Majaliwa acharuka ubadhirifu bil. 1.2/-

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Majaliwa acharuka ubadhirifu bil. 1.2/-

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge, ampeleke Ofisa Kilimo wa mkoa, Bernad Abraham, akakague mradi wa umwagiliaji wa Mpwayungu wilayani Chamwino ili kubaini waliohusika na ubadhirifu wa Sh. bilioni 1.2 za mradi huo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa picha na mtandao

Alitoa agizo hilo juzi baada ya Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde, kumwomba awasaidie kuhusu upotevu wa Sh. bilioni 1.2 zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi wilayani Chamwino, Dodoma alipokea ombi hilo la mbunge wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Mpwayungu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mpwayungu.

Alisema mara baada ya Ofisa Kilimo, Abraham, kukamilisha ukaguzi wa mradi huo wa umwagiliaji apelekewe taarifa ili waliohusika na ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alivunja kamati ya kusimamia huduma maji ya kijiji cha Mpwayungu na alimuagiza Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Chamwino, Godfrey Mbabaye aunde kamati mpya.

Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa kamati hiyo ambayo ilishindwa kutekeleza majukumu yake ikiwemo ujenzi wa vituo vya kuchotea maji licha ya kukusanya Sh. milioni 20 kwa mwezi, mradi huo unavituo vinne tu.

Alisema kitendo cha kamati hiyo kushindwa kuongeza kujenga vituo vingine vya kuchotea maji licha ya kukusanya fedha nyingi kwa mwezi kinasababisha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao ndio wanufaika wa mradi huo.

Pia Waziri Mkuu alimuagiza mhandisi huyo aombe taarifa ya akaunti ya benki ya mradi huo ili kubaini katika mfuko wa mradi huo una fedha kiasi na ndipo aunde kamati mpya ya maji ambayo anatakiwa ashirikishe wanawake kwa kuwa wao ndio wahusika wakuu.

Habari Kubwa