MAHOJIANO MAALUM Mbunge afunguka hatima ya katiba

14Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
MAHOJIANO MAALUM Mbunge afunguka hatima ya katiba

KAULI ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba mchakato wa katiba mpya si kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano kwa sasa, imeuibua Ukawa ambao umeipinga vikali huku ukitishia kuingia barabarani kuandamana.

Mbunge wa Temeke (CUF) Abdallah Mtolea.

Mchakato huo umesimama kwa takribani miaka mitatu sasa huku serikali ikikiri bungeni kwamba haina mpango wa kuuendeleza kwa sasa hadi pale itakapoimarisha makusanyo yake ya mapato.

Kauli hiyo iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imepingwa vikali na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, huku aliyeliibua suala hilo bungeni Alhamisi iliyopita, Abdallah Mtolea naye akisema hajafurahishwa na jibu alilopewa na serikali baada ya kuhoji sababu za kusimama kwa mchakato huo.

Mtolea, Mbunge wa Temeke (CUF), alimuuliza Waziri Mkuu hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano kukamilika mchakato huo ulioligharimu taifa mabilioni ya shilingi.

Katika kujenga hoja yake siku hiyo kabla ya kuuliza swali, Mtolea (41), alisema serikali ya awamu ya nne ilitumia mabilioni ya shilingi kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni kwa ajili ya kuandaa katiba mpya, lakini haoni hatua zozote zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano kumalizia mchakato huo.

Mbunge huyo mwenye shahada ya sheria, alisema uamuzi huo wa kuandaa katiba mpya uliridhiwa na serikali baada ya kubainika kwamba taifa linahitaji katiba mpya ili kutibu changamoto nyingi zinazolikabili katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali, haki za binadamu na tunu za taifa.

Katika jibu lake siku hiyo, Majaliwa alibainisha kuwa mchakato huo umesimama kwa sasa kutokana na ufinyu wa bajeti na pia suala hilo kutokuwa sehemu ya vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano.

Kauli hiyo ya serikali imepingwa vikali na Ukawa kupitia kwa Mbowe ambaye mwishoni mwa wiki alisema mchakato huo unapaswa kumaliziwa kwa kuwa hata ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ina hoja ya kumalizia mchakato wa katiba mpya.

"Sasa ambacho naweza kusema, ni jambo la kusikitisha sana kwamba kauli kama hii inatoka kwa Waziri Mkuu, tena ndani ya bunge, jambo ambalo Watanzania wote waliridhia kulifanya na lililigharimu taifa hela nyingi," alisema.

Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, Nipashe ilifanya mahojiano maalum na Mtolea kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge mjini hapa Jumapili na mbunge huyo akasema hakuridhishwa na sababu zilizotolewa na serikali kukwamisha mchakato huo.

Alisema kuwa kutokana na kauli hiyo ya serikali, yeye na upinzani kwa ujumla watakwenda kwa umma kuuambia serikali haina nia ya kuleta katiba mpya na kuunganisha nguvu na makundi mbalimbali kuibana serikali ili imalizie mchakato huo.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mbunge huyo...

Swali: Nini kinafuata baada ya jibu la Waziri Mkuu kuhusu mchakato wa katiba? Kama mmoja wa machampioni wa katiba mpya, hatua gani inafuata kwako binafsi na kama mwanaharakati?

Mtolea: Sasa ndiyo wakati wa kwenda zaidi kwa umma kuwaambia kuwa serikali haina nia ya kuleta katiba mpya. Ni wakati wa makundi mbalimbali kuunganisha nguvu zao na kuongeza mbinyo kwa serikali.

Wapinzani tutatumia fursa ya chaguzi hizi ndogo kuuzindua umma juu ya CCM kukalia na kunyonga haki yao ya kuwa na katiba mpya.

Tutawaambia wananchi katiba ni lazima hata pakiwa hapana maji, chakula na barabara maana kwa kuwapo kwake, mwafaka wa hayo yote utakuja maana patakuwa na serikali inayojali matakwa ya wananchi na kuwajibika kwa wakati.

Swali: Kimsingi unaweza kuwa na katiba nzuri, lakini ikawa kikwazo cha maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kama hali ilivyojionyesha Kenya. Nini maoni yako kuhusu hili?

Mtolea: Kwanza hiyo ni si tafsiri sahihi, kwamba katiba inaweza kuwa kikwazo cha maaendeleo. Unajua katiba kwa maana hasa ya katiba ni yale matakwa ya wananchi na maendeleo yoyote kama hayawagusi wananchi hayawezi kuwa maendeleo.

Ndiyo maana watu wanapiga kelele ujenzi wa uwanja wa ndege Chato kwamba kuna vitu vinafanyika, lakini havimgusi mwananchi moja kwa moja, si hitaji la wananchi kwa wakati huo.

Kwa hiyo, katiba haijawahi na wala haitakuja kutokea kuwa kikwazo cha maendeleo isipokuwa yenyewe ndiyo inakuwa chachu ya maendeleo.

Hata Kenya kusema kwamba katiba imekuwa kikwazo si sahihi. Katiba inaweza kuwa kikwazo kwa mambo ya kisiasa kwa namna moja au nyingine kwa sababu tu ya ubinafsi wa kisiasa kwa maana mtu anaitumia katiba vibaya, lakini kwa maana ya maendeleo, katiba ndiyo chachu hasa.

Hata Waziri Mkuu anaposema kwamba sasa hivi wanajikita katika kupeleka huduma za jamii, hizo huduma za jamii zenyewe ambazo leo anahangaika kuzipeleka ni kwa sababu ya hatukuwa na katiba nzuri.

Tungekuwa na katiba nzuri hizo huduma zote za kijamii zingekuwa tayari zimeshawafikia watu. Lakini hata ule mgawanyo wenyewe wa hizo huduma ungezingatia usawa.

Swali: Hivi kweli kipaumbele cha Watanzania ni katiba mpya au uboreshaji wa huduma za jamii kama za afya, maji, ajira na uhakika wa usalama wa maisha yao?

Mtolea: Haya mawili huwezi kuyatenganisha, huwezi kuyatenganisha! Yaani unapodai huduma za kijamii, unapodai maendeleo, unatumia nguvu nyingi kuyadai wewe kama wewe au watu wa maeneo Fulani, lakini kama yangekuwa yametajwa kwenye katiba, yaani kila kitu ambacho serikali inatakiwa kukifanya kwa mwananchi ni haki ya wananchi.

Na haki zimetajwa kwenye katiba.
Kwa hiyo mtu anaposema anadai katiba, ndiyo kwa maneno mengine anadai huduma zake za maji, hospitali kwa maana ya afya, yaani hivyo vyote hivyo ndiyo vinaitwa katiba.

Swali: Mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umekuathiri vipi wewe binafsi?
Mtolea: 'Of course' (Ni kweli) migogoro inaathiri sana kwenye shughuli za kisiasa. Wakati ninatekeleza majukumu yangu ninahitaji sana 'back up' (nguvu) ya chama, mtandao wa chama uwe nao unafanya kazi kwa kuwaambia wananchi vitu vizuri ambavyo tunavifanya kwa sababu si kila wakati jambo likifanywa mna muda wa kwenda kwa wananchi kuanza kuwaambia. Vitu vingi sana tunavifanya kila siku.

Sasa wale ambao walikuwa wanakwenda kukuombea kura, ndiyo walewale wanaotakiwa kwenda kwa wananchi kuwaambia kwamba 'mnaona hiki hapa, mnaona lile pale, mbunge kafanya, kura yetu ndiyo imetuletea'.

Sasa zile nafasi zote tunazikosa. Tunachokifanya ni mikutano tu ya chama, kuimarisha chama na nini. Mipango mingi imekwama. Kama mbunge unakuwa na jukumu pia la kukiimarisha chama, unatengeneza 'base' (nguvu) yako ya kuendelea kubaki madarakani.

Swali: Je, una mpango wa kujiunga na timu Lipumba kufuata nyayo za wabunge watatu wa jimbo waliojiunga naye mpaka sasa?
Mtolea: Ha ha haah! Mimi nawezaje kuwa timu Lipumba? Mimi simtambui Lipumba toka mwanzo na sitakuja kumtambua Lipumba. Alishajiuzulu, siyo mwenyekiti, tunamwacha ahangaike na hao ambao wanampa sapoti kutuvurugia chama chetu.

Lakini, najua hiki ni kipindi cha mpito, kesi ziko mahakamani. Naamini mahakama itatuonyesha haki iko wapi, chama chetu kitabaki vizuri tu.

Swali: Ukipata nafasi ya kukutana na Prof. Ibrahim Lipumba leo, utamwambia nini kwa maslahi mapana ya CUF?
Mtolea: Sitaki kukutana na Lipumba. Ameshakivuruga chama vya kutosha. Sina kitu ambacho naweza kumshauri tena. Kwanza simtambui kama kiongozi wa chama chetu. Sasa nikikutana naye nianze kumshauri mambo ya CUF, yeye hayamhusu kabisa.

Swali: Kwa hali ilivyo sasa ndani ya CUF, unafikiri utarejea bungeni mwaka 2020 kupitia chama hicho?

Mtolea: Sikuchaguliwa kuingia bungeni na wanaCUF pekee. Nimechaguliwa na wananchi wote. Kumbuka mimi ni mmoja kati ya wabunge wawili tu ambao tulipata kura zaidi ya 100,000 (mwingine aliyechaguliwa kwa kura zaidi ya 100,000 ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu').

Nilipata kura 103,000, lakini ukichukua wanachama wote wa CUF Temeke, hawawezi kufika idadi hiyo. Kwa hiyo, nina kura nyingi sana ambazo si za wanachama na watu mbalimbali wa vyama vingine.

Chama ni njia, ndiyo tiketi kwa sababu ndiyo hasa sheria inavyotutaka uwe na chama upite huko, lakini pia tunaheshimu kwa maana chama ndiyo kinabeba dhamana ya nchi na mimi naamini kwenye 'ideology' (sera) ya CUF, hivyo nitaendelea kufanya kazi na CUF, lakini nikiamini kabisa kwamba kura zangu zipo kwa wananchi.

Swali: Ni kiasi gani cha fedha za Mfuko wa Barabara kimetumwa kwenye jimbo lako katika miaka miwili ya utawaka wa Rais John Magufuli? Kinatosha?

Mtolea: Fedha hiyo haipelekwi kwa kupitia Mfuko wa Jimbo zinapitia kwenye halmashauri na halmashauri yangu ina majimbo mawili; Jimbo la Mbagala na Jimbo la Temeke.

Mwaka 2016/17, tulikuwa na bajeti ya Sh. bilioni 2.8 na 2017/18 halmashauri imetengewa Sh. bilioni 3.4. Sina'figure' (takwimu) kamili ya fedha zilizopokewa, lakini zilikuwa zaidi ya asilimia 70.

Swali: Nini maoni yako, kati ya mbunge na mkuu wa wilaya, nani mkubwa?

Mtolea: Ni utashi mdogo kwa mbunge na DC (mkuu wa wilaya) wanatafuta kujua nani mkubwa kwa sababu ni kama kutaka kuhoji Rais na Spika nani mkubwa.

Hiyo ni mihimili miwili tofauti na hawa watu (DC na mbunge) wanatoka kwenye mihimili miwili tofauti, hakuna namna ambayo unaweza kusema huyu ni mkubwa huyu mdogo.

Wanachotakiwa wote ni viongozi, wanahitaji kuheshimiana na sifa ya kiongozi mzuri ni kujishusha. Kiongozi anayetafuta kujua kama yeye ni mkubwa kuliko mwenzake, basi yeye ni tatizo na hana sifa za uongozi.

Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba DC na mbunge wanahitaji tu kuheshimiana badala ya kutafuta nani mkubwa kati yao kwa sababu wote wanatoka maeneo tofauti. DC anatoka kwa Rais na mbunge anatoka bungeni kwa Spika.

Ukitaka kujua nani mkubwa kati yao, inabidi uanze kuangalia mbunge anaripoti kwa watu wangapi na DC anaripoti kwa watu wangapi.

Ukitaka kutafuta hilo, utagundua kwamba mbunge naye ni mkubwa sana kwa sababu anaripoti kwa Spika na Spika ndiye kiongozi mkuu wa mhimili wa bunge ambapo kwa 'executive' (serikali) mkubwa zaidi ni Rais na wa pili yake anakuwa Makamu wa Rais.

Kwa maana hiyo, 'level' ya mbunge ni sawa na Makamu wa Rais 'which is not true' (jambo ambalo si sahihi) kwa sababu kila mhimili una ngazi zake.

Swali: Una maoni gani juu ya wakuu wa wilaya wanaotoa amri za kuwaweka ndani wabunge na kama ukiamriwa kuwekwa ndani utachukua hatua gani?

Mtolea: Kati ya vitu vilivyokuwamo kwenye mapendekezo ya wananchi kwenye katiba mpya ni huo mgawanyo wa madaraka; kwamba utawala umekuwa na nguvu nyingi sana ambazo baadhi ya 'wanazi-misuse'.

Kwamba maDC sasa wanakamata si wabunge tu, bali hata wananchi wa kawaida, kila wakienda kwenye mikutano lazima wamdhalilishe mtu, achukuliwe na awekwe ndani zaidi ya hata hizo saa 48 ambazo wanatakiwa kuwaweka.

Sasa, haya ni matumizi mabaya ya madaraka ya maDC. Na hii inatokana na kwamba hawa watu, maDC wengi wameteuliwa tu 'from nowhere' (kutoka kusikojulikana), yaani mtu alikuwa tu sijui ananyoa saluni huko anateuliwa anakwenda kuwa DC, mtu alikuwa mwanachama mzuri wa CCM anateuliwa anakwenda kuwa DC.

Kwa hiyo, ile 'management skills' (ujuzi wa kutawala) hawana. Wanafanyakazi kwa kutaka sifa, anamdhalilisha mtu ili aweze kupata sifa. Ni changamoto za utawala ambayo timu ya 'executive' huko haikujipanga vizuri kukabiliana na upungufu huu na hivi hawana semina elekezi, matatizo haya yatakuwa yanaendelea.

Kama ikitokea nimewekwa ndani, nimewekwa tu, lakini baadaye nitafuatilia haki zangu za msingi.

Swali: Jimbo la Temeke linakabiliwa na changamoto zipi kwa sasa?
Mtolea: Changamoto kubwa ni idadi kubwa ya watu. Eneo limekwisha, lakini idadi ya watu inaongezeka sana kwa sababu kwanza watu wanaamini Temeke ni sehemu ambayo unaweza kuishi kwa maisha nafuu zaidi kuliko maeneo mengine ya Dar es Salaam. Kwa hiyo dhana hii inaifanya Temeke kuwa na idadi kubwa sana ya watu. Tuna watu zaidi ya 780,000 hivi.

Kati ya hao, unakuta asilimia 41 ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 30 ambalo ni kundi kubwa ambalo asilimia 21 ni vijana ambao hawana ajira, hapa unazungumzia miaka 13-17, wengi hawana ajira.

Sasa, kundi hilo likiwa halina ajira ni lazima watajiingiza kwenye uhalifu; kuna matukio yanatokea ya vijana kujiingiza kwenye dawa za kulevya, mimba za utotoni, vikundi vya kihalifu mnasikia 'Panya Road' na vingine vinakuwa vinatokea.

Ndiyo maana tukizungumzia tatizo kubwa la ajira lipo sana. Kuna tatizo pia la miundombinu kwa maeneo mengi kuwa ujenzi holela. 'of course' tuna mradi wa Benki ya Dunia (WB) ambao baadhi ya kata zinapitiwa, lakini bado tatizo ni kubwa sana. Ikinyesha mvua kidogo inakuwa tafrani.

Mfumo wa maji ya bomba bado haujaenea Temeke, tunatumia sana visima badala ya maji ya bomba. Mabomba ya Ruvu Juu na Ruvu Chini yamepita, yametuzunguka, lakini Dawasco hawajatuunganisha.

Pia kuna mrundikano mkubwa sana wa wagonjwa kwenye zahanati zetu. Kama nilivyosema hapo awali, idadi ya watu ni kubwa.
Sera ya serikali inataka kila kata kuwa na kituo cha afya, lakini sisi tuna zahanati kwenye kata, hivyo kuna vitu vingi ambavyo havipatikani pale.

Tumejaribu kuziboresha na zingine zinazalisha, zinafanya kazi saa 24 japo ni zahanati, lakini bado mrundikano wa watu unakuwa mkubwa kuliko uwezo wenyewe. Kata moja unakuta ina watu 80,000, watu 90,000. Kwa hiyo kwa siku unakuta zahanati tu kwa mwezi inazalisha kina mama 50. Hii ni idadi kubwa kuliko hata baadhi ya hospitali za wilaya huko mikoani.

Huduma za afya ni changamoto. Hospitali yetu ya Rufani ya Temeke na yenyewe inazidiwa sana kwa sababu kwanza ipo hiyo hiyo na pili kijiografia. Watu kutoka mikoa ya kusini nao wanaitumia kama hospitali yao ya rufani. Mfano, kusini tunapakana na Mkuranga, kuna Kibiti na Rufiji.

Wale ni mkoa wa Pwani, hospitali yao ya rufani ni Tumbi, lakini kwa akili ya kawaida mtu hawezi kutoka na mgonjwa Kibiti akavuka Temeke anaitafuta Tumbi. Kwa hiyo, mzigo wote ule unaishia Temeke.

Hata wanaotoka Lindi na Mtwara pia hospitali yao ya kwanza ni Temeke. Kwa hiyo haihudumii tu watu wa Temeke, bali na watu wa idadi tusioijua kutoka mikoa ya jirani. Hii hali hata kwenye bajeti ni changamoto sana kwa sababu bajeti yako utaangalia idadi ya watu katika eneo lako.

Swali: Vipi kuhusu maeneo ya kuzikia Temeke ikizingatiwa kuna taarifa kwamba maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makaburi Dar es Salaam yamejaa?

Mtolea: Bado hatujakuwa na tatizo la maeneo ya kuzikia. Bado maeneo tunayo, tunaendelea kuzikia. Kwa idadi hii ya watu inayoendelea kukua, na Temeke kwa maana ya jimbo, hakuna eneo jipya ambalo unaweza kutenga kwa ajili ya shughuli zingine zozote za kijamii. Kila eneo kwa sasa lina mtu.

Ndiyo maana hata makaburi tunayoyatumia kwa sasa yakijaa tutapata taabu. Kwa hiyo ni jambo la kwanza kulifikiri kuanzia sasa.