Mahakama yawaweka kando wazee washauri

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Bunda
Nipashe
Mahakama yawaweka kando wazee washauri

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, amesema Mahakama inakusudia kupunguza kuwatumia wazee washauri wa Mahakama katika kuamua mashauri mahakamani.

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, picha mtandao

Badala yake amesema itabaki ikiwatumia katika mashauri ambayo yataonekana yana ulazima wa kuwatumia wazee hao.

Akizungumza wilayani Bunda mkoani Mara katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama, Jaji Kiongozi alisema wazee hao watatumiwa na Mahakama kwenye mashauri ambayo yatakuwa na ulazima wa kuwatumia, lakini yale ambayo siyo lazima, wazee hao wataacha kutumiwa.

Jaji Kiongozi alisema baadhi ya wazee washauri wa Mahakama hujishirikisha na vitendo vya rushwa na wakati mwingine huwatisha Mahakimu wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao.

Alisema matumizi ya wazee washauri wa Mahakama wakati mwingine husababisha mashauri kuchelewa kumalizika kutokana na kuchelewa kwao kufika mahakamani na kusababisha mashauri kutokusikilizwa kwa wakati.

Akizungumza kuhusu rushwa, Jaji Feleshi alisema Mahakama kama taasisi haijishirikishi na vitendo vya rushwa bali vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu ndani ya Mahakama.

“Tuachane na maneno mepesi mepesi kuhusu rushwa kwa kuwa taarifa zipo, pelekeni Takukuru, hakuna anayemlinda mtu,” alisema Jaji Kiongozi.

Alisema Mahakama itashirikiana na Serikali katika kupambanana na rushwa, hivvo aliwataka wananchi wenye taarifa juu ya vitendo hivyo kuwasilisha Takukuru.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Jaji Kiongozi aliwataka kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kubeba matarajio ya taasisi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aliwataka Mahakimu kumalizika mashauri kwa wakati pamoja na kutoa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri katika muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa utaratibu, nakala za hukumu ni siku 21 tangu kumalizika kwa shauri na mienendo ya shauri hutolewa ndani ya siku 30.

Aidha, aliwataka watumishi hao kujenga tabia ya kutafuta na kufahamu taarifa mbalimbali za Mahakama kupitia Tovuti pamoja na Blog ya Mahakama ya Tanzania.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, aliwashauri watumishi hao kujenga mazingira yatakayowafanya wananchi kuendelea kuiamini Mahakama ya Tanzania kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Jaji Kiongozi ameanza ziara ya kikazi ya siku tano Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma ambapo atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Musoma.

Habari Kubwa