MAHOJIANO MAALUM: Profesa aona tatizo kasi ongezeko la watu nchini

13Jan 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
MAHOJIANO MAALUM: Profesa aona tatizo kasi ongezeko la watu nchini

TOVUTI rasmi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu 55,890,747. Kati yao, wanaume ni 27,356,189 na wanawake 28,534,558.

Kamishna Mhifadhi Misitu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo

Kwa makadirio hayo, idadi imeongezeka kwa watu milioni 43.59 katika kipindi cha miaka 42 kwa kuwa takwimu za NBS zinaonyesha mwaka 1967 (sensa ya watu ya kwanza nchini), Tanzania ilikuwa na watu milioni 12.3, Tanzania Bara ikiwa na watu milioni 11.9 na Zanzibar watu 354,815.

Huku kukiwa na kasi hiyo ya ongezeko la watu, nchi iko katika safari ya kuelekea uchumi wa kati na mada kuu katika safari hiyo ni ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Juni 1999, Tanzania ilizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo pamoja na mambo mengine, inalenga kupunguza nusu ya watu wanaoishi katika umaskini na kuwafanya wawe katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Wakati safari hiyo ikiwa imeiva, Kamishna Mhifadhi wa Misitu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, anaungana na wadau wengine wanaopaza sauti kuhusu kutoka maeneo tofauti ya kitaifa kuhusu madhara ya kasi ya ongezeko la watu nchini.

Mbali na Profesa Silayo, wadau wengine 'wanaolia' na kasi ya ongezeko la watu nchini ni pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Benjamini Mkapa, ambaye katika kitabu chake cha 'My Life, My Purpose' (Maisha Yangu, Kusudio Langu), anaeleza kile anachokiona nchi kukosa dira sahihi ya kukabiliana na tatizo hilo.

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dodoma wiki iliyopita, Profesa Silayo alielekeza kilio chake kwa baadhi ya watu wanaosaka maeneo mapya na kuelekeza nguvu zao kwenye kuvamia na kubadili matumizi ya maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, hasa misitu na mapori tengefu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na Mtendaji Mkuu huyo wa TFS:-

SWALI: Vipo vilio vya wadau wa uhifadhi na utalii dhidi ya kasi ya ongezeko la watu nchini. TFS mnaichukuliaje kasi hii?

PROFESA SILAYO: Moja ya vikwazo kwetu ni kasi ya ongezeko la watu ukizingatia idadi kubwa ya watu nchini hupenda kutumia nishati itokanayo na mimea kama mkaa, kuni na vitu mbalimbali.

Hili linatupa mtihani mkubwa kutokana na kwamba inahitajika elimu kwa wananchi ili kuepuka kukata miti na kufyeka misitu ovyo, vinginevyo kutasababisha jangwa hapo baadaye.

Ukataji miti unatokana na baadhi ya watu kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na utunzaji bora rasilimali za misitu zilizopo nchini.

Sasa, panapokuwa na mtawanyiko wa watu, moja kwa moja panachangia uvamizi wa hifadhi za misitu na kusababisha uharibifu mkubwa.

Kukishakuwa na mtawanyiko mkubwa, shughuli za ufugaji zinaleta uvamizi, shughili za kilimo zinachangia kukata misitu ovyo, kunakuwa matatizo makubwa ya uharibifu wa hifadhi za misitu.

SWALI: TFS inachukua hatua zipi kuhakikisha kasi ya ongezeko la watu nchini haisababishi kuwa na Tanzania isiyo na misitu?

PROFESA SILAYO: Mikakati iliyopo ni pamoja na kutoa elimu kwa vijiji 150 kuhusu utunzaji na matumizi bora ya ardhi. Tunaamini kwa kufanya hivi, itasaidia kwa kiasi kikubwa jamii kujua umuhimu wa hifadhi ya misitu iliopo nchini.

Mkakati huu umelenga kupunguza matumizi mabaya ya hifadhi za misitu ambayo ina manufaa makubwa katika kuhakikisha uchumi wa nchi na afya za binadamu kutokana na uzalishaji wa hewa safi.

Maeneo ambayo bado hayajapangwa, yanakuwa na ugumu katika kuyasimamia kutokana na mtawanyiko wa watu katika eneo husika.

SWALI: Kwa kasi hii ya ukataji miti, Tanzania itakuwa na misitu katika miaka 100 ijayo?

PROFESA SILAYO: Ili nchi iwe na misitu miaka 100 ijayo, kila mmoja anapaswa kuwa askari wa wenzake katika kuihifadhi na kuilinda, kwa sababu hifadhi za misitu zinahitaji matunzo bora ili ziendelee kushamiri.

Kila mmoja ana haki ya kuitunza misitu vizuri, kwa sababu ni mali yetu wenyewe. Ndiyo maana nasisitiza kila mmoja ni mlinzi wa hifadhi za misitu zilizopo nchini.

Misitu ikitunzwa, ina faida nyingi sana kuliko watu wanavyofikiria. Moja, ikitunzwa inaleta hewa safi, maji yatapatikana kwa wingi na vitu vingine mbalimbali vinavyosababishwa na uwapo wa misitu bora yenye afya nzuri.

Ili tuendelee kuwa na hifadhi nchini, serikali inapaswa kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo wananchi wanaweza kuitumia kufanya maendeleo bila kuathiri hifadhi za misitu zilizopo nchini.

Miradi hiyo ikiwapo na wananchi wakipewa elimu jinsi ya kuitumia, hakuna atakayekata miti na kufyeka misitu ovyo, bila kusahau kwamba zinahitajika jitihada kukabiliana na mtawanyiko wa watu ambao nimeeleza awali kuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira ya hifadhi za misitu zilizopo.

Kwa hiyo, nchi lazima iwe na mikakati ya kuwajengea wananchi maisha bila kutegemea misitu iliopo. Tukumbuke idadi kuwa ya wananchi inatumia nishati ya kuni na mkaa katika kupikia.

Misitu yetu tukiilinda, itaendelea kuleta faida kubwa. Misitu inaleta tiba na vitu vingine vingi ambavyo vinatokana na uwapo wake.
Pia, kuna kila sababu serikali kutenga maeneo kwa ajili ya ufugaji na kilimo ili wakulima na wafugaji kila upande uwe na mipaka yake.

Tumeuanza mwaka wa tano wa uongozi wa serikali ya awamu ya tano. TFS inajivunia nini katika uongozi wa serikali hii?

PROFESA SILAYO: Tunajivunia kuanzisha viwanda vingi vikubwa vinavyotegemea rasilimali za misitu ambavyo vina uwezo wa kuzalisha bidhaa bora kwa matumizi ya wananchi.

Kwa mfano, sasa nguzo bora za umeme zinapatikana nchini. Kuna viwanda vinavyotengeneza nguzo zenye uwezo wa kudumu miaka hamsini.

Kuna viwanda vya misitu vimeboreshwa ambavyo vinaleta faida kubwa, ikiwa ni pamoja na kuchangia kuingiza mapato ya nchi kupitia utalii.

Awali ilikuwa idara ya misitu na wafadhili walikuwapo lakini vitu vingi walifanya kwa manufaa yao tofauti na ilivyo sasa, tunafanya kwa faida yetu.

Hivi sasa misitu inasaidia uzalishaji wa samaki kutokana na maji yaliyopo. Utunzaji na ulinzi wa misitu umechangia kuwa na uhakika wa maji nchini.

Suala usalama liko vizuri kabisa hasa ukizingatia ndani ya miaka minne, tumeweza kubadilisha kutoka uendeshaji wa kawaida na kuwa Jeshi Usu, imesaidia kwa kiasi kikubwa sana kuimarisha ulinzi na usalama wa hifadhi za misitu yetu.

Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa sababu hivi sasa TFS ina uwezo wa kununua magari 35 kila mwaka na mitambo yake, hilo si jambo dogo wakati awali ilikuwa magari 10 tu.

Usafiri umeimarika kuanzia ngazi ya chini hadi juu na utendaji kazi umekuwa rahisi sana. Kwa kweli tunapaswa kujivunia kutokana na serikali hii.

Kwa upande wa mistu iliyo kisiwani, tuna boti ambazo zina uwezo wa kufanya doria ndani ya bahari ili kudhibiti wahalifu wa misitu. Pia, tumefanikiwa kupandisha hadhi ya misitu tisa, hilo siyo jambo dogo kabisa katika maendeleo.

Misitu mingi ilikuwa na migogoro, lakini tumefanikiwa kuitatua na jamii ya maeneo hayo sasa inatuamini na tunashirikiana nayo katika kutunza hifadhi za misitu mbalimbali iliyopo nchini.

SWALI: TFS inakabiliwa na vikwazo vipi vikubwa kwa sasa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria?

PROFESA SILAYO: Kikwazo kikubwa ni uvamizi wa misitu unaofanywa na jamii inayozunguka misitu, lakini kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuidhibiti kwa sababu moja ya mkakati tuliojiwekea ni kutoa elimu vijijini na mkakati tulionao sasa ni kuanza na vijiji 150 halafu tutaendelea na vingine.

Tukishakamilisha utoaji wa elimu kwa jamii, tutakuwa na uhakika wa ulinzi wa hifadhi zetu kwa sababu kila mmoja atakuwa mlinzi wa mwenzake.

Katika kutoa elimu kwa jamii, tumekuwa tukiwasaidia wananchi kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inasaidia kuepusha matumizi mabaya ya misitu.

Ningependa kila mwananchi atumie zaidi gesi na umeme kama mbadala wa kuni na mkaa, ili kuacha kukata miti ovyo. Ifike wakati hifadhi za misitu ziwe za kwanza katika fikra zetu za ulinzi kabla ya kufikia mambo mengine.

SENSA TANZANIA
Mwaka Idadi ya watu Tanzania Bara Zanzibar
1967 12,313,469 11,958,654 354,815
1978 17,512,610 17,512,610 476,111
1988 23,095,878 22,455,193 640,685
2002 34,569,232 33,584,607 984,625
2012 44,928,923 43,625,354 1,303,569
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Habari Kubwa