Majaliwa ataja sifa kupigiwa kura 2020

13Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Tanga
Nipashe
Majaliwa ataja sifa kupigiwa kura 2020

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, amewataka wananchi kujitokeza kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kulinda tunu za taifa ikiwamo amani na muungano.

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA:PICHA NA MTANDAO

Alitoa rai hiyo jana alipomwombea kura mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli, mgombea ubunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini.

“WanaTanga bila ya kujali itikadi za vyama nipo hapa mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa ninawaomba ifikapo Oktoba 28, mwaka huu, tumchague Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha.

"Pia ninawaomba tumchague Ummy Mwalimu katika nafasi ya ubunge katika jiji letu la Tanga pamoja na wagombea wa udiwani wa CCM," Majaliwa alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa wamchague tena Dk. Magufuli kwa sababu ni kiongozi shupavu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi na asiyekubali kuyumbishwa na yeyote.

Alisema kuwa Dk. Magufuli ni kiongozi mwenye kuwajali Watanzania na atakayewaruhusu waendelee kuabudu kwa uhuru na ndiyo maana hata uchaguzi umepangwa kufanyika siku ya Jumatano ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuabudu.

Majaliwa alisema Sh. bilioni 66.8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Tanga hadi Pangani yenye urefu wa kilometa 50, ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa katika jiji hilo ni pamoja na ujenzi wa dampo la kisasa katika eneo la Mpirani Chongoleani ambapo Sh. bilioni 8.9 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa eneo la udhibiti wa taka ngumu na tayari ujenzi umekamilika.

Majaliwa alisema Sh. bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi kwenye stendi ya mabasi ya Jiji la Tanga. Alisema ujenzi unaendelea na upo katika hatua ya umwagaji zege katika ghorofa ya pili.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2020/21, Halmashauri ya Jiji la Tanga imepanga kutumia Sh. bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mabawa-Msambweni II na barabara ya 11 na ya 12 kwa kiwango cha lami na sasa utekelezaji wake uko katika hatua za awali.

Habari Kubwa