Maiti yazuiwa Bugando kisa deni

19Oct 2021
Richard Makore
Mwanza
Nipashe
Maiti yazuiwa Bugando kisa deni

HOSPITALI ya Rufani ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza, imedaiwa kuzuia maiti ya Rosemary Morumbe, mkazi wa kijiji cha Kerukerege wilayani Serengeti mkoani Mara, kutokana na kudaiwa Sh. milioni 2.4 za matibabu.

Marehemu Rosemary alifariki dunia usiku wa wiki iliyopita na mwili wake ukahifadhiwa hospitalini hapo kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

Mmoja wa ndugu wa marehemu, Scola Marungu, akizungumza na Nipashe, alisema ndugu yao alitibiwa hospitalini hapo kwa kipindi kirefu na kwamba gharama zote zilikuwa Sh. milioni 6.9.

Alisema familia ilitafuta fedha ikalipa Sh. milioni 4.4, na kwamba zikabaki zaidi ya Sh. milioni ambazo wameshindwa kuzilipa mpaka sasa.

Alisema Jumapili asubuhi alifika hospitalini hapo na kuambiwa na wauguzi kwamba ndugu yao alifariki dunia usiku wa iliyopita na mwili wake umehifadhiwa chumba cha maiti.

Aidha, alisema licha ya kupewa taarifa hiyo, aliambiwa kwamba ndugu yao anadaiwa zaidi ya Sh. milioni 2 ambazo zinatakiwa kulipwa ili wapewe mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Bahati Wajanga, alipoulizwa alisema hajui suala hilo na kuomba kukutana na wanafamilia hao.

"Nipe namba zao niwasiliane nao ili waje ofisini kwangu mimi nipo hapa sasa hivi,'' alisema.

Akizungumza na Nipashe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, alisema msimamo wa serikali ni kutozuia maiti hospitali kama aliyefariki anadaiwa.Alisema huo ndiyo msimamo, lakini alisema suala la utekelezaji ni kitu kingine katika hospitali husika.

Habari Kubwa