Mahojiano maalum: Bosi mkuu aanika vigingi viwili Takukuru

14Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Mahojiano maalum: Bosi mkuu aanika vigingi viwili Takukuru

MKURUGENZI Mkuu mpya wa Takukuru, Diwani Athumani, ametaja changamoto mbili zinazoikabili Taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Diwani Athumani (kushoto) akiwa na Rais John Magufuli.

Athumani ambaye ni Kamishna wa Polisi, aliteuliwa na Rais John Magufuli, kuiongoza Takukuru Septemba 6, mwaka jana, akichukua nafasi ya Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola, aliyeteuliwa kuwa balozi.

Katika mahojiano maalum na Nipashe wiki iliyopita, Kamishna Athumani, mbali na mambo mengine, alisema changamoto kubwa mbili zilizopo katika taasisi hiyo nyeti ni uhaba wa rasilimali watu na fedha pamoja na uoga wa mashahidi wanaopelekwa mahakamani kutoa ushahidi wa kesi wanazozifungua.

"Changamoto ninayoiona ni kwamba tunao uwezo wa kufanya kazi nyingi katika kuzuia na kupambana na rushwa, isipokuwa bado rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu hazitoshelezi," alisema kigogo huyo wa Takukuru.

Mkurugenzi Mkuu huyo aliongeza: "Kwa upande mwingine, bado tunayo changamoto ya mashahidi wetu katika kesi tunazozifungua mahakamani, kuwa waoga.

"Mashahidi wetu wanakosa ujasiri wa kuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi wa jambo ambalo alilishuhudia yeye mwenyewe dhidi ya washtakiwa wa makosa ya rushwa.

"Hata hivyo, kwa changamoto hizi zote mbili, si kwamba zinatufanya tubweteke, la hasha! Tunaendelea kutekeleza majukumu yetu ipasavyo kwa rasilimali hizi ndogo tulizonazo.

"Vilevile, tunaendelea kuelimisha jamii umuhimu wa kushiriki katika kutoa ushahidi mahakamani, ili kwa pamoja tuweze kudhibiti kero ya rushwa katika taifa letu, ambayo faida yake ni maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania."

Katika mahojiano hayo, Kamishna Athumani pia alizungumzia tuhuma za kuomba rushwa ya ngono inayowakabili baadhi ya wahadhiri na maprofesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia, alizungumzia maendeleo ya uchunguzi dhidi ya vigogo walioingia mkataba tata wa mradi wa ujenzi wa Mlimani City ambao pia uko chini ya UDSM.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na Katibu Tawala huyo wa zamani wa Mkoa wa Kagera:-

Swali: Kwa mujibu wa takwimu za Takukuru, ni aina ipi ya rushwa inayoongoza kwa kulalamikiwa?

Jibu: Kwa mujibu wa takwimu za Takukuru, kwa mwaka 2017/2018, makosa yanayoongoza kwa kulalamikiwa ni yale yanayohusu hongo, ambayo ni asilimia 28 ya malalamiko, pamoja na yanayohusu ubadhirifu unaofanyika kwenye fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Makosa haya ni kinyume cha Kifungu cha 15 na Kifungu cha 28 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Swali: Macho na masikio yameelekezwa katika kitakachobainika kwenye uchunguzi wa Takukuru kuhusu tuhuma za rushwa ya ngono UDSM. Mmefikia wapi katika uchunguzi huu? Kuna wahadhiri mliowahoji? Kama wapo, ni wangapi?

Jibu: Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizi unaendelea na utakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mtuhumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Swali: Kwa muda mrefu Takukuru imekuwa inachunguza mradi tata wa Mlimani City. Hatua zipi zimechukuliwa dhidi ya walioingia mkataba huo?

Jibu: Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizi unaendelea na utakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa kwa mujibu wa sheria inayoongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Swali: Takukuru iliwahi kueleza kuwa iwapo ikibainika kwamba anayechunguzwa kwa ufisadi amefariki dunia, mali zake zitachukuliwa. Je, wapo ambao mnawachunguza wakiwa kwenye kundi hili? Wangapi kwa mazingira ya kesi ya aina hiyo, huwa mnaifikisha mahakamani?

Jibu: Ni kweli kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inayo mamlaka kisheria baada ya uchunguzi, kufanya maombi ya kutaifisha mali za mtuhumiwa aliyefariki dunia kama ilivyoelekezwa katika Kifungu cha 4 na cha 5 cha Proceeds of Crime Act Sura ya 256 Pitio la Mwaka 2002.

Hata hivyo, bado hatujawahi kukutana na hali kama hii katika uchunguzi wetu.

Swali: Tutarajie nini mwaka 2019 kutoka Takukuru?

Jibu: Mwaka 2019, wananchi watarajie kuona Takukuru inayoongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini kwa kutumia mbinu mpya na za kisayansi.

Tutafanya kazi kwa bidii zaidi, tutafanya kazi kwa weledi zaidi, tutafanya kazi kwa kasi zaidi, tutashirikiana na wadau wengi zaidi na tutatafuta fursa zaidi za kutangaza mafanikio yetu.

Swali: Kesi ngapi kubwa zinazotarajiwa kufikishwa mahakamani mwaka 2019 kutokana na uchunguzi wake kukamilika?

Jibu: Wananchi watarajie kuona kesi nyingi zitakazofunguliwa mahakamani. Kutakuwa na kesi kubwa na kesi ndogo kwa kuwa Takukuru tunashughulikia makosa yote kwa kutambua kwamba makosa hayo yote yana madhara makubwa kwa jamii yetu.

Swali: Kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi nyeti kama hii ni jukumu zito. Hebu tuambie ratiba yako ya siku moja, kuanzia unapoamka mpaka unarejea tena kitandani kupumzika.

Jibu: Kwa kuwa mimi ni kiongozi wa chombo cha kiuchunguzi, nafikiri si sahihi kuzungumzia ratiba yangu hadharani.

Swali: Ipo kashfa ya kufanya ununuzi hewa sare za Jeshi la Polisi, na wahusika kulipwa Sh. bilioni 40 miaka minne iliyopita. Uchunguzi wake umefikia wapi?

Jibu: Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizi unaendelea na utakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa kwa mujibu wa sheria inayoongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Habari Kubwa