Majaliwa amwakilisha Rais mkutano wa SADC

28Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Majaliwa amwakilisha Rais mkutano wa SADC

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa aliondoka jana nchini kwenda Gaborone, Botswana kuhudhuria Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa Double Troika ya Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama, utakaofanyika leo.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akisalimiana na rais john magufuli

Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Gaborone (GICC).

Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Botswana, Sir Ian Khama na utajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini Lesotho. Mkutano huu ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu ambao ulifanyika jana.

Pia mkutano huo utahudhuriwa na Marais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye mwenyekiti aliyetoka wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama, Jacob Zuma , Jacinto Filipe Nyusi wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama.

Wengine ni Mfalme Mswati III wa Swaziland ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SADC, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Mwenyekiti anayeondoka wa SADC.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Aziz Mlima na maofisa wengine waandamizi.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa