Mahojiano maalum- Zitto Kabwe auweka kiporo uamuzi wake kujitosa urais

30Jun 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Mahojiano maalum- Zitto Kabwe auweka kiporo uamuzi wake kujitosa urais
  • *Aanika msimamo wa ACT kumpokea Membe
  • *Aanika msimamo wa ACT kumpokea Membe

JOTO la siasa kuelekea uchaguzi mkuu na hasa wa urais, limepamba moto. Ndani ya Chama cha ACT-Wazalendo, nako hali hiyo imetawala, tetesi zikisambaa za Kiongozi Mkuu wa chama, Zitto Kabwe, kuchukua fomu kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano, vivyo hivyo, baadhi ya walio nje ya chama.

Kupata majibu bayana ya hayo, Nipashe ilimtafuta Zitto kupata kauli ya kinywani mwake, hali kadhalika ufafanuzi wa tetesi mbalimbali za uchaguzi na nyinginezo za kisiasa ambazo sasa ndiyo zimetawala jikoni. Zitto ana haya katika ufafanuzi wake:

SWALI: Kuna tetesi kwamba awamu hii hautagombea ubunge na badala yake unafikiria kuwania urais. Kuna ukweli katika hili?

ZITTO: Tetesi za kwamba sitagombea ubunge, ninagombea urais nizichukulie kama tetesi kwa sasa kwa sababu nilieleza hili kwenye mkutano wa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Walileta maombi maalum ya kunitaka nitoe tamko la kwamba mwelekeo wangu wa kisiasa unakuwaje kwa sababu chama kinahitaji mtu ambaye atapeperusha bendera yake.

Niliwashukuru viongozi na wanachama wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ombi lao ambalo walilitoa, lakini nikiwaambia kwamba lazima niende nikafanye mazungumzo na wapigakura wangu wa Jimbo la Kigoma Mjini, ili kukubaliana ni hatua gani sasa inayofuata kuhusiana na mwelekeo wa kisiasa.

Kwa hiyo, hili nitalijibu baada ya kumaliza ziara yangu na mashauriano na viongozi, wanachama, wananchi na wazee wa Mji wa Kigoma na Mkoa wa Kigoma pamoja na mkutano mkuu wa Mkoa wa Kigoma wa Chama cha ACT-Wazalendo ambao tutajadiliana hayo.

Ni lazima tuangalie maslahi mapana ya taifa, lakini vilevile kuangalia na maslahi ya Mkoa wa Kigoma kwa kuwa wao ndiyo wamenifanya niweze kufahamika nchi nzima.

SWALI: Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ameweka wazi kwamba kuna makada wa CCM wanaofikiria kuwania urais kupitia upinzani. Je, ACT mmeshapata ombi lolote?

ZITTO: Suala la Ndugu Benard Membe ninafikiri angepaswa kuulizwa mwenyewe kwa sababu si mwanachama wetu, na kama kuna lolote ambalo linaweza likatokea, hilo ni jambo ambalo tunaweza tukalizungumza baadaye kwa pamoja. Sitaweza kulijibu kwa hatua ya sasa.

SWALI: Siku moja kabla ya Bunge la 11 kuvunjwa, ulisimama bungeni na kuibua hoja ya kupinga uamuzi wa serikali kukusanya mapato ya mamlaka za kihifadhi kwa maana ya Ngorongoro na TANAPA na TAWA. Wewe ni mtaalamu wa uchumi, uamuzi huu una athari zipi kiuchumi?

ZITTO: Kuhusiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) kukusanya mapato ya Ngorongoro na TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa) niliongea bungeni japo kwa kiufupi sana, lakini kiufasaha zaidi ni kwamba, kwa sababu hizi ni mamlaka za uhifadhi, ni vizuri ziwe na uhuru wa kukusanya na kutumia mapato yao, ili kuhakikisha uhifadhi hauporomoki nchini.

Kwa hatua ambayo serikali imechukua kwa kuamua TRA kukusanya mapato haya, maana yake ni kwamba kutakuwa na hatari kubwa sana kwa siku za usoni uhifadhi kuporomoka.

Na hatari hii inaweza kusababisha ujangili kurudi, inaweza kusababisha utalii kuporomoka na hata miundombinu ya msingi katika hifadhi kutokupatiwa huduma inavyostahili na tayari tumeshaambiwa kwamba eeh TANAPA mwaka huu kwa miezi michache iliyopita wameshindwa kulipa mishahara kutokana na madhara ya corona.

Kama TANAPA wana akiba ya kutosha kwenye akaunti zake, mimi nikiwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na mashirika ya umma na baadaye serikali kuu, ninafahamu kwamba TANAPA walikuwa na akiba ya kutosha kabisa kwenye benki kuweza kuendeleza shughuli zao bila wasiwasi wowote hata kama wangekuwa hawana mapato kwa mwaka mzima.

Kitendo kilichotokea kwamba corona imetokea miezi michache tu na baadaye TANAPA hawana fedha ya kulipa mishahara, inaonyesha dhahiri kwamba serikali ilikuwa tayari imeshaanza kutumia fedha za TANAPA kinyume cha taratibu ambazo zipo.

Kwa hiyo, mimi ninadhani serikali kuchukua na kutaka TRA waanze kukusanya vyanzo hivi vya mapato ni tatizo na si sawa kwa mustakabali wa uhifadhi na utalii nchini.

SWALI: Nini hasa kilisababisha ukamatwe na kushikiliwa kwa siku mbili na Jeshi la Polisi wilayani Kilwa wiki iliyopita?

ZITTO: Kama inavyofahamika kwamba sisi tulikuwa na ziara ambayo ilianzia Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Rufiji ambako tulipokea wanachama walikuwa ni madiwani wa vyama vingine takriban wanne katika jumla ya madiwani sita waliotoka upinzani katika Jimbo la Rufiji na siku ya pili tulikuwa tunafanya kazi Kilwa na tulikuwa tumeshaanza kikao chetu cha ndani kwa ajili ya kupokea wanachama wengine wakiwamo madiwani.

Cha kushangaza askari wa Jeshi la Polisi, wakiongozwa na OCD wa Kilwa, Ndugu Banzi, walivamia mkutano ule na kunikamata kwa nguvu pamoja na viongozi wenzangu wanane ambao wote tulipelekwa Kituo cha Polisi Kilwa, tukakaa pale kuanzia saa sita mchana mpaka saa tatu usiku na baadaye tukasafirishwa kwa gari la polisi kwenda Lindi mjini ambako tulifika kwenye saa saba usiku na kukaa ndani hadi asubuhi.

Viongozi wa chama kutoka makao makuu walihakikisha kwamba mwanasheria wa chama anafika, alisafiri usiku kucha ili kututetea na mwanasheria huyo alipofika, juhudi za dhamana zikaanza na ilipofika saa 10 jioni, tukawa tumepewa dhamana.

Sasa, kama nilivyoeleza katika mkutano na wanahabari, kwanza; Jeshi la Polisi lilifanya makosa makubwa kutukamata na kuvunja mkutano wetu kwa sababu tulikuwa na mkutano halali, ulikuwa ni mkutano wa ndani kupokea wanachama na kueneza sera za chama, jambo ambalo linaruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Wala hatukuandamana kama ambavyo polisi wanadai. Kwa hiyo, kitendo cha polisi kuuvamia mkutano wetu, kutukamata, usumbufu, vyote havivumiliki.

Haya yanafanyika dhidi ya upinzani lakini wengine wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, vile vyama tu ambavyo vinasimama na wananchi ndiyo vinaonekana shughuli zao kuzuiwa. Kwa hiyo, hili ni tukio ambalo tunalilaani kwa nguvu zetu zote na tunawataka Jeshi la Polisi waache kuingia kwenye mchakato wa siasa.

SWALI: Kipi unajivunia katika maisha yako ya ubunge?

ZITTO: Kuna vitu vingi sana ambavyo nimefanya nikiwa Mbunge wa Kigoma Mjini na kabla ya hapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Na ni ukweli kwamba siyo peke yangu, bali kwa kushirikana na viongozi wengine na vilevile kutokana na misaada ambayo tunaipata kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kubadilisha hali ya maisha ya watu wa Kigoma.

Sasa, hivyo vitu ni vingi sana, nikianza kuvitaja hapa, sitamaliza kwa sababu kuna vitu ambavyo vinahusiana na maisha ya watu moja kwa moja kwa maana ya masuala ya elimu, afya... lakini vilevile kuna vitu ambavyo vinahusiana na maendeleo ya kimiundombinu na uwekezaji katika Mji wa Kigoma.

Mimi kwangu jambo kubwa ambalo ninajivunia kuliko yote katika kazi zangu za kisiasa kuwawakilisha watu wa Kigoma, ni heshima ambayo watu wa Kigoma wanayo nchini kwa kuwa na kiongozi ambaye ana msimamo kutetea kila sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na hili kwangu ndiyo la muhimu sana.

Zamani ilikuwa watu wa Kigoma wakienda nje ya Mkoa wa Kigoma, wanaona aibu kujisema kwamba wanatoka Mkoa wa Kigoma.

Sasa hivi watu wa Kigoma wanaona ufahari kusema kuwa wanatoka Kigoma na hii ni sehemu ya kazi kubwa sana ambayo tumefanya kuonyesha kuwa Kigoma ni sehemu ya Tanzania na watu wa Kigoma wanastahili haki kama watu wengine wote, lakini bado hatujafikia mwisho kwa sababu bado kuna manyanyaso, ukandamizaji na kunyanyapaa, yote haya tutaweza kuyakamilisha kwa kuendelea kufanya kazi.

Habari Kubwa