Mahakama yatoa neno kesi ya Wambura

01Mar 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama yatoa neno kesi ya Wambura

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wana kamilisha upelelezi kwa wakati dhidi ya kesi inayomkabili,  Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.

Jana, kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Wankyo Simon,  ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliiomba mahakama kuuagiza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati.

"Jamhuri wana wajibu wa kuhakikisha wanakamilisha upelelezi kwa wakati kwa sababu hadi mshtakiwa anafikishwa mahakamani hapa, mlitakiwa muwe mmekamilisha upelelezi huo," alidai Wakili Magafu.

Kutokana na hoja hiyo, Hakimu Mhina, alisema upande wa Jamhuri ujitahidi kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo na  itatajwa tena Machi 13, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu. 

Katika kesi ya msingi, kigogo huyo anakabiliwa na mashtaka 17, likiwamo la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo, mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Ilidaiwa siku na tarehe ya tukio la kwanza, Wambura kwa nia ya kutapeli  alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha  imeandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck System Ltd, akidai kurejeshewa malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 30,000, pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa  alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF, huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiwa kutenda kosa hilo Juni 17, 2015, katika ofisi za TFF kwa kujipatia Sh. milioni 10 kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ya Jeck jambo ambalo si kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadaiwa kuwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya TFF, alijipatia Sh. milioni 25 kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kughushi.

Habari Kubwa