Maiti yafukuliwa Dar yavuliwa nguo za ndani

13Apr 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Maiti yafukuliwa Dar yavuliwa nguo za ndani

WATU wasiojulikana wamevunja kaburi na kutoa mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Wizara ya Madini, Mary Maramo, aliyefariki dunia mapema wiki hii na kuzikwa juzi katika makaburi ya Pugu Mwakanga, jijini Dar es Salaam.

kaburi ambalo limefukuliwa.

Mwili huo ulikutwa ukiwa umevuliwa nguo za ndani na kutanuliwa miguu na kisha kuachwa juu ya jeneza kabla ya waliotenda tukio hilo kutimka.

Akizungumza jana katika eneo la tukio, kaka wa marehemu, Deogratius Maramo, alisema juzi walimzika dada yake lakini usiku wa kuamkia jana watu wasiojulikana  walivunja sehemu ya kaburi na kuingia ndani.

Maramo alisema watu hao waliingia na kutoa mwili wa marehemu ndani ya jeneza na kufanya shughuli walizokuwa wamelenga kuzifanya na baadaye waliutelekeza mwili huo juu ya jeneza.

"Asubuhi tulipata taarifa kuwa kaburi limekutwa wazi. Tulipofika tulikuta kweli kaburi limevunjwa, mwili umetolewa kwenye jeneza na ukawekwa juu yake lakini hakuna kitu chochote kilichoibwa," alisema.

Maramo alisema mashada waliyokuwa wameweka juu ya kaburi hayakuguswa na watu hao, hali inayoonyesha hakuwakuwa na lengo la kufanya wizi wa aina yoyote.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mtaalam wa afya, waliufanyia uchunguzi mwili huo na kukubaliana kuuhifadhi tena.

Aidha, fundi aliyejenga kaburi hilo, Josephat Mkelemi, alikuwa wa kwanza kubaini tukio hilo wakati akienda kulimwagilia maji.

"Saa 1:00 asubuhi wakati nakuja kwa ajili ya kumwagilia kaburi, nilishtuka baada ya kukuta likiwa wazi ikabidi kwenda kutoa taarifa kwanza," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Bombani, Gido Benard, ambaye alifika na kushuhudia tukio hilo.

Baada ya uchunguzi, mwili huo ulivalishwa nguo upya na na kurudishwa kwenye jeneza na kurudishwa kaburini kisha kujengewa upya mahali palipokuwa pamevunjwa.

Tukio hilo lilizua taharuki kwa majirani na watu waliokuwa wakipita karibu na makaburi hayo huku mashuhuda wakilihusisha na ushirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Zuberi Chembera, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulihusisha na ushirikina.

"Hatutaki kuthibitisha moja kwa moja kuwa ni ushirikina isipokuwa tunalihusisha tukio hili na ushirikina," alisema Kamanda Chembera.

Alisema juzi mwili wa Mary ulizikwa katika makaburi hayo lakini jana wakati fundi alipoenda kumwagilia alikuta sehemu ya kaburi imevunjwa.

Alisema Jeshi la Polisi walipata taarifa na kwenda kufanya uchunguzi wake na bado wanaendelea kabla ya kutoa taarifa ya kilichofanywa na wahalifu hao.

Kamanda alisema eneo lilipochimbwa kaburi lilikuwa na mteremko, hivyo sehemu ya juu ya kaburi matofali hayakufunikwa na udogo, hivyo wahalifu hao walipavunja na kuingia ndani.

Alisema pia matofali na udongo wa saruji iliyotumika kujenga kaburi hilo haikuwa imara hali ambayo ilikuwa rahisi kwa mhalifu kuvunja.

Habari Kubwa