinzi alilikopesha shirikisho hilo kwa nyakati tofauti Sh. milioni 25 na Dola za Marekani 41,000.

aliyekuwa rais wa tff jamal malinzi (kulia) akiwa na washtakiwa wenzake mahakama ya kisutu picha mtandao

Kadhalika, mahakama hiyo imeambiwa na shahidi wa tisa Mhasibu wa zamani wa TFF, Seleki Mesack (68), kwamba fedha hizo zilikopeshwa kwa shirikisho, timu ya taifa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys na kugharamia safari za wajumbe wa shirikisho hilo kwenda nchini Afrika Kusini.

Mesack alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, anayesikiliza kesi ya kutakatisha Dola za Marekani 173,335 inayomkabili Malinzi na wenzake wanne.

Shahidi alidai kuwa aliajiriwa kama Mhasibu TFF 1985 mpaka Januari, mwaka huu, alipostaafu, kwa sasa ni mkulima Kibaha mkoani Pwani.

Alidai kuwa wakati wa utumishi wake, TFF majukumu yake yalikuwa kuingiza kumbukumbu mbalimbali ikiwamo risiti za malipo, kitabu cha risiti za malipo cha kupokelea fedha katika kompyuta.

"Mheshimiwa anayetoa fedha anakwenda kwa mhasibu akipokea malipo anapewa risiti, fedha inayolipwa inatakiwa isomeke katika kitabu cha risiti cha TFF ambacho kina alama maalum ikiwamo nembo inayotambulisha shirikisho,” alidai.

Shahidi huyo aliyekuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leornad Swai, aliomba mahakama hiyo kupokea vitabu hivyo sita kama kielelezo katika kesi hiyo.

Upande wa utetezi ulidai hauna pingamizi na vitabu hivyo kupokelewa kama kielelezo.

Hakimu alisema kwa kuwa pande zote mbili zimeridhia vitabu hivyo kupokelewa kama kielelezo, mahakama yake inapokea kama kielelezo namba sita cha kesi hiyo.

Shahidi alisoma risiti moja baada ya nyingine kwamba Oktoba 6, 2016, Malinzi alitoa mkopo kwa TFF wa Sh. milioni 10, Mei 9, 2016 aliikopesha Dola za Marekani 8,000.

Aliendelea kudai kuwa Mei 9, 2016 Malinzi aliikopesha TFF Dola za Marekani 7,000, Mei 27, 2016 aliikopesha Sh. milioni tano kwa ajili ya kuwahudumia wachezaji wa timu ya Serengeti Boys, Juni 16, 2016, aliikopesha TFF Dola za Marekani, 10,000.

Mesack aliendelea kuelezea Agosti 2, 2016 aliikopesha TFF Dola za Marekani, 1,000 za kuwawezesha Ayubu Nyenzi na P. Rutayuga kwa ajili ya kusafiri kwenda Afrika Kusini, Septemba 21, 2016 aliikopesha Sh. milioni saba.

Septemba 21, 2016 Malinzi aliikopesha TFF  Sh. milioni tatu kama posho za timu ya Serengeti Boys, Septemba 22, 2016 aliikopesha Dola za Marekani 15,000 kwa ajili ya matumizi ya timu hiyo nchini Rwanda/Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akihojiwa na utetezi, shahidi alidai kuwa mhasibu aliyesaini risiti hizo ndiye anayefahamu malipo hayo yalifikia kiasi gani na Malinzi alilipwa lini.

Alidai kuwa kiasi alichokopeshwa Malinzi hawezi kufahamu wala kukadiria mpaka apitie nyaraka za malipo hayo.
Kesi hiyo itaendelea Desemba 18, mwaka huu kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri.

Mbali na Malinzi (57), washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27).

Meneja wa  Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya, kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh. 43,100,000.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha, mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Flora wapo nje kwa dhamana.

 

Habari Kubwa