Majaliwa aonya wakiukaji maadili

07Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Korogwe
Nipashe
Majaliwa aonya wakiukaji maadili

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mtumishi wa umma asiyetaka kufuata maadili ya utumishi na maelekezo ya viongozi wake, hafai kufanya kazi katika serikali ya awamu ya tano.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, picha mtandao

Majaliwa aliyasema hayo juzi jioni alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Korogwe akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Alisema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma nchini, hivyo aliwataka watumishi wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Waziri Mkuu alisema serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ya kiutumishi na kwamba haitamvumilia mtumishi ambaye ni mwizi, mbadhilifu, mvivu na haitasita kumchukulia hatua.

“Watumishi mnatakiwa muwahudumie wananchi bila ubaguzi wa aliyenacho na asiyekuwa nacho kwa sababu wananchi wote wana haki sawa ya kuhudumiwa, hivyo hakuna sababu ya kuwabagua,” alisema.

Pia Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa, kuwasimamia wakuu wa idara katika kupanga ratiba za kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili.

Kuhusu upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama, Waziri Mkuu alisema serikali ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo hilo na kuwataka wananchi waendelee kuwa na subira wakati suala hilo linashughulikiwa.

Waziri Mkuu alisema serikali kupitia kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya majisafi na salama karibu na makazi yao.

Pia alisema maeneo yote nchini yakiwamo ya Wilaya ya Korogwe, yatasambaziwa umeme kupitia mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema wakati wa usambazaji wa huduma hiyo, wananchi hawatawajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa kuwa tayari gharama hizo zimeshabebwa na serikali.

“Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama ya sh. 27,000 tu,” alisisitiza.

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava, na mwenzake wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, waliishukuru serikali kwa kuboresha huduma za afya na elimu. Pia waliiomba iwasaidie katika kutatua changamoto za barabara, maji na umeme.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa shamba la ufuta Mkomazi na kujionea miundombinu ya umwagiliaji.

Pia Waziri Mkuu alizindua miradi ya ghala la kuhifadhia nafaka Mombo na kuifungua maktaba ya Chuo cha Ualimu Korogwe.

Habari Kubwa