Majaliwa asema serikali haijazuia barakoa

21Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Majaliwa asema serikali haijazuia barakoa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali haijakataza uvaaji wa barakoa na kusisitiza zivaliwe katika shughuli za kutoa huduma kwa watu walio ndani ya umbali wa chini ya mita moja.

Majaliwa aliyasema hayo jana katika misa ya kuaga mwili wa aliyekuwa  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, iliyofanyika Korogwe mkoani Tanga kabla ya maziko yaliyofanyika siku hiyo.

“Nimeona leo (jana) tabia ambayo tuliizungumza hata mwaka jana. Watu  wana tabia ya kunawa, wananawa kwa kutumia kitakasa mikono (sanitizers), wengine wamevaa barakoa.

“Barakoa utaivaa pale ambako unajua shughuli zako siku hiyo zitakupelekea (zitakusababishia) kupata au kutoa huduma na wengine walioko ndani ya umbali wa chini ya mita moja ambako kunapunguza hatari ya kutema mate, unyevunyevu. Hapo  unaweza kuvaa hakuna aliyekataza, muhimu kila mmoja aende kwa tahadhari,” alisema.

Majaliwa aliwasihi Watanzania wakati dunia ikiwa kwenye mahangaiko ya maambukizi ya maradhi mbalimbali, wawe watulivu na kwamba serikali inawapenda.

“Tumejikita kuhakikisha tunafuatiliana kuona mwenendo wa magonjwa haya. Tuna  magonjwa mengi, tuna malaria, UKIMWI, tuna shinikizo la damu, sukari, magonjwa chungu nzima. Wataalam wetu kwenye hospitali, maabara wanaendelea na uchunguzi na kujikita kutoa huduma. Rais ametusihi kipindi hiki, tuendelee kuzingatia masharti ya afya,” alisema.

Juzi, Rais John Magufuli aliwaomba Watanzania kuondoa hofu na kuwataka  viongozi wa dini kuongoza kufunga siku tatu na kuendelea na maombi.

“Ninawashukuru nimeshuhudia jana (juzi) swala za Ijumaa wameanza kutekeleza kwa kuzungumza na waumini kuliombea taifa. Hata  leo (jana) Wasabato nimeona kwenye vyombo vya habari walioko kanisani wanaliombea taifa. Ninaomba  Baba Askofu nanyi muwe na maandalizi ya kuliombea taifa kesho (leo),” alisema.

Majaliwa alisema wamesikia kwenye mitandao kila mmoja anasema lake na wale wenye simu zinazoonyesha taarifa wameona mataifa mbalimbali yakieleza hiyo ni vita iliyoanza kwa wakubwa na bado wanahangaika nayo.

“Mataifa madogo lazima tuwe makini. Bahati nzuri tuna Rais makini sana na ameendelea kutuongoza vizuri ametusihi tuondoe hofu, muhimu ndani tunaendelea kupambana kuhakikisha usalama wa watu wetu unaendelea kuwapo.

“Barakoa mnazozivaa wakati huo tulisema ni bora tukajiridhisha zinatoka wapi. Bora  ukatengeneza yako au iliyotengenezwa Tanzania. Barakoa  ni nguo inayozuia mate yasitoke au ukapokea vitu vingine. Tumeona  hata kwenye mitandao wakieleza hili na lile, lazima tuwe makini na tufuate masharti ya afya,” alisisitiza.

KIJAZI AENZIWE

Majaliwa alisema wanalo jukumu kubwa la kumuenzi Kijazi hasa watumishi wa umma wameachiwa somo zuri kwa yale mema aliyoyatenda wakati wa utumishi wake.

“Kwa yote mema yaliyotamkwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa serikali, Bunge na viongozi wa dini, jukumu la kumuenzi ni letu sote hatuna namna ametuachia misingi imara,” alisema.

Majaliwa aliwashukuru viongozi wa dini kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwaeleza kuwa serikali inatambua mchango wao wanaoutoa kulifanya taifa kuwa tulivu na watu wake waendelee kushirikiana.

Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson, akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitoa pole kwa familia na ndugu na kueleza kuwa Balozi Kijazi si tu ametoa mchango kwa serikali na Bunge bali pia kwa kanisa.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alisema wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama walikuwa karibu na Balozi Kijazi ambaye pia alikuwa Katibu wa Baraza la Usalama na wao ni wajumbe.

“Kabla ya kwenda kujadiliwa kwenye Baraza la Usalama, ilikuwa lazima zichambuliwe na sekretarieti ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wetu. Tulikuwa  karibu sana katika kuratibu masuala yote ya usalama wa nchi na alikuwa mahiri akiongoza kwa upole, unyenyekevu, weledi mkubwa na tulinufaika kwa kuishi kwake duniani,” alisema Jenerali Mabeyo kwa niaba ya wakuu wa vyombo vya usalama.

Alisema ameibua utashi wa namna gani na wao wataishi kwa weledi na kutaka waliobaki watafakari wanaishi au wanakuwepo duniani.