Maiti 21, siku 3 kanisa moja

30Jul 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Maiti 21, siku 3 kanisa moja

SERIKALI imesema hali inayoendelea nchini kwa sasa kuhusu corona sio nzuri, ikihadharisha wanaopinga chanjo watakapokwenda hospitali na kukuta mitungi ya Oksijeni imekwisha, wataikumbuka.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alitoa angalizo hilo jana mkoani Dar es Salaam alipofungua mkutano mkuu maalum wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alibainisha kuwa katika kanisa moja mkoani Kilimanjaro kumeshuhudiwa kuagwa kwa miili ya watu 21 ndani ya siku tatu.

Akizungumza kwenye mkutano huo ulioudhuriwa na viongozi wa dini, Simbachawene alisema hali inayoendelea nchini sio nzuri na kwa nafasi yake amekuwa akipokea taarifa za kila mkoa na wilaya kuhusu kinachoendelea kila saa.

“Hali siyo nzuri, ingawa wanasema usiseme unaleta hofu, kama hofu au dudu lishafika watu wanaumia unasemaje hofu?
"Hili jambo eleza watu wajue, hofu ni wakati jambo halipo au uwekezano wa kutokea jambo kubwa haupo, linapokuwa kubwa siyo hofu tena, linatakiwa liende ili watu wachukue tahadhari,” alisema.

Waziri huyo alisisitiza: “Hali siyo nzuri, Mkoa wa Kilimanjaro kanisa moja juzi majeneza saba, jana manane, leo sita. Ikitokea unakwenda kwenye Oksijeni halafu mitungi wamegawana imekwisha, utaikumbuka chanjo.

"Kwamba uhai kwao sasa utatokea kwenye Oksijeni halafu mitungi mnagawana inaletwa huku mnapeana kidogo kidogo pale ndipo utaikumbuka chanjo."

Waziri huyo alisema ni bora kuchanja na suala la madhara hakuna dawa ambayo haileti madhara.

“Niwasihi ushujaa mnaoutafuta haupo, bora sisi waoga tuliochanja kuliko shujaa wa kupambana halafu ukapoteza dunia, ninawapongeza sana mwenyekiti kwa kumuunga mkono Rais,” alisema.

Waziri huyo alisema Rais ni nembo ya nchi na aliposema kuchanja, hakufanya hivyo bila kutafakari na kupata ushauri wa wataalamu uliozingatia kila aina ya madhara yatokanayo na chanjo.

“Rais amechanja, wewe nani? Una shaka, yaani unakuwa na mashaka kuliko Rais, yaani Rais anapenda kufa? Nataka kuwaambia kupitia mkutano huu mnapaswa kuwa mfano kwa kuweka uongozi mbele kwenye jambo hili ndugu zangu chanjo ni jambo jema,” alisema.

Kuhusu mkutano huo, aliwataka pamoja na mambo mengine wabadilishe katiba yao ili yeyote atakayekwenda ndani ya jumuiya hiyo kwa nia ovu, hatazungumza kukidhalilisha chombo hicho.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, aliwaomba viongozi wa dini kuonyesha mfano kwa kuchanja katika mkutano huo.

Alisema chanjo hiyo itatolewa kwa utaratibu katika mikoa na makundi mbalimbali yatapatiwa.

Pia alitaka Watanzania kuwapuuza wale wanaoeneza uvumi kuwa chanjo hiyo ina madhara na kubainisha kuwa wanaosema ukiweka fedha inaganda, yuko tayari kutoa Sh. milioni moja kwa atakayefanikisha hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Alhad Mussa, alisema waliomba serikali iwapatie chanjo hiyo ambayo juzi Rais Samia Suluhu Hassan aliizindua kwa kuchanjwa.

Alisema wanamshukuru Rais Samia kwa hekima, busara na weledi katika kuwaelimisha Watanzania kuhusu chanjo hiyo ambayo kwa asilimia 99 imethibitishwa haina madhara.

Alisema jumuiya hiyo inaunga mkono chanjo hiyo inayotolewa kwa hiari na kuwataka Watanzania kuipokea kwa sababu wanaamini serikali haiwezi kuwatakia mabaya watu wake.

“Hata mimi jana (juzi) nilipata chanjo na nipo vizuri, hata yale mambo ya ndani yamezidi kama mnabisha mkaulize nyumbani kwangu. Tusisikilize redio mbao,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alisema tangu amechoma chanjo hiyo hajaona tofauti yoyote.

“Jana (juzi) nimechanjwa, asubuhi nilipoamka nikaangalia ujumbe mfupi kwenye simu, Instagram, WhatsApp watu wananiuliza baada ya kuchanja hali ikoje, kuna madhara yoyote nimepata? Nimewaeleza sijaona tofauti yoyote,” alisema.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe, alisema wanaofanya uchungaji wanaona watu wanakufa wakiwa na uchungu.

“Ushuhuda kwa mtu anayeugua corona kwenye mapafu anasikia kama nyuki 1,000 au zaidi wanamshambulia. Kwa hiyo, ni kifo cha kutisha, corona siyo kitu cha mzaha,” alisema.