Mahakama yatupilia mbali kesi dhidi ya Spika, AG, Mbunge

04Jun 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama yatupilia mbali kesi dhidi ya Spika, AG, Mbunge

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetupiliwa mbali kesi ya Kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Jobu Ndugai na wenzake kwamba imefunguliwa kinyume na utaratibu.

Wakili wa Shirika la Civic and Legal Aid Organization (CILAO), Paul Kaunda (kulia), akizungumza na Wakili wa Serikali, baada ya kesi ya kikatiba aliyoifungua katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya kuomba tafsiri ya kisheria kufuatia kitendo cha Spika Job Ndugai, kumrejesha Bungeni, Mbunge Cecil Mwambe, kutupiliwa mbali na mahakama hiyo, jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Kesi hiyo ilifunguliwa na Wakili Paul Kaunda dhidi ya Spika Ndugai, Mbunge wa Jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye kwa sasa amehamia CCM, Cecil Mwambe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti, Issa Maige, akisaidiana na Stephen Magoiga na Seif Kulita, ilitoa uamuzi huo baada ya kusikiliza pingamizi la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu.

Jaji Maige alisema jopo wamekubaliana na hoja za Mwanasheria Mkuu kwamba mlalamikaji amekosea kufungua kesi hiyo kwa kutumia ibara ya 26, bali alipaswa ajiegemeza katika ibara ya 83 ya Katiba ikiwa sambamba na kifungu cha 37 cha Sheria ya Uchaguzi.

Ibara hiyo inaelekeza utaratibu wa kuwasilisha malalamiko kama yaliyowasilishwa na mlalamikaji.

Alisema maneno aliyotamka Spika yako katika msingi na utaratibu wa kawaida katika utendaji wake.

Katika kesi ya msingi, Wakili Kaunda anadai Mwambe alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM kauli ambayo iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, aliyempokea rasmi Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM, na Mwambe naye alimkabidhi Katibu Mkuu huyo kadi yake ya Chadema.

Wakili Kaunda anadai kitendo cha Spika kumtambua Mwambe kama Mbunge halali wakati ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama Mbunge wa Ndanda (2015-2020), ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa kumrudisha bungeni mbunge ambaye kwa hiyari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.

Katika hoja za awali za serikali, pamoja na mambo mengine ilidai kuwa shauri hilo halistahili kwa kuwa linakinzana na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, pamoja na Ibara ya 26(2) ya Katiba ya nchi.

Pamoja na pingamizi hilo pia serikali katika majibu yake inadai kuwa Mwambe bado ni Mbunge halali wa Ndanda kwa mujibu wa Katiba na sheria nyingine za nchi na anastahili stahiki zote kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazotumika kusimamia masuala ya Bunge.

Serikali inadai kuwa Spika hajavunja sharti lolote la Katiba ya nchi kama inavyodaiwa, na hivyo inamtaka mdai kuthibitisha madai yake.

Habari Kubwa