Majaliwa anusa ufisadi bil. 129/-

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
RUVUMA
Nipashe Jumapili
Majaliwa anusa ufisadi bil. 129/-

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amenusa harufu ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kueleza kuwa hajaridhishwa na matumizi ya Sh. milioni 129 zilizotolewa kwa ajili ya kazi hiyo.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,

Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile, kufuatilia ili kumbaini mtu aliyehusika katika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo kisha kumpelekea taarifa.

 

Majaliwa alibaini harufu hiyo ya ufisadi jana alipotembelea hospitali hiyo na kukagua ukarabati wa jengo la wajawazito wanaosubiri kujifungua (mama ngojea) ambalo umegharimu Sh. milioni 129.

 

“Sijaridhishwa na gharama za ukarabati wa jengo hili kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kwani serikali inajenga vituo vya afya vyenye jengo la maabara, jengo la kujifungulia, wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, nyumba ya watumishi kwa gharama za Sh. milioni 400 hadi 500.  Sasa  inawezekajane jengo moja linalokarabatiwa ligharimu kiasi hicho?” alihoji.

 

Alisema kila mtumishi wa umma lazima azingatie maadili ya kiutumishi na kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na serikali. Alisema serikali imeagiza miradi ijengwe kwa kutumia ‘force account’ na kuhakikisha miradi inalingana na thamani ya fedha.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma za watoto walio chini ya miaka mitano zinazotolewa katika hospitali kwa kuwa baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatoza gharama za dawa wakati wanatakiwa watibiwe bure.

 

Waziri Mkuu alisema hayo baada ya Kanisia Fusi ambaye amelazwa na mtoto wake katika hospitali hiyo kumweleza kwamba ameandikiwa dawa na kuambiwa akanunue wakati mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu anatakiwa atibiwe bure.

 

Baada ya Dk. Ndugulile kuangalia cheti cha mtoto huyo, alisema dawa aliyoandikiwa iko hospitalini hapo jambo ambalo lilithibitishwa na Mganga Mfawidhi wa Hopitali hiyo, Dk. Majura Magafu, hivyo Waziri Mkuu kumwagiza mganga huyo amtafute mtendaji aliyemwambia mama huyo akanunue.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu jana alizundua mpango wa usambazaji wa x-ray za kidigitali ambazo zitasambazwa kwenye hospitali mbalimbali za rufani za mikoa ili kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mionzi.

 

Waziri Mkuu alisema kwa kuanzia x-ray hizo zitasambazwa kwenye hospitali za rufani katika mikoa 11 na baadaye kwenye hospitali zingine 20 ili kuhakikisha  hospitali zote za rufani za mikoa zinakuwa na huduma hiyo.

 

 

Habari Kubwa