Mahojiano maalum: DCI 'alia' na uhaba wa polisi

16Jan 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mahojiano maalum: DCI 'alia' na uhaba wa polisi
  • Askari mmoja analinda raia 1,300

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robart Boaz, amesema Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa askari polisi licha ya jitihada zinazofanywa na serikali kutatua changamoto hiyo.

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robart Boaz, picha mtandao

DCI Boaz aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Nipashe ofisi kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Nipashe, pamoja na mambo mengine, ilitaka kujua mikakati ya Jeshi la Polisi kukabiliana na wahalifu wanaovunja milango usiku na wanaopora kwa kukwapua wakiwa kwenye pikipiki.

Katika majibu yake, DCI Boaz alisema kuwa licha ya kuwapo askari polisi ambao hufanya doria katika mitaa mbalimbali, kumaliza uhalifu wa aina hiyo kunahitaji ushirikiano wa wananchi wenyewe.

“Unajua wakati mwingine makosa kama hayo ya mwananchi kavunjiwa mlango, kuibiwa au kaporwa kitu mtaani, inatakiwa wananchi wenyewe watoe taarifa kwa sababu kuna baadhi ya maeneo ambayo polisi wanatakiwa kufanya doria mara kwa mara na kuna maeneo ambayo huwa wanawekwa askari kanzu kwa ajili hiyo kutokana na matukio ya sehemu husika," alisema.

DCI Boaz alibainisha kuwa viwango vya kimataifa vinataka askari mmoja alinde raia 500, lakini Tanzania kwa sasa askari mmoja analinda raia 1,300.

"Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba askari mmoja amezidiwa mara tatu," DCI Boaz alisema, kwa hali ya kawaida, huwezi kuona askari kila mahali kwa wakati unaotakiwa.

"Kwa hiyo, lazima wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi kuzitambua kero zao na kutafuta majawabu yake."

Katika mahojiano hayo, DCI Boaz pia alitaja malengo maalum ya Idara ya Upelelezi kwa mwaka huu, akisisitiza kuwa malengo hayo yatasaidia kazi zao kuwa bora zaidi.

Alisema yako mambo ambayo wameyapanga kuyaboresha, na wanaamini huenda ndiyo yamekuwa kikwazo na sababu ya kuchelewesha kazi za upelelezi.

Alisema malengo hayo ni pamoja na kuhakikisha wanaongeza juhudi ya kuhudumia wateja na kumaliza kero zote ambazo kitengo hicho kilikuwa kikitupiwa lawama kwa kuchelewa upelelezi.

Alisema wamejipanga kuhakikisha upelelezi unafanyika kwa haraka na kwa ufanisi.

DCI alisema jambo la pili ni kupambana na changamoto ya kukosekana kwa uadilifu kwa baadhi ya watendaji wake wanapotekeleza majukumu ya nafasi zao.

"Na hapa tumejipanga kweli kweli, tunataka kupambana na wasio na uadilifu, mtu anapokuwa si mwadilifu, maana yake ndiyo unaanza kuziona hizo za njoo leo, njoo kesho, njoo keshokutwa, kumbe mtu anatengeneza mazingira ambayo siyo mazuri, katika hili hatuna mzaha," alisema.

Mkurugenzi huyo aliongeza: “Hatuwezi kuvumilia watu wanaoendekeza rushwa kwenye shughuli za upelelezi, yaani unakuta wakati mwingine mtu anatakiwa aandikiwe maelezo, unakuta anakalishwa muda mrefu bila kupata huduma hiyo kwa sababu tu mtu anatengeneza mazingira ya rushwa.

"Vitu kama hivyo kimsingi hatuvifumbii macho na kuvichelewesha. Na tunataka kuhakikisha tunavikomesha visipate nafasi kabisa."
DCI Boaz alisema mkakati wao wa tatu ni kuwajengea uwezo wapelelezi ili kuhakikisha wanapunguza kama si kumaliza malalamiko ambayo yamekuwa yakielekezwa dhidi yao.

Alisema mkakati huo unakwenda sambamba na kujenga weledi kwa watendaji wake.

“Kwa sababu ukikosa weledi, unakaribisha mtu mwingine akulalamikie," DCI Boaz alisema, "ukikosa weledi upelelezi lazima utachelewa tu.

"Kwa sababu unashindwa kujua kwamba katika upelelezi wako unatakiwa kuthibitisha kitu gani. Sasa kama hujui namna gani unatakiwa ukusanye ushahidi, maana yake hiyo kesi lazima ufeli.

"Kwa hiyo, tutaweka msisitizo kwa kufundisha askari wetu wawe mahiri katika shughuli mbalimbali zikiwamo hizi za upelelezi."

Kigogo huyo pia alisema wamejipanga kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine ambazo wanafanya nazo kazi katika kukamilisha masuala ya upelelezi.

Alisema suala la upelelezi wakati mwingine huhitaji kushirikiana na taasisi nyingine za serikali na kwamba ili kufanikisha wanafanikisha, kuna umuhimu kwa kujipanga zaidi.

"Upelelezi huu wakati mwingine unahitaji kushirikiana na watu wengine. Tunajaribu kuona namna bora ya kupunguza urasimu katika taasisi moja na nyingine. Kwa mfano, unapeleka kielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, unachukua muda gani kukipata? Kwa hiyo, idara hizi tunatakiwa tuwe na ushirikiano," alisema.

DCI Boaz aliongeza: "Na kama kuna changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wa idara hizi, tuzitatue haraka ili kufanikisha masuala ya upelelezi. Isipokuwa vile vitu ambavyo haviko ndani ya uwezo wa idara hizi.”

Akieleza kuwa changamoto kubwa zinazoikabili idara ya upelelezi, mkurugenzi huyo alisema kubadilika kwa teknolojia kumeleta tatizo kubwa katika masuala ya upelelezi.

“Na naweza kusema hii ndiyo changamoto kubwa sana. Kwa mfano, zamani watu walikuwa wakitukanana wakiwa wanaonana ana kwa ana, lakini sasa hivi watu wanaweza kutukanana kupitia Instagram," alisema na kueleza zaidi:

"Sasa kupata ushahidi kutoka Instagram ili ukubalike mahakamani kwamba huyu mtu katukanwa ni changamoto kubwa sana, kwa sababu sheria inasema kwamba lazima uwapo na uwezekano wa kutokea uvunjifu wa amani.

“Lakini labda mtu anakutukana kupitia Instagram ambayo haiko Tanzania, kukusanya huo ushahidi na ukubalike kisheria ni changamoto kwa sababu ni rahisi sana kuupoteza.

"Kwa hiyo, mtu anaweza kufanya kosa leo, kesho ukianza kumfuatilia, ushahidi umeshafutika, hata kama tayari watu wameshaona kwamba huyu kafanya kosa hilo. Kwa hiyo, unaweza kuona mabadiliko ya teknolojia inavyokuwa changamoto kubwa sana.”

DCI Boaz alisema changamoto ya pili inayoambatana na mabadiliko ya teknolojia ni makosa yanayovuka mipaka. Alisema kuwapo kwa kesi ambazo mhalifu anafanya uhalifu husika Tanzania wakati huo akiwa nje ya Tanzania ni changamoto kubwa.

"Leo hii ziko kesi ambazo mtu anaweza kuwa nchi nyingine, lakini akafanya uhalifu Tanzania, hasa wa wizi, akaiba pesa na kuzihamishia nje ya nchi. Namna ya kukusanya ushahidi huo ni kazi ngumu sana," alisema.

DCI Boaz alifafanua: "Kwanza, unahitaji uelewe zaidi jinsi jambo hilo linavyofanyika, lakini pia unahitaji 'resources' za kuweza kufuatilia huko.

"Kinachotusaidia ni kupitia Jeshi la Polisi la kidunia (Interpol) kwamba tunaweza kushirikiana nao kumtafuta mhalifu tukampata na akachukuliwa hatua, japokuwa inategemea na sheria za kila nchi.

"Ili mtu ashtakiwe, ambaye yuko nje ya nchi, inategemea yuko nchi gani na je, ile nchi na sisi tuna uhusiano wa kusaidiana? Lakini je, nchi ile inaliona lile ni kosa?

"Tunapohitaji kwamba huyu mtu amefanya hili kosa huku kwetu, lazima kwenye sheria zao nao waone ni kosa na wakiona kama ni kosa na wakamshtaki, basi mahakama ya nchi husika ndiyo inaweza kumrudisha mtuhumiwa aje ashtakiwe huku.

"Lakini wakiona kama siyo kosa au halielekei kwenye jinai kwa mujibu wa sheria zao, mahakama inaweza kukataa asiletwe, na ndiyo maana nasema hizo ndiyo changamoto kubwa. Mtu mwingine anaweza kufanya kosa kwa makusudi akijua kwamba ni vigumu kumkamata kutokana na changamoto za kisheria."

MIAKA MITATU YA JPM

Katika mahojiano hayo, DCI Boaz alizungumzia miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano, akimpongeza Rais John Magufuli kwa kurejesha uwajibikaji kwa watumishi wa umma likiwamo Jeshi la Polisi.

“Ninaona mabadiliko makubwa, kila mtu anajitahidi kufanya kazi ile ambayo amepangiwa. Na watu wakifanya kazi namna hii, nafasi ya kufanya uhalifu pia inapungua, watu watatumia muda mwingi kufanya kazi, kwa hiyo hawatakuwa na muda wa kufanya uhalifu," alisema Boaz.

“Lakini pia katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano, mazingira ya kufanyika kazi kwa Jeshi la Polisi yameboreshwa zaidi, tuna vitendea kazi vya kutosha na hata makazi yameboreshwa," DCI Boaz alisifu.

MAITI KWENYE VIROBA

Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa maiti zinaopolewa baharini zikiwa zimefungwa kwenye viroba, mkurugenzi huyo alisema upelelezi wa kesi zozote za mtu ambaye amepotea au ameokotwa akiwa amefariki dunia na hajulikani, unategemea kwa kiasi kikubwa taarifa za ziada zinazopatikana baada ya kuokotwa.

“Kwa mfano, labda kama atatambuliwa kwa sura au vinasaba vyake au alama za vidole au mazingira aliyokutwa na kama kuna kitu kinachoweza kuhusiana kuweza kujua kwamba huyu anaweza kuwa ni fulani," alisema DCI Boaz na kufafanua zaidi:

“Lakini, maiti nyingi zilikuwa zinaokotwa kwanza zikiwa zimeharibika sana, hazitambuliki kwa sura na hata kama zikitambulika tulikuwa tunatangaza.

"Kama wataalamu tunachofanya huwa tunatunza vinasaba kwa ajili ya mtu yeyote anayeibuka na kusema amepotelewa na ndugu yake, kama ni ndugu yake, basi tunachukua vinasaba vyake, tunaoainisha na vinasaba vya mwili uliookotwa ili kujua kama ndiye au siye. Mpaka sasa hatujawahi kuona mtu yeyote anajitokeza."

MWANDISHI AZORY

Nipashe pia ilimuuliza DCI Boaz kuhusu maendeleo ya upelelezi wa kutoweka kitatanishi kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda.

Katika majibu yake, mkurugenzi huyo alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo, lakini akaeleza kuwa mpaka sasa, hawajapata ushahidi unaoweza kufanikisha kupatikana kwake.

“'Of course', watu mbalimbali wamejitokeza kutoa maelezo, lakini maelezo hayatufikishi mwisho kutuonyesha kwamba mara ya mwisho alikuwa wapi," alisema DCI Boaz.

Kigogo huyo wa Jeshi la Polisi alisema ni vema mwaka huu ukawa ni wa utii wa sheria zaidi na watu wakaachana na tabia za uhalifu.

“Ni vizuri sana wakati serikali inafanya juhudi za kuleta maendeleo, watu wakajenga utamaduni wa kutii sheria, kuacha uhalifu na kama umepewa dhamana ya kushika pesa, ni vema ukaziacha zikafanya maendeleo, usizitamani na sisi kama Jeshi la Polisi, haya mambo ndiyo tumepanga kuongeza juhudi kwa kazi zaidi kupambana na wahalifu," alisema DCI Boaz.

Habari Kubwa