Majaliwa akagua kiwanda cha barakoa cha MSD

09May 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Majaliwa akagua kiwanda cha barakoa cha MSD

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Mei 9, 2022 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vya kutengeneza barakoa na dawa vilivyopo katika eneo la MSD, Keko jijini Dar es Salaam, ambapo amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD.

Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa bila ya mikataba halali jambo ambalo siyo sahihi.

Pia amesema taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.52 kwa wazabuni sita bila ya kufuata utarabu na wala kuitaarifu bodi ya zabuni ya MSD.

MSD ilifanya zabuni 23 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.55 zilifanywa nje ya Mfumo wa Ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na PPRA kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi.

“MSD ilifanya malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 14.89 kwa wazabuni watano (5) bila ya mikataba yoyote au makubaliano mengine ambayo yanabainisha msingi wa malipo ya awali.” Amesema Waziri Mkuu huyo.

Habari Kubwa