Majaliwa amtuma CAG Bukoba kumaliza mgogowo wa viwanja

16Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa amtuma CAG Bukoba kumaliza mgogowo wa viwanja

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenda Bukoba kufanya upya tathmini na kukagua ugawaji wa viwanja 843 kwenye manispaa hiyo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Majaliwa alitoa agizo hilo juzi alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mayunga, mjini Bukoba.

Alifikia hatua hiyo baada ya wananchi kubeba bango lenye ujumbe kuelezea kutopewa viwanja vilivyopimwa na Manispaa ya Bukoba. Viwanja hivyo vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi ambao baadhi yao baada ya kulipa fedha, hawajapewa kwa takriban zaidi ya miaka 10 sasa.

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu alilazimika kumpandisha jukwaani Mkurugenzi wa Mtendaji wa Manispaa hiyo, Wallace Karia, ili atoe maelezo juu ya nini kimekwamisha wananchi kupewa viwanja hivyo.

Katika maelezo yake, Karia alisema mwaka 2003, vilitengwa viwanja 843, kati ya hivyo 352 vilikuwa eneo la yabitembe, 137 Ihungo na Rwome na vingine 132.

Karia ambaye hana muda mrefu tangu ahamishiwe katika manispaa hiyo, alisema kumbukumbu za ofisi zinaonyesha uwa viwanja 182 ndivyo wahusika hawajapewa, na viwanja vingine 85 vilikuwa havijapimwa eneo la Kilimahewa na Kashai, huku kukiwa na vingine 5,000 vya mradi.

Aliongeza kuwa walitarajiwa kuwalipa wananchi hao katika mwaka wa fedha wa 2016/17; kauli ambayo ilisababisha kelele kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa Waziri Mkuu.

Kutokana na hilo, Waziri Mkuu aliingilia kati na kumweleza mkurugenzi huyo kuwa kelele hizo zinaashiria watu hawajaridhishwa na majibu yake.

Alisema anafahamu kuwa mkurugenzi huyo na meya ni wapya, lakini akawaagiza ndani ya mwezi mmoja, kufanya mapitio ya viwanja hivyo 843, na hasa watu 182 ambao hawajapatiwa viwanja wahakikishe wanawapatia
kwa sababu viwanja vipo.

“Rais mstaafu alikuja hapa na kupewa kilio cha kupunjwa fedha. Najua wakati huo mtasema ninyi hamkuwepo. Wewe na Meya wako mkae na kupitia mikataba na mafaili. Nyie na mkoa mkae pamoja na kujua vile viwanja vilivyochukuliwa na JWTZ (Jeshi la Wananchi wa Tanzania). Nitamleta CAG hapa, ndani ya mwezi mmoja afanye mapitio ya viwanja tu,” alisema.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia aliwahakikishia wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuwa watalipwa fidia zao baada ya kukubali kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 31.

Habari Kubwa