MAHOJIANO MAALUM: Mbunge: Polisi wanapambana na kivuli -2

22Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe Jumapili
MAHOJIANO MAALUM: Mbunge: Polisi wanapambana na kivuli -2

KATIKA sehemu ya kwanza ya mahojiano maalum haya wiki iliyopita, Joseph Selasini alipinga vikali kitendo cha polisi kuwatisha watu wanaodaiwa kutaka kuandamana Alhamisi kwa kuhamasishwa na Mange Kimambi, Mtanzania anayeishi Marekani.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.

Mbunge huyo wa Rombo (Chadema) alisema kitendo hicho ni sawa na Jeshi la Polisi linapambana na kivuli kwa kuwa mpaka sasa hakuna mtu aliyewasilisha barua ya maombi kwao ili kupewa kibali cha maandamano hayo.

Selasini (57), pia alizungumzia tukio la kushambuliwa kwa kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) pamoja na kamata kamata ya viongozi, wabunge na madiwani wa vyana vya upinzani inayofanywa na Jeshi la Polisi, akieleza kuwa si ishara njema kwa ustawi wa demokrasia nchini.

Leo katika sehemu ya pili ya mahojiano haya, mbunge huyo anazungumzia masuala mengine ya kitaifa na jimbo lake la Rombo…  

SWALI: Kwa mtazamo wako, unafikiri ipo haja Tanzania kurejea kwenye mfumo wa chama kimoja cha siasa? 

SELASINI: Sisi tumewaambia na tunarudia kuwaambia, hakuna haja ya kupiga watu, hawana sababu ya kubeza watu. Kama wanataka mfumo wa chama kimoja cha siasa, walete muswada hapa bungeni wafute mfumo uliopo sasa.

Lakini ninachokwambia una hasara kubwa katika nchi. Na hii wala haihitaji uende shule, haihitaji uende shule kwa sababu unapopata mawazo mbadala au unapopata upinzani, kuna mawili; kwanza utafikiri zaidi, yaani utafikiria lile ambalo ulikuwa unataka kwenda kuamua utalifikiria mara mbili zaidi, utalipa 'attention' (umakini) kubwa zaidi, lakini pia unaweza ukajikuta yale mawazo mbadala wewe ukayachukua na ukayafanyia kazi.

Watanzania ni mashahidi kwamba tangu tumeanza upinzani, mawazo mengi sana ambayo wapinzani wamekuwa wakiyaibua ndiyo ambayo yamefanyiwa kazi na serikali. 

Hata huyu Rais wa awamu ya tano alipoingia madarakani ni kama amechukua ileile Ilani ya Chadema anaifanyia kazi. Unaona! Kwa hiyo, ukisema kwamba hawa wasiwapo, maana yake umekubali kujifungia kwenye chungu wewe mwenyewe tu, kitu ambacho hutafika.

Kwa hiyo, wazo lolote la kufikiria tukiua upinzani tukidhani ndiyo tutaendelea, Watanzania tutapata shida kubwa sana.

Na si kuua upinzani tu. Wazo lolote la kupunguza idadi ya wapinzani humu ndani (bungeni), litaleta matatizo makubwa sana. Mimi tamaa yangu ni kwamba walau tuwe na wabunge nusu kwa nusu ya upinzani na chama tawala. Nchi itakwenda vizuri zaidi. Mambo ya ndiyo mzee, ndiyo mzee yatakwisha.

SWALI: Kuna wimbi la wanasiasa hasa wa upinzani kujiuzulu nafasi zao za uongozi na kutangaza kuhamia CCM. Je, tutarajie kuona hili kwa Mbunge wa Rombo?

SELASINI: Kwanza; kuniuliza swali kama hilo ni kumnitukana. Kuniuliza mimi Joseph Selasini kwamba naweza nikatoka upinzani nikarudi CCM ni kunitukana.

Kwa wale wasiojua ni kwamba waasisi wa mageuzi hapa bungeni tuko wachache sana. Mimi ni mmoja kati ya watu tulioanzisha huu upinzani. Nina imani na tulichoamua. Niko humu kwenye upinzani tangu mwaka 1990.

Hawa kina Antony Komu, kina (James) Mbatia na hao wengine wamefukuzwa chuo kikuu wametukuta tukawalea. 

Kwa hiyo mimi kutoka upinzani ni sawa kuua mtoto ambaye mimba nilibeba mimi na kuzaa. Mama wa aina hiyo ni shetani, siyo mama wa kawaida.

Lakini, sababu zile zilizofanya tukaanzisha hiyo zipo mpaka leo, hazijaisha. Mimi ninaamini katika kushindanisha hoja kwenye jamii.

Hata ndani ya familia, ninaogopa sana kuwa na kizazi ambacho ninakielekeza 'watoto wangu nendeni hivi' halafu wote kweli mbio wanatimua kufuata nilichosema, naogopa sana. Ukiwa na kizazi kama hicho ni sawa na kwamba huna kizazi.

Mimi nawapenda watoto ambao nikiwaambia leo kwamba 'watoto kesho tutaenda shambani halafu wanahoji 'baba tutakwenda saa ngapi?', Nasema saa tatu, lakini wanahoji 'baba kumbuka tukienda saa tatu shambani, kuna hawa ng'ombe ambao tunatakiwa tuwapeleke kwa dume. Sasa tupangane vizuri'.

Kwa hiyo, mimi ni muumini wa hali hiyo. Na mimi nimezaliwa katika kizazi cha siasa. Babu yangu alikuwa Mangi, maana yake ni mtawala, yaani mtemi. Hilo la kwanza.

La pili, baba yangu ni mmoja kati ya wazee walioleta chama cha Tanganyika African National Union (TANU), katika Mkoa wa Kilimanjaro, Mzee Alkael Mbowe, ambaye ni baba yake Freeman Mbowe na wengine. Na baba yangu amekuwa diwani mpaka alipofariki dunia Julai 30, 2012, akiwa na umri wa miaka 91.

Fikiria wenzake ndani ya CCM walimwamini, wakamwachia kiti cha udiwani mpaka akiwa na miaka 91, alikuwa mtu wa aina gani? Na katika familia yeye alikuwa diwani wa CCM, mimi ni mbunge wa Chadema na tulifanya kazi vizuri kabisa.

Na ikifika mahali hoja za halmashauri, kwa sababu wote tulikuwa halmashauri moja, tunakaa tunakubaliana kwamba aah, hii hapana! Tunakwenda.

Kwa hiyo, huwezi kuisaidia serikali eti mbunge wa upinzani ukaifuata serikali. Unaisaidia vizuri zaidi kwa kuipa mawazo mbadala ili kama ikichukua yale mawazo iende vizuri zaidi.

Huwezi ukasema unakwenda chama tawala eti ili uwe na uwezo wa kuhudumia jimbo. Ukifanya hivyo, maana yake ni sawa sawa na kutangazia umma kwamba hiki chama na serikali ni ya kibaguzi, inabagua yale majimbo ya wapinzani kama hoja ndiyo hiyo.

Kwamba nikienda huku ndiko serikali itahudumia jimbo langu vizuri zaidi. Maana yake unataka kusema hiyo serikali inabagua majimbo ya wapinzani. Na kama ni hivyo, serikali hiyo itakuwa ni serikali dhalimu kwa sababu majimbo yanayoongozwa na wapinzani yana wananchi ambao wanalipa kodi na kodi ndiyo zinatoa haduma.

Utasemaje kwamba nikienda huko ndipo jimbo langu litahudumiwa? Wewe unaona jimbo lako halihudumiwi kwa sababu labda uko mbali na serikali, uko mbali na wananchi, hujui matatizo ya jimbo lako, hujui namna ya kuyawasilisha n.k.

Na wengi waliohama usifikiri kwa sababu ya kwenda kupata hizo huduma. No (hapana), wamehama kwa sababu ya njaa zao kwa sababu wengi wanatuambia wameshawishiwa na wamepata kidogo.

Sasa mimi utaninunua kwa shilingi ngapi ambayo itakidhi utu wangu pamoja na utu wa wale walionileta bungeni? Huwezi! Kwa hiyo, hilo 'forget about it' (sahau kuhusu hilo).

SWALI: Serikali imesema mchakato wa Katiba Mpya kwa sasa haumo kwenye vipaumbele vyake. Una maoni gani kuhusu hili?

SELASINI: Hawa wanafanya utani kwa sababu wanaandika historia na historia inaishi. Hawajui kwamba hii nchi baada ya miaka kadhaa itatawaliwa na kiongozi gani. 

Fedha zilizotumika kwa ajili ya mchakato wa Katiba Mpya, mabilioni ya shilingi hayakuwa mali ya Jakaya, wala si mali ya viongozi wa sasa wa serikali. Itafikia mahali Watanzania watadai fedha ambazo zimetumika katika mchakato wa Katiba Mpya, ni nani mhusika nazo achukuliwe hatua.

Kwa sababu wanachokifanya maana yake ni kwamba kodi za wananchi zinaweza kutumika tu kwa jinsi wanavyotaka. Na hii mimi inaniuma sana. 

Ni kama unavyoona hapa Dodoma, kimejengwa kituo cha mabasi pale kwa fedha za wananchi, wameenda wamevunja, kimejengwa kile kingine pale, wameenda wamevunja.

Haiwezekani fedha za wananchi zikachezewa namna hiyo. Halafu lazima waelewe Katiba haiandikwi kwa matamanio ya watawala, Katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa. 

Sasa, hawa wataliwa ambao ni wananchi kwa ujumla wanasema 'tunataka turekebishe ule mkataba wetu, sawa na mkataba wa biashara. Wewe umeingia mkataba wa biashara na mtu na umeona ule mkataba hauna maslahi, si ni lazima muitane mrekebishe!

Wananchi kwa makundi yao kupitia viongozi wa dini, kupitia taasisi za kijamii, kupitia vyama vya siasa wanasema 'huu mkataba wetu, hii Katiba yetu kati ya watawala na watawaliwa ina matatizo.

Inawapa baadhi ya watu mamlaka makubwa sana hata ya kutuumiza, inaondoa uhuru wa namna ambavyo tunafanya uchaguzi, inapoka baadhi ya haki zetu sisi kama watawaliwa, tuiandike upya. Huwezi kusimama tu kwa sababu una madaraka makubwa unakataa.

Kuna vitu ambavyo sisi tunavifanya, lakini watoto wetu ambao wako nyuma yetu wanaviona, baada ya muda hawa watoto wataingia madarakani, watafungua mafaili na vitu vingine, kuna watu watajikuta wanashtakiwa wakiwa makaburini wakiwa maiti. Na hiyo mimi naogopa. 

Ukikaa mahali kama mbunge, eeh hata kesho ukiondoka, watu watakukumbuka wakikuta kila kitu kiko vizuri. Lakini haya mambo ya kupinga kitu ambacho ni cha wananchi, si sahihi. Tunahitaji Katiba Mpya sasa kuliko wakati mwingine.

Pengine haya mambo ya kamatakamata ya wapinzani na mambo yanayozungumzwa ya mamlaka ya polisi, mamlaka ya tume ya uchaguzi yangeangaliwa vizuri kwenye Katiba Mpya.

Habari Kubwa