Majaliwa ataja amani, utulivu

13Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa ataja amani, utulivu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za ibada kuwahamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Amesema serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija.

Waziri Mkuu alitoa rai hiyo wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu baada ya kumaliza kuswali swala ya Eid El Hajj katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam jana.

“Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo mjini Makka na Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada ya Hijja warudi salama.

Pia Waziri Mkuu amewaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla ya watu 16 walifariki dunia na wengine 253 kujeruhiwa.

Aidha, maelfu ya wananchi hawana makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Awali akisoma hotuba ya Eid, Sheikh Nurdin Kishki alisema Uislamu ni dini ya amani, hivyo amewaomba Waislamu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwamo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Sheikh Kishki alisema ni muhimu watu kulinda amani kwa kuwa ikitoweka ni vigumu kuirudisha na kutolea mfano wananchi wa Libya na Misri ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha.

Alisema mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya umwagaji wa damu, kudhulumu mali za watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake, atakuwa ameangamia.

Kwa msingi huo amewataka Watanzania kujiepusha navyo hususan wakazi wa Temeke.

“Temeke sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao, wanauawa bila ya hatia," alisema.

Katika hatua nyingine, Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Amewaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa lisonge mbele.

“Ndugu zangu, tumepewa heshima kubwa leo kuswali Eid na Waziri Mkuu tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga.

Hii inaonyesha ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini,” alisema.

Habari Kubwa