MAHOJIANO MAALUM Profesa ataka matuta yaondolewe barabarani

21Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
MAHOJIANO MAALUM Profesa ataka matuta yaondolewe barabarani

Profesa Norman Sigalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ameishauri serikali kuondoa matuta yote yaliyojengwa barabarani kutokana na kile anachodai yanasababisha uharibifu wa magari na barabara zenyewe.

Profesa Norman Sigalla.

Msomi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Makete (CCM) pia ameitaka serikali kutoa fasili sahihi barabara inazozijenga ni kwa ajili ya magari au watu.

Katika mahojiano na Nipashe mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Prof. Sigalla (47), ambaye ni mbobezi katika masuala ya uchumi, fedha, benki, biashara na utawala, mbali na kutaka fasili sahihi ya matumizi ya barabara nchini, alizungumzia kuhusu hali ya miundombinu na uchumi wa nchi.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na msomi huyo:

SWALI: Umekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kipindi cha kutosha. Hebu tueleze mafanikio na matatizo, tuseme 10 unayoyaona katika ujenzi na utunzaji wa barabara nchini.

PROF. SIGALLA: La kwanza; kama Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, niseme tu kwamba, kubwa kuliko yote ni changamoto.

Miundombinu inajengwa vizuri lakini ni lazima taasisi zinazosimamia barabara zifasili kwa usahihi chanzo cha ajali zetu maana yake mtazamo umekuwa ni kana kwamba ajali zote zinasababishwa na mwendokasi.

Sasa sina hakika kama kitaalamu imekaa hivyo. Dereva mzembe si lazima awe anayeenda kasi. Unaweza ukawa unaenda 'speed' (mwendo) ya kilomita 60 kwa saa lakini 'una-overtake' (unayapita) magari yaliyokutangulia mahali ambapo hapapaswi kufanya hivyo.

Unaweza ukawa unatembea 'speed' 40 lakini husimami unapotakiwa kusimama, unaweza ukatembea 'speed' 60 au 70 lakini hukai upande wa kwako, wewe lazima utasababisha ajali tu.

Unaweza kuendesha 'speed' 80 au 90 au 'speed' ndogo kabisa yotote ile lakini gari lako hujapima matairi kama yana upepo unaofaa au la. Unaweza ukaendesha 'speed' ndogo lakini kama hujatazama uchakavu wa matairi yako au mwaka ulionunua matairi yako, maana matairi haya nayo yana muda wake wa matumizi, mengi ni miaka mitatu.

Kwa hiyo, kama umenunua tairi ambalo mfano, lililotengenezwa mwaka 2013 na leo ni mwaka 2017, hata kama ni jipya, hilo tairi litakupasukia tu likiwa kwenye gari. Kwa hiyo, vyanzo vya ajali ni vingi zaidi ya mwendo. Hilo ni la kwanza ambalo naona ni changamoto.

La pili ni kufasili kiusahihi kwamba, hivi barabara ni kwa ajili ya watu au ni kwa ajili ya magari? Ukienda Ulaya yote, nchi zote zilizoendelea barabara ni kwa ajili ya magari. Unayechukua 'risky' ya kuvuka barabara ni mtu.

Sasa nchi changa nyingi fasili haijakaa vizuri. Barabara ni kwa ajili ya magari lakini tunachotaka sisi huku barabara ziwe za magari na watembea kwa miguu. Ukifika hapo sasa utalazimika kila sehemu uweke vidhibiti mwendo vingi. Kwa hiyo, hilo ni tatizo.

Tatizo la tatu ni kwamba, mamlaka zinazosimamia barabara zifasili kiusahihi pale ambapo barabara imepita mahali ambapo hapana watu na watu wakaamua kuifuata barabara, bado baada ya muda unaweka matuta.

Kitaalamu kabisa ni kwamba, matuta yanachangia uchakavu wa barabara na magari yenyewe, ndiyo maana kila unapofika mahali ambapo kuna tuta, unakuta lami inatitia kwa sababu unamfanya aliyekuwa anaendesha gari, tuseme 'speed' 80 au 100 kwa saa, anapokaribia kwenye tuta, ashike breki apungumze mwendo.

Kwa hiyo, mkandamizo kati ya matairi na barabara unakuwa mkubwa, ndiyo maana unakuta panatitia. Lakini angalia pia aina ya matuta yanayowekwa; yanasaidia uchakavu wa magari na barabara yenyewe.

Matuta pia kitaalamu, pengine mamlaka za serikali zifanye utafiti, yanachangia msongamano wa magari. Kwa mfano, kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam ni kilomita 860 hivi. Ukitoka Mwanza mpaka Dar es Salaam ni kilomita nyingi tu, zaidi ya 1,000. Lakini ukitoka Arusha mpaka Dar es Salaam ni zaidi ya kilomita 600, kama 660 hivi.

Kama karibu theluthi moja ya njia hiyo, hata ukiweka moja ya tano (1/5) ya njia hiyo, magari yanalazimika kutembea kwa 'speed' 30. Maana yake akitokea dereva anayetii hiyo njia, hawezi kuingia Dar es Salaam siku hiyo. Lazima ataingia usiku wa manane au kesho yake.

(Matuta) yanasababisha foleni. Kivipi? Utaona wanalazimika kuyakusanya magari yote, yanayotoka jiji la Arusha, yanayotoka Mwanza, yanayotoka kusini unayalazimisha yaingie Dar es Salaam kwa muda unaofanana.

Ndiyo maana sasa ukifika Kibaha tu ile unaanza kukutana na foleni kwa sababu gari lililotoka saa 12 Moshi ambalo kama lingeenda wastani wa kawaida wa 'speed' km 100 au 120 kwa saa, huku vitu vingine vikiwa vimeangaliwa vizuri; kwa maana ya matairi mazuri, dereva ana leseni nzuri na injini imefanyiwa 'services' (ukaguzi). Eeeh, kama una dereva mzuri, 'speed' itasaidia kupunguza msongamano.

Badala ya kutulazimisha watu wote sasa tutumie 'speed' 30 kutoka Kibaha kwenda Dar es Salaam ni lazima kama umefika saa moja jioni Kibaha, utaingia Dar es Salaam saa nne au saa tano usiku mahali ambapo pana umbali wa kilomita 40. Kwanini? Kwa sababu magari yote yamesimama.

Ndiyo maana nasema mamlaka za serikali zifasili, hivi barabara ni kwa ajili ya magari au ni kwa ajili ya waenda kwa miguu?

Ukipata fasili sahihi, utakuja na sheria na utakuja na utaratibu wa kusema ninyi watembea kwa miguu tembeeni pembeni mwa barabara, yaani kwenye eneo ambalo limewekwa maalum kwa ajili ya watembea kwa miguu.

Na ukitaka kuvuka barabara vukia kwenye eneo ambalo lina alama za kuvuka. Ukivuka eneo jingine lolote, uvuke kwa gharama zako mwenyewe. Eeeh... ifanyike hivyo! Utaondoa haya malalamiko mengi.

Tumepita mahali fulani tukaona kuna ajali lakini nyumba ya karibu na barabara iko kilomita moja (kutoka barabarani).. Mtoto wa miaka mitatu amegongwa barabarani, kwa hiyo wananchi wanataka matuta yawekwe. Sasa tukauliza, 'mama unamwachaje mtoto wa miaka mitatu anavuka barabara peke yake?'

Mamlaka za serikali pia ziepuke mihemko. Siyo kwa sababu tu dharura imetokea, mtu au mnyama amegongwa basi gharama yake ni kuadhibu wananchi wote na madereva wote Tanzania nzima kwa kuweka matuta.

Ni vizuri kuangalia kwamba mtu aliyevunja sheria aadhibiwe yeye lakini siyo sasa unawaadhibu Watanzania wote au waendesha magari wote kwa kuweka matuta.

Mafanikio ni makubwa sana. Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana ya kuendeleza miundombinu na ninamshukuru Mungu.

Mimi binafsi namshukuru Mungu kabisa kwa sababu tumepata marais watano mfululizo ambao kila mmoja anajenga kwa ufasaha kwa Rais aliyetangulia. Ndiyo faida ninayofurahia mimi na ninamshukuru Mungu sana.

Mzee Nyerere alipoondoka, alipoingia Mzee Mwinyi alijenga kwa ustadi sana pale Mwalimu Nyerere alipoishia. Kafungua mipaka ya Kenya ambayo ilikuwa imefungwa, akafanyia marekebisho bidhaa zote zikawa zinaingia nchini ambazo zilikuwa zimezuiwa, mambo yakawa vizuri.

Mzee Mkapa alipoingia akatengeneza mifumo ya sera kutengeneza sheria za kuliongoza taifa muda mrefu ndo maana akaja mpaka na 'policy statement' ya mwaka 1999 inayoelezea ushindani wa biashara bila kuonewa.

Ndiyo maana akaanzisha Sumatra, akaanzisha TCRA, Ewura na mashirika mengine haya ya kudhibiti, lakini yasishiriki biashara. Alipokuja Mzee Kikwete naye akafanya kazi hiyo hiyo kwa kuendeleza pale Mkapa aliposimika.

Kumbuka Mzee Mpaka alitengeneza nafasi ya Tanzania kukubalika kukopesheka kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Kwa hiyo, alipokuwa anaondoka, tayari alikuwa amekamilisha mikakati hiyo na Mzee Kikwete alipoingia akaendeleza.

Na kaka yetu wa sasa aliyeingia amefanya kazi nzuri sana ya kuendeleza yale ambayo yaliachwa na wenzake lakini pia kwa kukazia zaidi uimarishaji wa miundombinu kama ambavyo wenzake walifanya.

Ndiyo maana nikasema namshukuru sana Mungu kwa serikali hii ya CCM. Vyama vingine yawezekana vikawa vinatoa Rais lakini viongozi wakawa wanakinzana, lakini serikali ya CCM imetoa viongozi ambao kila mmoja anajenga kwa ustadi pale alipoishia mwenzake.

Miondombinu imeimarishwa sana Tanzania lakini changamoto ni chache sana kulinganisha na uhalisia, tunaenda vizuri.

SWALI: Je, kwa matazamo wako huo, uanfikiri huu ni muda mwafaka sasa matuta yaondolewe kwenye barabara za Tanzania?

PROF. SIGALLA: Matuta nadhani ndiyo maelekezo, lakini yanatakiwa yawekwe matuta ambayo hayaharibu gari. Unaweka tuta kubwa lililosambaa ambalo gari likipanda, yaani ni alama ya kumwonyesha kwamba punguza mwendo, unaingia eneo ambalo lina watu wengi. Eeeh, siyo alama ya kuharibu gari!

Lakini unaweza kuweka pia kibao tu. Polisi wa usalama barabarani kazi yao ingekuwa sasa kuadhibu ambao hawazingatii vibao. Lakini pia alama ziwekwe kwa kuzingatia weledi.

Kuna alama zingine zimewekwa sehemu; kwamba utumie 'speed' 50 au 60, ni porini kabisa. Unajiuliza wameziweka ili iweje na mahali penyewe wanyama hakuna.

Kama kuna wanyama, weka bango kwamba eneo hili lina ng'ombe wengi, endesha kwa uangalifu.

SWALI: Kwa kuzingatia hali halisi ya miundombinu nchini, unadhani matumaini yapo hai kwamba Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015?

PROF: SIGALLA: Ndiyo! Kwa kuzingatia hali ya miundombinu iliyopo sasa hivi iliyojengwa na serikali zote za CCM; kuanzia ya awamu ya kwanza kwa maana ya Mwalimu Julius Nyerere na awamu ya pili chini ya mzee wetu, baba yangu, Mzee Ali Hassan Mwinyi na

Mzee wetu, Mzee (Benjamin) Mkapa na iliyofanywa na kaka yetu, Dk. Jakaya Kikwete na sasa kaka yetu mwingine, Rais John Pombe Magufuli, mikakati hii ya uimarishaji miundombinu ni wazi itatupeleka kwenye uchumi wa kati.

Tutafika kwa sababu moja ya vitu ambavyo ni chachandu na kichochezi cha maendeleo ni miundombinu bora.

Unapokuwa na miundombinu bora na hasa ya usafirishaji kama anavyofanya Rais wetu, unajihakikishia kwamba mwenye kulima atalima kwa sababu atakuwa na nafasi ya kwenda, lakini mkulima akivuna ana nafasi ya kusafirisha.

Na miundombinu mkiiboresha kwa kawaida ina tabia moja ya kupunguza gharama za usafiri, unapunguza gharama eeeh!

Unapokuwa na barabara nzuri kijijini unakuwa na uhakika kwamba nauli zilizokuwa zinatozwa kwenye eneo husika zitapungua kwa sababu ya ubora wa miundombinu.

Kwa hiyo, itachochea usafirishaji kwa ujumla kwa wanaolima, kwa wanaovuna, kwa wanaosafiri na wanaofuata masoko au bidhaa na mahitaji mengine. Miundombinu ni muhimu kwa namna hiyo.

SWALI: Mchakato wa kufikia uchumi, utaendana na usafirishaji wa mizigo, mitambo na mashine, vyote vizito, kwa ajili ya viwanda vinavyokusudiwa kujengwa. Barabara zetu zitabaki na ubora kiasi gani baada ya miaka saba ijayo?

PROF. SIGALLA: Labda niliseme hili tu kwamba msimamizi wa barabara, Tanroads (Wakala wa Barabara), kwa mfano, ambao sisi tuna dhamana kuisimamia wizara na kwa kuwa tuna nafasi ya kusimamia wizara, msimamizi au taasisi ambayo imepewa madaraka ya kutengeneza barabara kwa maana ya Tanroads, inaangalie vigezo vyote vya kitaalamu.

Na ndiyo maana unakuta kwamba hizi barabara zikishajengwa wana vigezo ambavyo vinajulikana, kwamba ikijengwa kiasi hiki lazima idumu kwa muda wa miaka fulani. Kwa hiyo, hilo sina shaka limechukuliwa umuhimu mkubwa.

SWALI: Pamoja na kuwapo kwa mizani baadhi ya barabara nchini zimeharibika tayari licha ya kujengwa hivi karibuni, mfano barabara ya Morogoro-Dodoma ambayo imetitia katika baadhi ya maeneo. Kwanini?

PROF. SIGALLA: Jambo muhimu hapa si kutitia wala kutokutitia. Muhimu ni kwamba, je katika kititia huko serikali imepata hasara ya fedha zake ilizowekeza?

Sasa jibu lake ni kwamba, utaratibu unaofanywa na mamlaka inayosimamia barabara ni kuwa, ukishamaliza (kujenga) barabara kwa kawaida unapewa muda wa uangalizi kabla hujakabidhi hiyo barabara ili magari yapite.

Usije ukatukabidhi ikaonekana lami ni nzuri kumbe yakipita magari haitafanya vizuri. Kwa hiyo, wanapewa muda wa uangalizi, mara nyingi unakuwa mpaka mwaka mmoja kwa ajili ya kuangalia hii barabara kweli imekidhi vigezo.

Na matengenezo yote yanayotokea ikiharibika kabla ya hapo gharama unabeba wewe uliyejenga, inakuwa kwa gharama zako wewe mwenyewe. Ndiyo utaratibu wa barabara.

Kwa hiyo, kutitia au kutokutitia ni masuala mengi yanayochangia lakini ni muhimu kuzingatia kwamba, je, katika huko kutitia baada ya muda mfupi serikali inapata hasara ya fedha zake? Jibu lake ni kwamba serikali haipati hasara ya fedha zake.

SWALI: Serikali imepania kufufua, pamoja na usafiri wa reli ya kati kwa kiwango cha 'standard gauge', mfumo wa njia ya Tanga na Arusha-Moshi. Huoni kuwa sababu zilizopelekea kufa kwa usafiri wa treni katika njia hizo bado zipo hai ikiwamo kutumia muda mrefu kulinganishwa na mabasi na malori na kwamba hata SG na mkakati mpya vitakufa kifo kilekile?

PROF. SIGALLA: Hiyo hapana. Kwa mfano, unaweza ukaona reli inayojengwa kutoka Kigoma-Tabora-Dar es Salaam na matawi yake ya Mwanza pamoja na Mpanda, na Isaka pia, 'speed' (mwendokasi) yake ni kilomita 160 kwa saa. Hata tungeenda na 'speed' 120 kwa saa, bado ni 'speed' kubwa ukilinganisha na treni za zamani zilizokuwa zinakwenda 'speed' 30 kwa saa.

Eeeh! Kwa hiyo, kwa vyovyote vile sababu za kufa kwa treni za zamani kwa sasa hivi hazipo. Yaani mtu ukitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam unafika mapema kuliko aliyepanda basi.

Na nikuhakikishie tu, watu watayakimbia mabasi. Kwa sababu unaambiwa unatoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kwa muda mfupi sana.

Kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam mtu anakwenda kwa saa tatu tu, eeh! Nani atapanda basi? Itakuwa ngumu sana kwa mtu kupanda basi.

Haimaanishi kwamba hakutakuwapo mabasi, la hasha! Mabasi yatakuwapo kwa sababu bei za mabasi zitarekebishwa, zitashuka. Serikali inafanya kazi nzuri, inafanya vizuri sana.

SWALI: Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kunaendana na safari nyingi za uzinduzi wa miradi mbalimbali ya serikali ukiwa na Rais John Magufuli.

Akiwa jukwaani kuzungumza na wananchi anaonekaka ni mtu mcheshi na mwenye kupenda kuchomeka utani utani kulingana na hadhira. Unaweza usijibu ukiona haifai, vipi mnapokuwa katika mazungumzo baina yetu ambayo si rasmi? Ni utani gani huwa anapenda kukwambia?

PROF. SIGALLA: Siku zote Rais wetu anapenda kusema 'fanyeni kazi'. Hataki ubabaishaji, basi! Yeye anasema tu 'chapeni kazi', 'fanya kazi'. Rais wetu utani wake mkubwa ni kusema 'fanya kazi kwa bidii'.

Rais wetu kama unavyoona na kimsingi viongozi wetu wote kwa maana ya wakuu wote wa nchi, jukwaani kitaalamu tunasema 'utani wa mfalme ni maelekezo'.

Mfalme anaweza akakutania lakini hatanii kwa kukusingizia, anatania kwa kupunguza ukali wa yale maneno lakini ujumbe utakuwa umefika.

Anaweza akasema Mheshimiwa Rais kwa mfano, 'ninyi wabunge, fanyeni kazi bwana, acheni uvivu' halafu akacheka. Hamaanishi vinginevyo, anamaanisha mfanye kazi.

SWALI: Faida ya kuwa na miundombinu bora, barabara za lami kwa mfano, ni pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kwa jamii inakopita.

Kama kamati, mna utaratibu wa jinsi ambavyo kilomita za barabara mpaka sasa zimebadili maisha ya watu ambako zinapita?

PROF. SIGALLA: Siyo kazi ya kamati, siyo kazi ya kamati! Kuna taasisi inayoshughulika na takwimu za uchumi Tanzania ambayo ni mali ya serikali, ipo. Tuna vyombo kama hivyo nchini.

Hizo ndo kazi zake, kujua kama uimarishaji wa miundombinu hii unahamasishaje uchumi, ni taasisi ya serikali inayohusika na takwimu ambayo ipo Dar es Salaam.

Kazi yake ni kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine takwimu za uchumi umekuaje, lakini pia vichocheo vya uchumi huo vinakuaje. Ni jukumu la taasisi hiyo, lakini kamati si kazi yake kujua kukua kwa uchumi barabara zimechangia kwa kiasi gani.

SWALI: Mikoa ya kusini ipo nyuma katika nyanja ya usafirishaji kutokana na kutokuwa na reli na barabara za uhakika zinazounganisha eneo hilo na Dar es Salaam, lakini serikali inakuja na mkakati wa kufungua eneo la kusini kiutalii na kiasi kikubwa cha fedha kimeshatolewa na Benki ya Dunia kufanikisha azma hiyo. Watalii hao watafikaje?

PROF. SIGALLA: La kwanza, nataka nikwambie kwanza utalii ni 'adventure' (mzizimizi/bahatisho). Wapo watu ambao wanapenda kutembelea maeneo kwa sababu tu ya kutokuwa na lami.

Lakini kwa jinsi ulivyoniuliza, niseme tu kwamba barabara za kusini zinaimarishwa, zinaimarishwa! Unaweza ukaona zamani tulikuwa hatuna barabara, kwa mfano inayoweza kutoka Mtwara kuelekea Nanyumbu-Songea.

Hapakuwa na barabara ya lami, lakini sasa unaweza ukatoka Songea kwa lami, kwenda Lindi pia hivyo hivyo.

Kwa sasa miundombinu ya barabara kusini imeimarishwa na inazidi kuimarishwa, ndiyo maana serikali ina mpango wa kujenga reli mpya kuelekea Bambabay kule, kuelekea Liganga na Mchuchuma kupitia Mtwara.

Serikali ipo katika harakati za kupaisha miundombinu, imeenda kuimarisha miundombinu ya bahari, kuongeza kina cha Bandari ya Mtwara ili upande wa kusini pale napo tuwe na bandari kubwa maana pale ni karibu na Beira, tuweze kushinda na Msumbiji.

Lengo ni kusaidia watu wa kusini waboreshe miundombinu yao. Lakini pia barabara za nyanda za juu kusini zinajengwa. Yote hii ni kuimarisha miundombinu ya ukanda huo.

Kwa hiyo, hakuna mahali serikali hii ya awamu ya tano imesahau kujenga na kuimarisha miundombinu na ndiyo maana utalii unakwenda vizuri.

Na ikumbukwe kuwa rafiki mkubwa wa utalii ni viwanja vya ndege. Na ndiyo maana mikoa yote ambayo ina vivutio vya utalii imepewa kipaumbele kwenye viwanja vya ndege.

Na siyo tu mikoa yenye vivutio vya utalii, bali pia hata ile ambayo hifadhi haina, utalii umeimarishwa.

Uwanja wa Ndege wa Mtwara umeimarishwa, nenda Shinyanga, nenda Sumbawanga, Songea, miundombinu imeimarishwa.

Tumeimarisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza, tumeimarisha pale Kagera na tunajenga uwanja wa kutua ndege kubwa pale Chato.

Tunaimarisha Uwanja wa Kilimanjaro (KIA) na viwanja vya ndege vya Arusha. Kwa hiyo, Tanzania tunakwenda vizuri sana katika kuimarisha miundombinu inayochochea utalii.

Na nimesema viwanja vya ndege ni rafiki mkubwa wa utalii.

Habari Kubwa