Majaliwa aipa TAKUKURU maagizo mazito

13Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Majaliwa aipa TAKUKURU maagizo mazito

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha Watanzania hawarubuniwi ili watumie vizuri utashi wao wa kisiasa kuchagua viongozi bora.

Alitoa agizo hilo jana alipofungua jengo la Intelijensia TAKUKURU Makao Makuu, Dodoma na kuwasihi watumie vizuri ofisi hiyo kukusanya taarifa muhimu za kiintelijensia zinazowahusu wagombea, vyama au wananchi watakaojihusisha na rushwa kwenye uchaguzi mkuu.

“Sote tunatambua kuwa Oktoba, mwaka huu, taifa letu litaendesha uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo mna jukumu zito la kuhakikisha Watanzania hawarubuniwi na msimwonee au kumpendelea yeyote kwa maslahi yenu binafsi,” alisema.

Waziri Mkuu alisema wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 28 na kwamba wana wajibu wa kuchagua serikali bora na kiongozi bora atakayewaletea maendeleo.

“Chagueni kiongozi mwenye maono, aliyetenda na atakayetenda. Tayari tumeshuhudia mking’ata baadhi ya wagombea waliojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye hatua za awali za uteuzi wa wagombea kupitia vyama vyao. Msiache, endeleeni kukaza uzi na kuwadhibiti wote wenye kujihusisha na vitendo hivyo,” alisisitiza.

“Niungane pia na Mhesimiwa Rais John Magufuli kuwasihi wanasiasa na wagombea wenzangu wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, tuache kutumia rushwa kwa lengo la kununua uongozi,” aliongeza.

Alisema kuelekea uchaguzi mkuu ni vyema Watanzania na viongozi wakazingatia nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika moja ya hotuba zake alipowataka wajiulize kwamba mgombea anayetumia rushwa kununua kura amepata wapi fedha hizo na je, akipata uongozi, fedha hizo atazirudishaje?

“Kwa hivyo, nasi ifike mahala tuwahoji hawa wanaotutia doa. Je, wewe mwenzetu unayetumia rushwa kununua uongozi umepata wapi fedha hizo? Na je, tukikuchagua, utarejesha vipi fedha hizo? Nitoe wito kwa Watanzania wote, msikubali kuwachagua wagombea wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi,” alisema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na watendaji wa TAKUKURU kwa kusimamia vyema mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ndani na nje ya serikali.

Alisema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti wa matumizi ya ovyo ya fedha za umma, kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuziba mianya ya ukwepaji kodi.

Pia alisema ni lazima wafanye uchunguzi wa kutosha juu ya matumizi ya fedha zote za umma na kujua kama matumizi hayo yanaenda sambamba na matakwa ya kisheria na pale ambapo watabaini ukiukwaji wa sheria wachukue hatua.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa miongoni mwa mambo yaliyopewa uzito mkubwa na serikali ya awamu ya tano ni kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Rais Magufuli amemudu kurejesha imani ya Watanzania kwa watumishi wa umma na zaidi ya yote amerejesha uwajibikaji. Ni ukweli usiopingika kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kulikabili tatizo la rushwa na ufisadi ndani ya taifa letu,” alisema.

Ufunguzi huo ulihudhuliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika; na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo.

Wengine Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mary Mwanjelwa, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kicheere, Katibu Mkuu Ikulu, Dk. Moses Kusiluka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge na maofisa wengine wa serikali.

Habari Kubwa