Maiti 2 zatambuliwa ajali iliyoua 11

17Jan 2018
Lilian Lugakingira
Nipashe
Maiti 2 zatambuliwa ajali iliyoua 11

MIILI ya watu wengine wawili ambao walipoteza maisha katika ajali ya gari dogo la abiria aina ya Hiace iliyosababisha vifo vya watu 11 mkoani Kagera, imetambuliwa.

Kutambuliwa kwa miili hiyo, kunasababisha jumla ya miili ambayo hadi sasa imetambuliwa kufikia tisa. Miili ambayo haijatambuliwa ni miwili na inaendelea kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali Teule ya Biharamulo.

Akizungumza na gazeti hili Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo,  Grasimus Sebuyoya, alisema waliotambuliwa ni Zainabu Rajab (34), mkazi wa Runzewe mkoani Geita na Juma Shanzo (50), mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma.

Dk. Sebuyoya alisema pia majeruhi watatu wameondolewa katika hospitali hiyo baada ya ndugu zao kuomba wawachukue kwa ajili ya kuwapeleka katika hospitali nyingine.

Aliwataja majeruhi ni Basheka Masinga  ambaye alivunjika miguu yote miwili, na kuwa ndugu zake wameomba kumpeleka Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Ziwa Bugando mkoani Mwanza. 

“Lakini pia Oscar Leonard Sebastian aliyechanika usoni na kushonwa na Juma Samu aliyevunjika mkono na kuumia kifuani, wote wakazi wa Kibondo mkoani Kigoma, wamechukuliwa na ndugu zao baada ya kuomba,” alisema.

Alisema mmoja wa wagonjwa wawili waliobakia hospitalini, Mwaruko Charles, ambaye hajajitambua, uongozi wa hospitali wanafanya utaratibu wa kumwandikia barua, ili kumwamishia Bugando.

“Mgonjwa wa pili, Josephat Otieno raia wa Kenya, hali yake  siyo nzuri, alivunjika mkono ambao inabidi ufungwe kwa kifaa ambacho sisi hapa hospitali hatuna, tunashindwa kumwandikia rufani kwenda Bugando maana hadi sasa hakuna ndugu yake ambaye amefika hapa hospitalini,” alisema. 

Januari 14, 2018 kati ya saa 11 na saa 12 jioni katika eneo la Nyangozi Kata ya Nyantakala Tarafa Rusahunga wilayani Biharamulo, mkoani Kagera, ilitokea ajali ya gari dogo la abiria aina ya Hiace iliyogonga magari mawili ya mizigo  na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi watano. 

Magari yaliyohusika katika ajali hiyo ni Hiace, ambayo ililipita gari lililokuwa mbele yake na kugongana na gari la mizigo lililokuwa likivuta trela. 

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Augustine Ollomi, alisema baada ya kugongana na lori la kwanza la mizigo upande wa kulia, Hiace iliyumba na kukosa mwelekeo na kwenda kuligonga lori lingine na kusababisha vifo hivyo. 

Kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya madereva waliokuwa wakiendesha magari ya mizigo, kamanda Ollomi alisema hawajachukuliwa hatua yoyote. 

“Hawajafanya kosa, mtu ukiwa unatembea katika upande wako na mtu mwingine akakufuata akakugonga una kosa gani?” Alihoji.

Gari hilo la abiria lilikuwa likitoka Kakonko mkoani Kigoma likielekea Kahama mkoani Shinyanga, likiwa na abiria 17.  

 

Habari Kubwa