Majaliwa asema Tanzania si ya kuchezewa

14Sep 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa asema Tanzania si ya kuchezewa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini, Mousa Farhang.

“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi wawe makini na waendelee kuidumisha amani yetu,” alisema.
 
Alisema kwa sasa serikali iko katika mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya na uhujumu uchumi.
 
Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, serikali imeendela kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.
 
Majaliwa alisema mbali na kuimarisha amani nchini, pia serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha wanaotaka kuwekeza nchini kupata tija.
 
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Iran ili kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwamo  vya kuchakata mazao ya  kilimo.
 
Pia aliwakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko Tanzania kama Mlima Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.
 
Naye Balozi Farhang  aliipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.
 
Balozi huyo alisema serikali ya Irani iko tayari kushirikiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na vitendo vingine vya kihalifu.
 
Balozi Farhang alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Tanzania ifungue ofisi ya ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo na Waziri Mkuu alikubali ombi hilo.
 
Pia Farhang alisema aliwahi kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema ni maeneo mazuri ambayo hajawahi kuyaona tangu azaliwe.
 

Habari Kubwa