MAHOJIANO MAALUM- Mbunge asimulia saa ngumu kuhamia CCM-2

23May 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
MAHOJIANO MAALUM- Mbunge asimulia saa ngumu kuhamia CCM-2

DESEMBA 14, mwaka jana, Dk. Godwin Mollel, alitangaza kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Siha na kujivua uanachama wa chama kikuu cha upinzani – Chadema - kisha kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Godwin Mollel.

Katika sehemu ya kwanza ya mahojiano maalum na Dk. Mollel (48) jana, pamoja na mengine, alieleza jinsi ilivyokuwa vigumu kwake kujiunga na CCM.

Alisema uamuzi wa kujiunga na chama tawala hicho aliufanya baada ya kutafakari kwa saa tatu akishauriana na watu wawili aliowaita Watanzania wazalendo.

Ifuatayo ni sehemu ya pili ya mahojiano ya Nipashe na mkurugenzi huyo wa zamani wa Hospitali ya Selian Arusha:-

SWALI: Ni lini hasa ulikaa na kugundua kuwa unapoteza bure muda wa maendeleo Chadema na hivyo kuamua kuhamia CCM? 

DK. MOLLEL: Niligundua mara moja baada ya kuingia bungeni. Yaani baada tu ya kushinda sikuwa na amani kabisa. 

Nilianza kuona hoja nyingi ni za kitoto. Mimi ni mtu wa kazi, si maneno. Halafu mimi napenda kuwa kiongozi, si mwanaharakati. 

Tabia ya wanaharakati ni watu fulani ambao ni wazuri sana kuelezea matatizo, lakini ukiwatuma kufanya hawezi. 

Yaani ni mtu tu ambaye muda wote analaumu, ukifagia atakwambia 'umefagia lakini umeweka takataka mahali pasipofaa', ukiondoa takataka anakwambia 'ulitakiwa kabla ya kufagia uwashe moto'. Yaani ni mtu fulani hivi ambaye ukimwambia yeye afagie hata hajui ashikeje ufagio. 

Kwa hiyo, nilikuja nikagundua niko katikati ya kikundi cha watu fulani ambao wanakuwa 'remoted' (wanaongozwa) na watu wengine. Hawana mawazo yao binafsi.

Lakini pia nikajikuta niko katika kikundi cha watu ambacho hakina sera mbadala. Mimi niliamini kwamba Chadema ingekuwa na sera mbadala; kwamba wakati CCM wanafanya haya, sisi tunaonyesha tutayafanyaje haya vizuri zaidi.

Sasa mimi siwezi kuwa kwenye chama ambacho muda mwingi natakiwa kujiuza kwa kutumia makosa ya viongozi wa serikali. Siwezi kungojea mtu fulani akosee ndiyo naanza kufanya siasa, natakiwa nieleze nitafanya nini.

Kwa mfano, Chadema wanapata ruzuku kubwa lakini limetokea sakata la hivi karibuni bungeni la kushindwa kuajiri watumishi wanne kwa ajili ya Kambi Rasmi ya Upinzani na wakawa wanajaribu kumwambia Spika awasaidie kulipa watumishi wale. 

Tulitegemea kwamba wakati wanajadili na Spika, ni haki yao kujadili, ilitakiwa watumie ofisi yao ya kanda ya hapa Dodoma na kuwalipa wale watu kwa kutumia ruzuku ya chama ili shughuli za kambi ziendelee wakisubiri utaratibu wa ajira za Spika, lakini hawafanyi hivyo.

CCM kwenye baadhi ya wilaya inaweza kujilipa yenyewe mishahara bila hata kutegemea ruzuku ya serikali kwa sababu imewekeza kwenye miradi, tofauti na Chadema.

Kwa hiyo, mapema sana nilianza kujihisi siko mahali sahihi. Nilihisi siko sehemu sahihi ndiyo maana nikafikiria kuondoka lakini nilijaribu kuwashauri, hawakunielewa. 

Kibaya zaidi, kwenye suala la madini nilitukanwa matusi makubwa sana na wabunge wa Chadema kwenye makundi ya WhatsApp ya Chadema, eti kisa tu nimewashauri kwamba suala la muswada huu litatuletea shida kisiasa. Kikubwa tuunge mkono jitihada za Rais.

Mimi mwenyewe niliwahi kuandaa muswada kuhusu rasilimali za nchi na nilifanya 'research' (utafiti) nikabaini njia sahihi ya kwenda nayo ni hiyo aliyochukua Rais lakini hawakunielewa. Nafikiri kuna wafanyabiashara wanaipotosha Chadema.

Sasa, mimi ni mtu ambaye nataka niongozwe na taratibu za nchi yangu na si wafanyabiashara au kikundi fulani cha watu.

SWALI: Matumaini ni makubwa kiasi gani kwamba Dk. Mollel atarejea hapa bungeni 2020?

DK. MOLLEL: Kwanza, suala la msingi si mimi kuwa bungeni. Mimi nimewekeza zaidi kwenye kufanya wananchi wapate kile nilichoahidi. Kikubwa ninachokiangalia si mimi kuwa bungeni. Mimi sasa nimehamia CCM, ninachokiangalia kwa sasa ni CCM kushinda uchaguzi ujao kwenye jimbo langu. 

Hata kama si mimi nitakayekuja bungeni mwaka 2020, lakini kiwe ni Chama Cha Mapinduzi kitakacholeta mbunge hapa kutoka Siha. 

Kwa hiyo, mimi kinachoniumiza kichwa ni mimi leo kurudi CCM halafu keshokutwa Chadema ikashinda tena.

Ninachotaka hata kama mimi sitakuwa mbunge, aje mtu mwingine wa CCM. Kama nilivyojiuzulu nikiwa sijui kama nitarudishwa tena kuwa 'candidate' (mgombea) wa CCM, nilikuwa tayari kuachia ngazi.

Kwa wilaya zetu hizo za vijijini, Chadema wamepoteza mwelekeo, wamekuwa kikundi ambacho hakitetei tena maslahi ya wananchi, wamekuwa kikundi cha watu wajanja wajanja wachache wanaotetea maslahi yao binafsi.

Yaani, ndani ya Chadema tulijikuta tunawaingiza wananchi kwenye mivutano ambayo si ya lazima. Rais anakwenda huku, sisi tunakwenda sehemu tofauti.

SWALI: Kufuatia Bunge kuridhia Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris mapema mwezi uliopita, nchi inatakiwa kuwa makini sana na masuala ya uchafuzi wa mazingira. Mkataba huu utaathiri vipi jitihada za ujenzi wa viwanda katika jimbo lako ambalo lipo nyuma katika nyanja hiyo ukiacha mashamba makubwa? 

DK. MOLLEL: Kwanza nakushukuru kwa sababu unatambua kwamba Wilaya ya Siha ina mashamba makubwa sana. Nafikiri utambue zaidi kwamba ina mashamba ambayo hayaisaidii na yanatumika vibaya.

Lakini vilevile ni ardhi ambayo hailinufaishi taifa. Ni jambo la msingi sana kutambua hilo. Ninachoweza kusema, sioni kwamba huu mkataba una shida, umeboresha na wala hauwezi kuzuia viwanda. 

Tusingekuwa na huu mkataba maana yake, hata tukijenga viwanda Siha, tukipata fedha tutaitumia kuwatibu wagonjwa wa kansa baadaye. Kwa hiyo, haina manufaa yoyote.

Lakini ukiangalia kama tutakuwa na viwanda ambavyo mwisho wa siku vinaacha wananchi wetu wakiwa na magonjwa, sumu zikiwaingia na tunakuwa na viwanda ambavyo mwisho wa siku vinakuwa vinasababisha uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa, baadaye tuanze kupata ukame, tuanze kupata mvua ambazo ziko juu ya wastani, vinaumiza wananchi, bado huwezi kusema umefanikiwa kiviwanda.

Kwa hiyo, huu mkataba umekuja wakati mwafaka ambao sasa nchi yetu inaenda kuingia kwenye sera ya viwanda. Naona tunakwenda kupokea viwanda salama.

Bila huu mkataba maana yake tulikuwa tunakwenda kupokea viwanda ambavyo Ulaya vimewaumiza halafu vinaletwa huku vichafu.

Sasa wanaokuja na viwanda vyao, wanakuja na viwanda salama lakini huko nyuma tungepata viwanda ambavyo si salama. Kwangu mimi naliona kwa jicho la manufaa makubwa sana badala ya kuliona kama ni kikwazo.

Na nikueleze tu, ukiangalia gharama ya kuwa na kiwanda kinachozalisha bidhaa za bei rahisi ni kubwa kuliko kuwa na kiwanda kinachozalisha bidhaa za bei ghali lakini kikawa salama.

Hiki cha bei rahisi ambacho kinachafua mazingira, gharama yake ni kubwa hasa kwa kupoteza maisha na nchi kuingia gharama za kutibu magonjwa.

Na baadaye hata vizazi vijavyo tunaweza kuwa na 'generation' ambayo viwanda vikifungwa baadaye, masalia yake yanaingia kwenye chembechembe za urithi na kwa baadaye tunaweza miaka ijayo kuwa tunazaa nyani kwa sababu tu kiwanda fulani kilijengwa sehemu fulani.

SWALI: Baada ya kuchaguliwa tena kuwa mbunge, ahadi ipi kwa wananchi wa Siha umeipa msukumo kuitekeleza? 

DK. MOLLEL: Tayari nimeshaanza kuzitekeleza. Waziri wa Nishati alikwenda Jumatano ya wiki iliyopita, alikuwa kule Siha akizundua miradi ya umeme ambayo imekamilika.

Lakini tatizo kubwa kwenye wilaya yetu hii ya Siha ni ardhi. Kimsingi, wilaya nzima tatizo la ardhi ni kubwa sana. Kule kuna maeneo makubwa sana yanayomilikiwa na serikali na wawekezaji binafsi.

Ya serikali yakitumika vizuri yanaweza kuondoa tatizo la ardhi. Tunahitaji pia wale wawekezaji binafsi ambao wameshindwa kuyaendeleza, utengenezwe mkakati vizuri waweze kuendeleza na wakishindwa, basi ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi.

Ushirika ni kidonda ndugu, ushirika umekufa na umekuwa mali ya watu wachache. Kikubwa ambacho tunataka kukishughulikia kwenye eneo la ushirika ni kuhakikisha kwanza ushirika unafufuliwa na vilevile kuhakikisha ubadhirifu unaondolewa ili ushirika uwe mali ya watu wa Kilimanjaro.

Kibaya zaidi, kila wanapokula fedha za umma, wanaona njia rahisi ya kuzifidia ni kuuza ardhi iliyopo Siha kwa wawekezaji. 

Kuna mambo mengi ya ufisadi ambayo mnyororo wake unaanzia Siha unakwenda mkoani hadi wizarani.

Na nilimwandikia Waziri wa Kilimo nikamweleza kwamba sisi wananchi wa Wilaya ya Siha tunahisi Wizara ya

Kilimo ni sehemu ya ufisadi wa ardhi uliopo wilayani kwetu ilhali kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya makazi.

Tuna tatizo la mipaka kati ya Siha na Arumeru. Watu wameumizwa huko kwa sababu ya masuala ya mipaka. 

Pia kuna eneo ambalo polisi wamekuwa wakipambana sana na wananchi lakini ukiangalia ile ni ardhi ya mila, ilipokwa na wakoloni enzi hizo lakini tuliirudisha baada ya ukoloni. 

Ni eneo ambalo Wamasai tunakwenda kuhiji lakini polisi wanaona kama ni eneo la wazi na wanalitumia kwa mafunzo yao, wanapiga mabomu na kusababisha kuharibika kwa mimba za kina mama.

Lakini pia kuna tatizo kwenye bodi zetu za maji. Rais ameshaliona hilo na ameshaagiza ziwe zinasimamiwa vizuri na ziwekewe utaratibu mzuri wa kukaguliwa. Naamini changamoto ya upatikanaji wa maji inakwenda kutatuliwa haraka Siha. 

Habari Kubwa