Majaliwa: Agizo upunguzaji kodi sekta ya uvuvi limetekelezwa

22Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa: Agizo upunguzaji kodi sekta ya uvuvi limetekelezwa

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, amesema Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015 -2020 ilielekeza upunguzaji wa kodi kwenye sekta ya uvuvi, na agizo hilo limetekelezwa.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa, akimkabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya chama hicho ya 2020-2025 mgombea ubunge Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kwenye mkutano wa kampeni uliyofanyika viwanja vya Bukima, Musoma Vijijini Mkoa wa Mara jana.

Alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Bukima, wilayani Musoma, mkoani Mara katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Majita.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, aliwaombea kura pia mgombea ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na madiwani wengine wa wilaya hiyo.

Mgombea udiwani wa kata ya Bukima, Januari Simla alipita bila kupingwa.

"Katika kutekeleza Ilani ya CCM, tumepunguza kodi kwenye malighafi na zana za uvuvi, kwenye injini za uvuvi, nyuzi za kushonea nyavu za kuvulia samaki, vifungashio na kwenye ada za leseni za kuvulia samaki," alisema.

Akielezea mambo mengine yaliyofanyika kwenye sekta hiyo, amesema kazi kubwa iliyofanyika ni kuwatambua wavuvi na kuwaweka kwenye vikundi kazi ambayo alisema imesaidia kuongeza vikundi hivyo kutoka 37 hadi kufikia 113.

"Ni kwa nini tuliamua kuwaweka kwenye vikundi ni kwa sababu inakuwa rahisi kuwafikia, kuwaelimisha na kuwahudumia. Hii imefanikisha idadi ya samaki wanaovuliwa iongozeke kutoka 415,000 hadi 800,000."

Alisema kiwango cha uvuaji samaki kimeongezeka kutoka tani 300 na kufikia 448, 467. "Kikubwa ninachowaomba ni kwamba, tumieni vyombo vya kisasa kuvua samaki ili kutunza mazalio yao."

Akiwa njiani kuelekea Musoma Mjini, Majaliwa katika kata za Kusenyi, Mugango na Mkirira, pia aliwaombea kura wagombea wa urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM.

Habari Kubwa