Mahakamani kwa rushwa kujifanya afisa TAKUKURU

03Jul 2020
Dotto Lameck
Pwani
Nipashe
Mahakamani kwa rushwa kujifanya afisa TAKUKURU

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani imempeleka Mahakamani Joseph Mwenda, kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya zaidi ya Shilingi Milioni 15 ambapo ni kinyume na sheria.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Suzana Raymond.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Suzana Raymond, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo.

Suzana amesema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kupata fedha hizo kutoka kwa mwananchi kwa madai ya kuwa fedha hizo ziliombwa na Afisa wa TAKUKURU ili aweze kumsaidia mtuhumiwa huyo katika kesi yake.

Suzana amesema taasisi hiyo ilipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuhusiana na mtuhumiwa huyo ndipo wakapojipanga na kufanikiwa kumkamata.

Aidha, Suzana amesema uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyo unaendelea ili kubaini malengo yake na watu ambao tayari ameshawatapeli.

Pia, Suzana ametumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kutoa taarifa mara wanapopigiwa simu na mtu yeyote atakayejitambulisha kuwa ni Afisa wa TAKUKURU na kudai fedha au kutaka kuonana eneo ambalo sio ofisi ya Taasisi hiyo.

Habari Kubwa