Majaliwa atoa siku 15 hospitali kukamilika

21Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
pm
Nipashe
Majaliwa atoa siku 15 hospitali kukamilika

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kwa uongozi ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Shirika la Uzalishaji Mali la Suma JKT, kuhakikisha ujenzi wa hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino, unakamilika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya Uhuru, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma jana. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge. PICHA: OWM

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inazinduliwa na Rais John Magufuli, ifikapo Desemba 9, mwaka huu.

“Nimeridhika na hatua hii ya ujenzi lakini haitoshi, hamieni hapa, huu ni wakati wa kazi, hakikikisheni kazi inafanyika usiku na mchana ili Desemba 5, 2020 kazi ikamilike na Desemba 9, 2020 izinduliwe,” alisema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa anataka kuona vifaa vyote vya ujenzi wa hospitali hiyo vinatoka kwenye viwanda vya ndani, ili kuharakisha ukamilishwaji wa hospitali hiyo hasa marumaru, kwani kuna viwanda vikubwa nchini vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa ubora. 

“Mnabishana kuhusu uwekaji wa marumaru, mnataka za nje? TBA mnang’ang’ania kununua marumaru kutoka nje ya nchi, kwa nini? Sisi tumehamasisha ujenzi wa viwanda na viwanda vipo vinavyotengeneza marumaru tena nzuri,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Tuna kiwanda Chalinze kikubwa sana na kingine kipo Mkuranga, hata jengo letu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeweka marumaru za ndani, na bora mshitiri hujazinunua, na usinunue kutoka nje, tuna viwanda vipo nchini,” amesisitiza Majaliwa.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMSEMI), Mhandisi Joseph Nyamhaga, alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilolitoa kuwa Sh. milioni 995.1 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya uhuru mwaka 2018, zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.
Pia, Januari 2019, wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza kiasi cha Sh. bilioni 2.415 zitumike kwenye ujenzi huo.

Alisema hadi kufikia Novemba 19, mwaka huu, Sh. Bilioni 4,430 zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, kwamba kati ya kiasi hicho Sh. milioni 368.411 hakijatumika.

Alisema kwa mwaka 2020/2021, serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 ambazo kila moja imetengewa Sh. bilioni moja.

Aidha, alisema Sh. bilioni 27.75 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati 555, kwamba zahanati tatu zitajengwa kwa kila Halmashauri na kila zahanati inagharimu Sh. milioni 50.

Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanali Laurence Lukema, alisema watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.

   

Habari Kubwa